24.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

‘MARIA MANYAMA’ Msichana wa kwanza kitaifa mwenye ndoto ya udaktari bingwa wa moyo


VERONICA ROMWALD– DAR ES SALAAM

“NDOTO ya kuwa daktari bingwa wa moyo, nimekuwa nayo muda mrefu, ilichochewa zaidi na mazingira ambayo nilikuwa nikiishi kila siku hasa nilipokuwa nikisoma huko Mbeya.

“Kila tulipofanya ziara za kimasomo hospitalini, nilikuwa najisikia huzuni, nilipoelezwa kuhusu idadi kubwa ya vifo vya watoto na watu wazima vinavyotokana na magonjwa ya moyo.

“Huwa nakosa raha kabisa, kwa kweli hali ile ndiyo iliyochochea nia niliyokuwa nayo moyoni mwangu kwamba lazima nisomee na nibobee katika udaktari wa moyo,” ndivyo alivyoanza kunieleza Maria Manyama (17), nilipokutana naye kwa mara ya kwanza katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Maria aliyekuwa akisoma Shule ya Sekondari St. Francis Girls ya Mbeya, ni miongoni mwa wanafunzi 10 bora waliohitimu kidato cha nne mwaka 2018.

Ameshika nafasi ya tatu kitaifa na akiwa msichana pekee aliyeshika nafasi ya kwanza kitaifa katika matokeo yaliyotangazwa hivi karibuni na Baraza la Taifa la Mitihani (Necta).

Februari Mosi, mwaka huu alifika JKCI akiwa ameambatana na walezi wake, lengo hasa likiwa ni kujifunza kwa vitendo namna wataalamu wa taasisi hiyo wanavyofanya kuchunguza na kutibu magonjwa ya moyo.

“Ndicho kilichonileta huku leo, kujifunza… kwa sababu ya maono yangu niliyonayo kwamba baada ya masomo nije kuwa daktari bingwa wa moyo, hivyo nimekuja hapa kujifunza kwa vitendo, kujionea namna ambavyo wataalamu wanafanya.

“Nimeamua kuja ili nijionee jinsi ambavyo madaktari waliopo hapa ambao tayari wamebobea katika kuchunguza na kutibu moyo wanavyofanya katika kusaidia watu wanaokabiliwa na magonjwa haya.

“Nataka kujifunza ‘knowledge’ walioyonayo jinsi wanavyoitumia kusaidia, angalau na mimi nijifunze kitu kutoka kwao, ili ninapokwenda shuleni kuanza masomo yangu ya kidato cha tano, nisome nikiwa tayari nina kitu kinachonipa msukumo wa dhati kutoka ndani.

 “Nataka nijifunze changamoto gani ambazo huwa wanakabiliana nazo na jinsi gani huwa wanazitatua ili na mimi nitakapokuwa shuleni nikisoma nijue niweke msukumo zaidi wapi katika kujifunza ili baadaye niimarike zaidi kusaidia wagonjwa.

“Kwa sababu katika mazingira yale niliyoishi niliona hakukuwa na msaada mkubwa ambao watu wanaokabiliwa na magonjwa haya walikuwa wakiupata.

“Nikawa naona ni changamoto kubwa ndiyo maana nikapata msukumo zaidi wa kujifunza ili nije kuongeza nguvu ya kusaidia watanzania wenzangu wanaokabiliwa na magonjwa haya,”anasema.

Je ni bahati nasibu? 

MTANZANIA lilihoji iwapo kufaulu kwake ni tendo la bahati nasibu au alilitarajia kulingana na historia yake ya kimasomo na au jinsi alivyokuwa amejiandaa kwa mtihani huo.

“Siwezi kusema kwamba matokeo haya ni bahati nasibu au ni kwa sababu nilijiandaa mno kuliko wenzangu au rekodi yangu ya nyuma kimasomo inanibeba kwa sababu ya kufanya vizuri darasani.

“Hapana, kwangu naona hii ni neema ambayo Mwenyezi Mungu amenipatia, ingawa ni kweli nimekuwa nikifanya vizuri darasani tangu darasa la tano nimekuwa nikishika namba za juu.

“Kwa hakika Mwenyezi Mungu amenisaidia, nilihakikisha pia naweka juhudi katika masomo yangu, kwani kadiri mtu anavyoongeza juhudi kwenye masomo ndivyo anavyojiweka pia kwenye nafasi ya kufanya vizuri zaidi kwenye ngazi ya Taifa,”anasema.

Muda kwake ni mali

Maria anasema akiwa shuleni alijitahidi anapangilia vema muda wake na kuhakikisha hapotezi hata sekunde moja kwa kufanya mambo yasiyo na maana kwake.

“Nilihakikisha kama ni muda wa kusoma najikita kwenye kusoma, nilipopewa nafasi ya uongozi nilipata changamoto kubwa mno, niliona ni suala ambalo liliingilia muda wangu wa masomo.

“Kwa sababu katika muda ambao nilitaka kujisomea nilikuwa nahitajika kwenye shughuli za kiuongozi, ikabidi nikae chini kutafakari na kujipanga upya.

“Nikapanga ratiba na mikakati upya, nikapangilia muda wa kusoma na nilihakikisha ukifika nautumia ipasavyo, basi ikawa kama ‘motivation’, nikasoma kwa nguvu zaidi kufidia muda ule ambao nilikuwa nautumia kwenye shughuli za kiuongozi, nilijitahidi kutunza muda wangu,” anasema.

Kwanini wasichana ‘hawang’ari’

“Nadhani ni kwa sababu hawajaamua kujiamini na kujikita zaidi katika kile wanachokitaka, wengi naona hawajaweka ‘focus’ katika jambo moja, utaona wapo ambao wanatamani vitu vingine ambavyo kwa wakati huo si vya msingi kwao.

“Kwa mfano unakuta mtu anataka kupendeza, kuiga kuwa kama watu wengine, wanakimbilia mahusiano, wanataka kuonekana kwenye mitandao, wengine wanataka waonekane wanajua vitu vingi zaidi lakini wanashindwa kabisa ‘ku-focus’ mambo ya msingi,”anasema.

Amshangaza Daktari

Ziara ya Maria ni jambo lililomshangaza Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Magonjwa Shirikishi na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa JKCI, Dellila Kimambo.

“Ni mara ya kwanza kuona jambo hili, ingawa najua kwa kawaida kuna ziara za kimasomo lakini kwa binti huyu imekuwa tofauti, yaani amekuja kujifunza ili anapokwenda shuleni awe tayari ana uelewa wa kumsaidia.

“Nimeambiwa ni msichana wa kwanza kitaifa, nampongeza kwa hatua hiyo, nadhani ni wakati mwafaka kwa jamii yetu kujifunza, si tu kwa fani ya udaktari bali hata zile nyingine, kuna umuhimu wa kipekee kufanya ziara za namna hii.

“Ni jambo ambalo nadhani linafaa kuigwa na wengine, hii inasaidia kumjenga katika msingi ulio mzuri na iwe kwa fani zote, kwani atakapokwenda shuleni atakuwa akijifunza kwa moyo na huku akiwa na picha halisi ya kile anachokitarajia kufanya katika maisha yake.

“Hatua hii itasaidia vijana wetu wanapokwenda kujifunza shuleni wanakuwa na jambo la msingi ndani yao linalowapa msukumo wa kujifunza zaidi na hata kuibua mambo mapya zaidi.

“Kwa msingi huu, nimekubali kuwa mlezi wa Maria, nitahakikisha namsaidia popote pale atakapokuwa akihitaji msaada ili aweze kufikia ndoto yake,”anasema.

Baba mlezi

Baba mlezi wa Maria, Leonard Manyama anasema walipokea kwa furaha kubwa matokeo ya binti yao huyo yalipotangazwa na Necta.

“Ni binti ambaye alianza kutushangaza siku nyingi kabla hata hawajafanya mtihani husika, alitushirikisha kuhusu ndoto yake hiyo, hakika ni mtu ambaye anapenda kuchunguza mambo.

“Tangu akiwa mdogo amekuwa akijituma katika kila kazi aliyopangiwa, aliifanya kwa ufasaha na anapomaliza hurudi na kutoa ripoti,”anasema.

Anasema kabla hata hajafanya mtihani wa kumaliza kidato cha nne, Maria alianza kutafuta kwenye mtandao shule itakayofaa kwenda kusoma kidato cha tano na sita.

“Akatueleza kulingana na matokeo ya miaka mitano iliyopita, anaona shule inayomfaa ni Feza Sekondari, tukashangaa mno, yaani ameweza kufanya uchambuzi ambao hata sisi watu wazima hatukufikiria.

“Tukasema tupo tayari hata kula ugali wa mchicha kila siku, kuhakikisha tunampeleka huko akasome, tukaamua kumuweka karibu zaidi ili kumsaidia, matokeo yalipotoka tulistaajabu, amefaulu kwa kiwango cha juu na uongozi wa Feza umekubali kumsomesha bila malipo.

“Kwa kweli sisi kama wazazi na walezi wake tumemlea kwa muda mrefu ana kipaji na uwezo mkubwa wa kujituma na kuishi kwa malengo, tabia ambayo alianza nayo muda mrefu tangu akiwa mdogo.

“Tulibaini ana kipaji maalumu, tukahakikisha tunamlipia ada na kumpeleka kwenye shule nzuri, tukamuweka karibu na imani, tukiamini asipokuwa karibu na Mungu ataharibikiwa.

“Tulijiweka karibu naye, hakuna jambo atatuficha au tutamficha, kila siku tunamsihi siri kubwa ya urithi wake ni elimu, hakika ametuelewa, amefanyia kazi hilo na ametupa heshima kubwa mno ya kuwa wa kwanza kitaifa,” anasema.

Manyama anatoa rai kwa wazazi na walezi nchini kubadilika na kuwathamini watoto wa kike, kwani nao wanao uwezo mkubwa sawa sawa na watoto wa kiume.

“Watoto wa kike ni majasiri, wanajielewa, wanajituma, jambo la msingi ni kujenga nao mahusiano mazuri ili watushirikishe hata pale wanapokutana na vishawishi, lakini si kujenga uadui kati yao na sisi,”anatoa rai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles