WASHINGTON, MAREKANI
Serikali ya Marekani imetishia kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), ikiwa itaendelea na mikakati yake ya kuwashtaki raia wake.
Mahakama hiyo kwa sasa inatathmini kuwafungulia mashtaka wanajeshi wa Marekani kwa madai ya kuwatesa wafungwa nchini Afghanistan.
Mshauri wa masuala ya usalama ya taifa, John Bolton, amesema mahakama hiyo si halali na kuapa kuwa Marekani itafanya kila iwezalo kuwalinda raia wake.
Marekani ni kati ya nchi kadhaa ambazo hazijajiunga na ICC ilihali imekuwa mstari wa mbele kushinikiza viongozi fulani wa mataifa mengine hasa Afrika kushtakiwa.
Novemba mwaka jana, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Fatou Bensouda alisema kuna sababu za msingi za kuamini kwamba uhalifu dhidi ya ubinadamu ulifanyika katika vita nchini Afghanistan, tangu uvamizi ulioongozwa na Marekani mwaka 2001.
Bensouda alisema uchunguzi makini wa awali umemfanya aamini kwamba vigezo vyote vya kisheria vipo kuwezesha kuanza kwa uchunguzi.
Lakini Bolton ameonya iwapo waendesha mashtaka wa ICC watajaribu kuanzisha uchunguzi huo, Marekani italipiza kisasi kwa kuwalenga majaji na waendesha mashtaka wa mahakama hiyo.
Hiyo ni pamoja na kuwapiga marufuku kukanyaga ardhi ya Marekani na kutumia mfumo wake wa fedha.
Mshauri huyo wa Rais Donald Trump alitishia pia kuwafikisha katika mahakama za nchi yake watendaji hao wa ICC.
Vile vile alisema nchi yake itaziwekea vikwazo kampuni zitakazoshirikiana na mahakama hiyo yenye nchi wanachama zaidi ya 120.
Tisho hilo linakuja huku mwaka uliopita ukishuhudia nchi tatu za Afrika; Burundi, Gambia na Afrika Kusini zikionyesha nia ya kujitoa kutoka mahakama hiyo na kulikuwa na hofu kuwa nchi zaidi zingefuata.
Oktoba mwaka juzi, Burundi na Afrika Kusini zilimwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuelezea uamuzi wao wa kuondoka ICC.
Taifa jingine la Gambia lililopo magharibi mwa Afrika lilitangaza kuwa lingejitoa kabla ya kufuta uamuzi huo baada ya kuingia madarakani Serikali mpya.