MAREKANI YAMTAJA MFADHILI WA ISIS

0
999

WASHINGTON, MAREKANI


HATIMAYE Wizara ya Fedha nchini Marekani imemwekea vikwazo na kumtangaza mtu hatari zaidi raia wa Kenya, Waleed Ahmed Zein, kama mmoja wa watu wanaofadhili kifedha kundi la kigaidi la Islamic State au ISIS, ambalo limehusika na mashambulizi katika nchi mbalimbli za barani Asia na baadhi za Ulaya na Amerika.

Zein alikamatwa jijini Nairobi Julai baada ya uchunguzi kubaini kuwa amekuwa akitoa ufadhili huo ambao kwa mujibu wa sheria za Marekani, yeye ni gaidi na anafadhili hujuma zinazofanywa na magaidi.

Taarifa ya nchi hiyo imeeleza kuwa kati ya mwaka 2017 na 2018 alituma Dola 150,000 kusaidia shughuli za kundi hilo nchini Syria, Libya pamoja na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Kenya imekuwa mshirika wa karibu wa Marekani katika vita dhidi ya ugaidi tangu mwaka 1998, wakati Ubalozi wa Marekani uliposhambuliwa jijini Nairobi.

Hivi karibuni, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, alizuru Marekani na kukutana na Rais Donald Trump, ambaye aliahidi kuendeleza ushirikiano wa karibu wa kupambana na ugaidi na taifa hilo la Afrika Mashariki.

Marekani pia imekuwa katika mstari wa mbele kuungana na Kenya kupambana na kundi la kigaidi la Al Shabab nchini Somalia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here