Serikali ya Marekani imekamata meli ya mizigo ya Korea Kaskazini iliyokuwa ikitumika kusafirisha makaa ya mawe kinyume na vikwazo vya Marekani na Umoja wa Mataifa.
Maafisa wa Marekani wamesema waliikamata meli hiyo kwa jina Wise Honest jana Alhamisi wakati wahudumu wake walipojaribu kuficha kuelezea nchi ilikotokea, na kwa sasa inashikiliwa na Marekani.
Hii ni mara ya kwanza kwa Marekani kuchukua hatua kama hiyo dhidi ya Korea ya Kaskazini.
Hatua hiyo inaweza kuongeza mivutano kati ya nchi hizo mbili wakati ambapo mazungumzo kuhusu mpango wa silaha za nyuklia za Korea Kaskazini yamekwama.