23.8 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

MAREKANI YAJITOA MPANGO NYUKLIA IRAN, ULAYA KUULINDA

BRUSSELS, UBELGIJI



VIONGOZI wa Ulaya wametangaza wataendelea kuunga mkono makubaliano ya nyuklia ya Iran muda mfupi baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza kujitoa kutoka mkataba huo.
Wakati Umoja wa Mataifa (UN), Ulaya, Iran, Urusi na China zikiishangaa Marekani, Israel na Saudi Arabia zimeshangilia uamuzi wake huo.

Licha ya uamuzi wa Trump, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimeapa kufanya kazi pamoja na mataifa yote yaliyosalia katika mkataba huo huku zikiitaka Marekani kutovuruga utekelezwaji wake.

Mataifa mengine yaliyosaini mkataba huo wa 2015 ni Urusi na China, ambazo zimesema pia zitaendelea kuyaunga mkono kutokana na manufaa yake kwa dunia.

Juzi Rais wa Iran, Hassan Rouhani alisema watashirikiana na mataifa ya Ulaya ,China na Urusi kunusuru makubaliano hayo bila uwapo wa Marekani.

Aidha jana, Kiongozi wa Kiroho wa Iran, Ayatollah Ali Khamanei aliilaani Marekani kwa uamuzi wake huo huku wabunge wa Iran wakichoma moto bendera ya Marekani kwa uamuzi wake huo.

Bila kufafanua Ayatollah Ali Khamenei alimtuhumu Rais Trump kwa uongo na kuonya nchi yake haipaswi pia kuziamini Uingereza, Ufaransa na Ujerumani.

Makubaliano hayo ya 2015 yaliizuia Iran kuendelea na mpango wake wa nyuklia huku UN ukikubali kuiondolea vikwazo vilivyowekwa pamoja na, Marekani na Ulaya.
Katika taarifa yake kwenye runinga juzi, Rais Trump alisema Marekani inajiondoa katika mkakati huo wa pamoja (JCPOA).

Aliutaja kuwa mkataba mbaya unaopendelea upande mmoja na ambao haungeweza kufikiwa.
Mbali na kutaka kuilinda Marekani na washirika wake, alisema mkataba huo umeweka masharti hafifu kuhusu mipango ya nyuklia ya Iran na kwamba haikuwekewa vikwazo vyovyote kuhusu nyendo zake ikiwamo nchini Syria, Yemen na kwingineko.
Rais huyo aliongezea kuwa makubaliano hayo hayakuangazia utengezaji wa silaha za masafa marefu za Iran.
Amesema kuwa atarudisha vikwazo vya kiuchumi dhidi ya taifa hilo ambavyo vilikuwa wakati makubaliano hayo yalipotiwa saini mwaka 2015.

Wizara ya Fedha Marekani imesema vikwazo vya kiuchumi havitawekwa dhidi ya Iran mara moja bali baada ya kipindi cha kati ya miezi mitatu na sita ijayo.

Mshauri wa masuala ya usalama wa Taifa nchini Marekani John Bolton ameripotiwa akionya mataifa ya Ulaya yanayofanya biashara na Iran yatalazimika kuisitisha katika kipindi cha miezi sita la sivyo ziwekewe vikwazo na Marekani.

Aliyekuwa Rais wa Marekani Barrack Obama ambaye alichukua jukumu kubwa katika makubaliano hayo alisema katika mtandao wa Facebook kuwa makubaliano hayo yanalinda maslahi ya Wamarekani.

”Kujiondoa katika makubaliano hayo ya pamoja kunaiweka Marekani katika hali mbaya na washirika wake wa karibu katika makubaliano ambayo wajumbe wakuu wa taifa letu, wanasayansi na wapelelezi wetu walijadiliana na kuafikia”, alisema.

Lakini Saudi Arabia ambayo ni hasmu mkuu wa Iran pamoja na Israel kupitia Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu zimeeleza kuunga mkono hatua ya Trump kujiondoa kutoka katika mkataba huo walioutaja janga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles