24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Marekani yajitoa mkataba wa nyukilia

WASHINGTON, MAREKANI

WAZIRI wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Mike Pompeo ametangaza kuwa serikali ya nchi hiyo inajitoa kwenye mkataba wa kudhibiti matumizi ya silaha za nyukilia duniani na kuongeza kuwa Urusi imeshindwa kuheshimu utekelezwaji wa mkataba huo, hivyo basi inauvunja rasmi.

Kwa mujibu wa Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani, imesema kuwa Mike Pompeo ametangaza kuwa nchi yake inajitoa kwenye mkataba kati yao na Urusi ambao unazuia urutubishaji wa silaha za nyukilia tangu kumalizika kwa vita baridi.

Kujiondoa kwa Marekani kumekuwa kukitarajiwa kwa miezi kadhaa sasa. Hatua hiyo imetokana na mzozo ambao haujasuluhishwa kwa miaka mingi wa madai kuwa Urusi imekuwa ikikiuka mkataba huo ulioafikiwa mwaka 1987 ambao unapiga marufuku baadhi ya makombora ya kufyatuliwa ardhini. Urusi imekana madai ya kukiuka mkataba huo.

Taarifa ya Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Mike Pompeo ilionyesha kuwa nchi hiyo inatarajia kujitoa rasmi kwenye mkataba huo jana, akiongeza kuwa ikiwa Urusi haitarudi katika njia ya kuheshimu utekelezwaji wa mkataba huo, basi utavunjika. 

“Tuliipa Urusi muda wa kutosha wa kurekebisha mienendo yake na kujitolea kikamilifu kuheshimu mkataba wa INF. Muda huo unamalizika kesho(jana) lakini Urusi imekataa kuchukua hatua yoyote ya kurejesha hali halisi na inayoweza kuthibitishwa ya kuheshimu mkataba katika kipindi cha siku 60 tulizoipa. Kwa hivyo kuanzia kesho (jana), Marekani itajiondoa kwenye mkataba huo’,” alisema Pompeo

Maafisa wa Marekani wameelezea wasiwasi kuwa China ambayo si mwanachama wa mkataba huo, imekuwa ikijiwekea makombora mengi barani Asia, hatua ambayo Marekani haiwezi ikazuia kwa sababu ya mkataba huo.

Pompeo ameongeza kuwa nchi yake ingali inataka kushiriki katika mazungumzo na Urusi kuhusu udhibiti wa silaha na inatumai Urusi itaheshimu utekelezwaji wa mkataba huo

Madai dhidi ya Urusi yametokana na hatua ya Urusi kutengeneza makombora ya ardhini aina ya 9M729, lakini ambayo Urusi inashikilia kuwa hayana uwezo wa kufyatuliwa kupita umbali unaokubaliwa na mkataba huo.

Mapema mwezi Disemba, mwaka jana, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Mike Pompeo alitangaza kuwa Marekani ingeipa Urusi siku 60 kurejea katika hali ya kuuheshimu mkataba huo, kabla iipe notisi rasmi ya kujiondoa hatua ambayo itakamilika baada ya miezi sita.

Mkataba huo ambao pia unajulikana kwa Kiingereza kama Intermediate-Range Nuclear Forces (INF), ulikuwa hatua ya kwanza ya kupiga marufuku kabisa aina ya makombora ya ardhini yanayoweza kufyatuliwa umbali wa kati ya kilomita 500 hadi kilomita 5,500.

Kuachana na mkataba wa INF kunaruhusu utawala wa Rais Trump kuikabili China japo haijabainika wazi ni vipi utafanya hivyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles