29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, September 19, 2024

Contact us: [email protected]

Marekani yaingilia kati Zanzibar

maalim seif (3)*Ni baada ya matokeo kufutwa, wataka tamko liondolewe

*Makamishna wa ZEC wataka kuzichapa kavukavu

NA SARAH MOSSI, ZANZIBAR

SAA chache baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kutangaza kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa rais, wawakilishi na madiwani visiwani Zanzibar jana, Serikali ya Marekani imeingilia kati na kutaka tamko hilo liondolewe.

Serikali ya Marekani imesema imeshtushwa sana na tamko la Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, kufuta matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar.

Katika tamko lake, ubalozi wa Marekani nchini, umesema hatua hii inasitisha mchakato wa uchaguzi uliofanyika vizuri na kwa amani, kama ilivyoelezwa na waangalizi wa uchaguzi kutoka Ubalozi wa Marekani,  Jumuiya ya Ulaya, Jumuiya ya Madola na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika pamoja na kusitisha zoezi la majumuisho ya kura lililokuwa linakaribia kukamilika.

“Tunatoa wito wa kuondolewa kwa tamko hilo na kuzisihi pande zote kudhamiria kwa dhati kuukamilisha mchakato huu wa kidemokrasia kwa uwazi na kwa amani. Watu wa Zanzibar wanastahili jambo hilo,” ilieleza taarifa hiyo iliyotumwa na ubalozi wa Marekani nchini kwa vyombo vya habari.

Awali Mwenyekiti wa ZEC, Jecha, alisema kuwa wameamua kufuta uchaguzi huo baada ya kubaini kasoro tisa, ikiwamo kuchezewa kwa matokeo katika Kisiwa cha Pemba.

Akitangaza uamuzi huo mjini Unguja mbele ya waandishi wa habari, Jecha, alisema wamelamizika kufuta uchaguzi huo na matokeo yake yote hasa ya rais wa Zanzibar, Wawakilishi na madiwani baada ya kukabiliwa na vikwazo vingi katika kutekeleza majukumu yao.

Mwenykiti huyo wa ZEC, alivitaja vikwazo tisa alivyokabiliana navyo ambavyo alidai vimechangia kuchelewesha matokeo ndani ya muda uliopangwa kisheria.

Alisema kutokana na hali hiyo, kuliibuka mizozo na kutoelewana kwa makamishna wa ZEC hali iliyofikia wengine kuvua mashati na kutaka kupigana.

Jecha alisema ni dhahiri baadhi ya wajumbe badala ya kuwa makamishna wa tume, waligeuka kuwa wawakilishi wa vyama vyao vya siasa.

“Na ikumbukwe kuwa vipo vyama vingi zaidi ambavyo havikupata fursa ya kuwa na makamishna ndani ya tume na vimeshiriki katika uchaguzi huu mkuu,” alisema Jecha.

Alitaja vikwazo vingine vilivyoikanili tume ni kubainika kwa kasoro nyingi katika uchaguzi huo na miongoni mwa hizo ni baadhi ya vituo, hasa vilivyoko kisiwani Pemba kuwa na kura nyingi kuliko idadi ya watu walioandikishwa katika daftari la wapigakura katika kituo husika.

“Hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya wapigakura hawakwenda kuchukua vitambulisho vyao vya kupigia kura,” alisema Jecha.

Pamoja na hali hiyo, alisema taarifa kutoka kwa wajumbe walioiwakilisha ZEC kisiwani Pemba ilieleza kwamba kulifanyika uhamishaji wa masanduku ya kuhesabiwa katika eneo nje ya kituo kinyume na utaratibu.

Alisema mawakala wa vyama vingine hususani wa Chama cha TADEA walitolewa nje ya vituo kisiwani Pemba na kupigwa pamoja na vijana walioandaliwa na vyama vya siasa kufanya fujo, kupiga watu na kuwazuia watu wasiokuwa wa vyama kwenda katika vituo vya kupiga kura.

Mwenyekiti huyo alitaja vikwazo vingine ni vyama vya siasa kuonekana kuingilia majukumu ya tume, ikiwamo kujitangazia ushindi na kusababisha kuwapo shinikizo kwa tume.

Jecha alitaja sababu jinginge kuwa ni kuwapo malalamiko mengi kutoka vyama mbalimbali yanayoashiria kutoridhika na mchakato mzima wa upigaji kura pamoja na kuhesabu na kutoa matokeo ya uchaguzi.

“Na kikwazo cha tisa ni kuonekana kufutwa na kuandikwa upya kwa nambari katika fomu za matokeo ya vituo vingi kisiwani Pemba, lakini nambari hizo zikiandikwa juu ya zilizofutwa.

“Kwa kuzingatia hayo na mengine ambayo sijayaeleza, mimi nikiwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, nimeridhika kwamba uchaguzi huu haukuwa huru na wa haki.

“Kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za uchaguzi, hivyo kwa uwezo nilionao, natangaza rasmi kwamba uchaguzi na matokeo yake yote yamefutwa na kwamba kuna haja ya kuurudia uchaguzi huu,” alisema Jecha.

Mwenyekiti huyo wa ZEC na wanahabari mjini hapa, alitumia dakika mbili kueleza kufutwa kwa uchaguzi huo na kunyanyuka huku akigoma kuulizwa maswali na wanahabari.

Hatua hiyo ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi ni mara ya pili. Januari mwaka 1961 kabla ya kufanyika kwa mapinduzi, pia ulifutwa uchaguzi wa ngazi ya wawakilishi katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Uchaguzi huo ulishirikisha vyama vya Afro Shirazi Party (ASP),  Zanzibar Nationalist Party (ZNP) na Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP).

Matokeo ya uchaguzi huo yalifutwa baada ya kubainika baadhi ya watu kupiga kura zaidi ya mara moja, na hata kusababisha kuzuka kwa vurugu katika eneo la Darajani na kusambaa katika maeneo mengine ya kisiwa cha Unguja.

 

VYAMA VINAVYOSHIRIKI

Vyama vinavyoshiriki uchaguzi wa Zanzibar mwaka huu ni CCM, CUF, TADEA, NRA ADC, Demokrasia Makini, Jahazi Asilia, DP, TLP na AFP.

 

KATIBA YA Z’BAR

Pamoja na ZEC kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, Ris aliyemaliza muda wake, Dk. Ali Mohammed Shein, ataendelea na wadhifa wake huo kwa mujibu wa katiba.

Katiba ya Zanzibar kifungu cha 28 (1) ya mwaka 1984 inatamka kuwa rais aliyepo madarakani ataendelea kuwa rais mpaka (a) Rais anayefuata ale kiapo cha urais (b) au afariki akiwa rais (c) au hapo atakapojiuzulu au (d) iwapo amechaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na (e) kwa sababu yoyote nyingine ameacha kuwa kiongozi kwa mujibu wa vifungu vingine vya katiba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles