
WASHINGTON, MAREKANI
MAREKANI jana iliadhimisha mwaka wa 15 tangu wapiganaji wa Kiislamu walipoendesha mashambulizi katika ardhi yake Septemba 11, 2001 na kusababisha vifo vya watu 3000.
Katika Ikulu ya hapa, Rais Barack Obama aliadhimisha shambulio hilo saa mbili na dakika 46 asubuhi muda ambao ndege ya kwanza iliyotekwa nyara ilibamiza moja ya majengo pacha ya Kituo cha Kimataifa cha Biashara (WTC) mjini New York.
Baadaye majina ya waathirika wote yalisomwa katika ibada ya kumbukumbu katika eneo la Ground Zero ambako jengo hilo la WTC lilianguka.
Shambulio hilo lilisababisha kuanza kwa vita dhidi ya ugaidi pamoja na uvamizi wa Marekani nchini Afghanistan na Irak, huku kukizuka mashambulizi zaidi ya kigaidi kuanzia Asia hadi Ulaya na Amerika.
Ndege tatu za abiria zilizotekwa nyara ndizo zilizotumika kubamiza majengo pacha ya mjini New York pamoja na jengo la makao makuu ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, nje ya Washington.
Ndege ya nne iliyotekwa nyara ilianguka mashambani huko Pennsylvania baada ya abiria kupambana na watekaji wa ndege hiyo.