MAREKANI: TUTATUMIA NGUVU DHIDI YA KOREA KASKAZINI

0
550
Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, akifurahia na wanasayansi na mafundi sanifu wa Chuo cha Sayansi cha Kijeshi cha taifa hilo, baada ya uzinduzi wa kombora la masafa marefu lenye uwezo wa kuipiga Marekani, mjini Pyongyang mapema wiki hii.
Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, akifurahia na wanasayansi na mafundi sanifu wa Chuo cha Sayansi cha Kijeshi cha taifa hilo, baada ya uzinduzi wa kombora la masafa marefu lenye uwezo wa kuipiga Marekani, mjini Pyongyang mapema wiki hii.

WASHINGTON, MAREKANI

SERIKALI ya Marekani imesema itatumia nguvu za kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini kutokana na jaribio la kombora la masafa marefu lililotekelezwa na taifa hilo.

Balozi wa Marekani, Nikki Haley, alisema uamuzi mpya pia utawasilishwa dhidi ya Pyongyang katika Umoja wa Mataifa (UN).

Jaribio hilo la kombora, ambalo ni la hivi karibuni miongoni mwa majaribio mengine, linakiuka katazo lililowekwa na Baraza la Usalama la UN.

Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, James Mattis na mwenzake wa Japan, Tomomi Inada, walisema jaribio hilo ni uchokozi ambao hautakubalika.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Marekani, imesema wawili hao walizungumza kwa simu na Jenerali Mattis alisema nchi yake itaendelea kuilinda Japan.

Aidha Haley alisema jaribio la kombora la masafa marefu la Korea Kaskazini, ambalo lina uwezo wa kupiga Jimbo la Alaska, Marekani, linakwamisha juhudi za uwezekano wa mazungumzo ya kidiplomasia.

“Marekani imejiandaa kutumia uwezo wake wote kujilinda na washirika wetu,” aliliambia baraza hilo, ambalo lilikutana kwa kikao cha dharura kuzungumzia hatua hiyo ya Korea Kaskazini.

Hata hivyo, Balozi wa China katika UN, Liu Jieyi, amekiambia kikao hicho kuwa suluhu ya nguvu za kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini haifai kupewa kipaumbele.

Badala yake, Jieyi alirejea wito wa China na Urusi kuwapo mazungumzo ya kusitisha majaribio ya makombora iwapo Marekani na Korea Kusini zitasitisha mazoezi ya pamoja ya kijeshi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here