Mazungumzo ya kibiashara kati ya Marekani na China yanatarajiwa kuanza tena masaa machache kabla ya Marekani kuziongezea ushuru bidhaa za Kichina, huku mvutano ukizidi kati ya mataifa hayo yenye uchumi mkubwa duniani.
Maafisa wa mjini Beijing wamesema leo kwamba watalipiza kisasi iwapo Rais Donald Trump wa Marekani ataziongezea ushuru bidhaa za China, lakini hawakutaja watachukua hatua gani hasa.
Mazungumzo hayo yanayoanza tena leo yalivurugika mapema wiki hii baada ya waziri wa fedha wa Marekani, Steven Mnuchin, na ofisa mwengine anayehusika na mazungumzo hayo, Robert Lighthizer, kuishutumu China kwa kutotekeleza ahadi zake ilizozitoa awali.