NAIROBI, KENYA
SERIKALI ya Kenya imesema imemchagua kwa bahati mbaya mwanaume mmoja aliyefariki mwaka mmoja uliopita kuwa kiongozi wa bodi ya filamu ya Kenya (KFCB).
Robert Kochalle alifariki dunia mwezi Mei mwaka jana lakini alikuwa ni kati ya watu watatu waliochaguliwa kwa ajili ya uongozi wa bodi hiyo, ambayo inasimamia filamu na habari.
Katika mitandao ya kijamii, wakenya wameonyesha kuchukizwa na jambo hilo na kudai kuwa ni ishara ya uzembe katika kusimamia masuala ya taifa hilo.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya filamu, Ezekiel Mutua, amesema kuwa hilo lilikuwa ni kosa dogo sana ambalo linakuzwa kuwa kubwa.
Mutua alieleza kuwa kosa hilo linaweza kuwa limesababishwa na mfanyakazi mmoja kujichanganya katika uhamishaji wa nyaraka za ofisi ya KFCB kutoka ofisi moja ya serikali hadi nyingine.
Baadhi ya wakenya kwenye mitandao bado hawajafurahishwa na sababu anazozitoa Mutua, Huku wengine wakiuliza kama waliomba ruhusa yake kabla ya kumchagua tena.