23.8 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

MARANDO AIBUKA BAADA YA SIKU 973


Na EVANS MAGEGE-DAR ES SALAAM

MWANASHERIA wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mabere Marando, ameibuka ghafla Jumanne ya wiki hii, ikiwa ni baada ya kupita siku takribani 973 za kutokuonekana hadharani na katika matukio ya kijamii na kisiasa.

Marando ambaye ni mwanaharakati wa siasa za vyama vingi na gwiji wa sheria nchini, aliungana na viongozi wengine wa Chadema ambao walifika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu kushuhudia ukamilishaji wa dhamana ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe pamoja na viongozi wenzake saba ambao walikuwa mahabusu wakikabiliwa na kesi ya uchochezi na kuhamasisha maandamano yaliyosababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.

Akiwa katika mwonekano wa furaha huku baadhi ya watu wakimsogelea kwa kumsabahi, Marando kwa mwendo wa pole alijongea hadi walipokuwapo mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, ambapo alishikana nao mikono kwa furaha na kuteta mambo kadhaa.

Kabla ya tukio hilo la Jumanne, gwiji huyo wa sheria na siasa za upinzani hakuwahi kuonekana hadharani kwenye shughuli za kisiasa za Chadema tangu Septemba mwaka 2015, baada ya kuugua ghafla ambapo alipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, baadaye kupelekwa nchini India kwa matibabu zaidi.

 

Hata hivyo, haijawahi kuwekwa wazi ugonjwa uliokuwa ukimsumbua Marando ingawa taarifa zaidi zinadai kwamba alitibiwa nchini India na kurejea kwa ajili ya kuendelea na mazoezi madogo madogo ya kumsaidia kuimarisha afya yake.

Siku chache kabla ya kuugua ghafla, Marando aliwaahidi wafuasi wa upinzani kuwa atatangaza matokeo ya uchaguzi kila kituo kitakapomaliza upigaji wa kura kabla ya kutangazwa na Tume ya Uchaguzi (NEC).

Alisema njama zote zinazotumiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) za kutaka kuhujumu matokeo, zikiwamo za kukusanya shahada za polisi na wanajeshi wameshazigundua na wamejipanga kuzikabili.

“Njama zote walizonazo kutaka kujaribu kuhujumu kura za Lowassa, wabunge na madiwani pamoja na kuhujumu kura za Zanzibar tutazidhibiti, nawaambia mawakala baada ya kupiga kura tu msisubiri saa 12, nitumieni saa saba mchana nitatangaza matokeo, mheshimiwa usiwe na wasiwasi, endelea na kazi yako,” alisema Marando.

Alisema ofisi ya sheria ya chama hicho imejipanga kulinda kura za wagombea wote na hakuna atakayeibiwa mwaka huo.

Pamoja na kutoa msimamo huo, lakini Marando alishindwa kutimiza azma yake hiyo baada ya kuugua ghafla siku 11 kabla ya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2015 kuanza.

Hatua hiyo ilisababisha awe kando na majukumu ya kichama wakati wa zoezi la upigaji kura hadi kutangazwa kwa matokeo ya kura za Rais zilizompatia ushindi mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli, huku upande wa Zanzibar ukilazimika kurudia uchaguzi.

Marando ni miongoni mwa wanasiasa wa kwanza wa upinzani nchini na alikuwa mmoja wa waanzilishi wa jukwaa la Katiba la NCCR na kisha chama cha siasa cha NCCR-Mageuzi mwaka 1992.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles