22.7 C
Dar es Salaam
Friday, August 12, 2022

Maradhi ya mahusiano janga kwa familia

Na ELIYA MBONEA

-ARUSHA 

MAHUSIANO mabaya kati ya mume na mke, wazazi na watoto na wakati mwingine wanafamilia, yanatajwa kuwa ni maradhi mapya yanayozitafuna kwa kasi familia nyingi.

Kutokana na kuwapo kwa maradhi hayo ndani ya familia, jamii imekumbushwa kuchukua tahadhari za kuonana na wataalamu ili kuepuka kusambaratika. 

Hayo yalibainishwa juzi jijini hapa katika maadhimisho ya Siku ya Taaluma ya Ustawi wa Jamii, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid. 

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Dk. Naftali Ng’ondi, alisema taifa linapaswa kujengwa katika misingi ya kuwa na familia bora pamoja na mila zinazoheshimu utu wa mtu. 

“Tumeshiriki matembezi ya maadhimisho ya Siku ya Taaluma ya Ustawi wa Jamii kuikumbusha jamii kuacha vitendo vya kikatili ili kuwe na familia njema. 

“Ukiangalia katika familia na jamii zetu utaona watu wazima wanatumia muda mwingi zaidi katika maeneo ya starehe kunywa pombe na anasa nyingine. 

“Watu hawa hawawezi kuwahi majumbani kwa ajili ya kukaa na watoto na kuzungumza na familia, hii yote ukiangalia kwa ndani ni tatizo la maradhi ya uhusiano,” alisema Ng’ondi. 

Aidha, Ng’ondi aliwaomba maofisa ustawi kutoa kipaumbele katika fani yao ili kuwezesha familia nyingi kuwa bora. 

Akielezea kuhusu umuhimu wa fani hiyo, Ng’ondi alisema katika Mkoa wa Arusha taaluma hiyo ina umuhimu sana kwani mkoa huo una watoto takribani 50,000 wanaoishi katika mazingira hatarishi. 

“Pengine ndiyo maana mkoa huu unaongoza kwa kuwa na vituo vingi vya kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi,” alisema Ng’ondi. 

Kwa upande wake, Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Arusha, Denis Mgupe alisema kuanzia Januari hadi Desemba mwaka jana majalada 132 yalifikishwa mahakamani na kufanyiwa kazi. 

“Mwaka 2017/18 watu 1,437 walifanyiwa ukatili katika Mkoa wa Arusha, huku wahanga wakubwa wakiwa ni wanawake na watoto. Hii ni kwa wale waliofika kwenye maeneo rasmi kutoa taarifa,” alisema Mgupe. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,580FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles