33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mapokezi Yanga si ya kitoto

Theresia Gasper-Dar es salaam

KIKOSI cha Yanga kinatarajia kuwasili leo jijini Dar es Salaam, saa 12 jioni, kikitokea Morogoro kilikokuwa kimeweka kambi ya wiki tatu, kujiandaa na msimu ujao, wakikabiliwa na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Ligi Kuu Tanzania Bara na mingineyo ya ndani.

Wakiwa kambini Morogoro, Wanajangwani hao walicheza mechi tano za kirafiki ambazo zote walishinda, huku washambuliaji wao wapya, waking’ara.

Katika mchezo wa kwanza, Yanga iliichapa Tanzanite mabao 10-1, Moro Kids (2-0), ATN FC (7-0), Moro Komaini (3-0) na Mawenzi Market bao 1-0.

Mchezo wao wa kwanza msimu ujao, utakuwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers ya Botswana, unaotarajiwa kuchezwa kati ya Agosti 9 na 11 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya timu hizo kurudiana kati ya Agosti 23 na 25, mwaka huu, nchini Botswana.

Lakini kabla ya kipute hicho cha kimataifa, Yanga inatarajiwa kuumana na Kariobang Shark ya Kenya kwenye Uwanja wa Taifa, keshokutwa, ukiwa ni mchezo wa kirafiki wa kuhitimisha tamasha lao la Wiki ya Wananchi ambalo shamrashamra zake zilianza tangu wikiendi iliyopita kwa wapenzi wa timu hiyo kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii.

Mchezo huo wa keshokutwa dhidi ya Kariobang Shark, utaambatana na tukio la Yanga kuwatambulisha wachezaji wao wapya, akiwamo straika David Molinga kutoka FC Lupopo ya DR Congo, aliyetua nchini katikati ya wiki hii.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alisema kikosi chao kitaondoka Morogoro saa saba mchana na kuwasili Dar es Salaa saa 12 jioni.

“Timu itaingia (Dar es Salaam) jioni na kupokewa na wanachama pale Kibaha na kuongozana kwenye msafafara huo hadi hotelini tutakapoweka kambi,” alisema.

Alisema wanachama mbalimbali wa Dar es Salaam, Kibaha na Mlandizi, watajitokeza kwa ajili ya mapokezi hayo ya wachezaji wao.

Mwakalebela alisema baada ya kuwasili Dar es Salaam, kikosi chao kesho kitaendelea na programu ya mazoezi ya mwisho kwa ajili ya mchezo huo dhidi ya Kariobang Shars.

Mbali ya Molinga, nyota wengine wapya wa Yanga wanaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa klabu hiyo wa Dar es Salaam, ni Farouk Shikalo, Mechata Mnata, Ally Ally, Muharami Issa ‘Marcelo’, Ally Mtoni ‘Sonso’, Mustapha Seleman na Lamine Moro.

Wengine ni Mapinduzi Balama, Abdulaziz Makame, Patrick Sibomana, Issa Bigirimana, Juma Balinya, Sadney Urikhob, Maybin Kalengo wa makinda kutoka timu ya vijana, Omary Abbas na Frank Yohana.   

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles