24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

MAPENZI YASIKUPE UPOFU, UKAMVUMILIA ANAYEKUDHALILISHA  

Na Christian Bwaya


MIAKA mitatu iliyopita, akiwa mwaka wa pili chuo kikuu, Frida alikutana na mchumba wake Fred. Mbali na kuwa kijana mwenye bidii na ndoto kubwa maishani, Fred alikuwa kijana mwaminifu na kwa hakika alionesha mapenzi ya kweli kwa Frida. Mara kwa mara alijitahidi kupata muda wa kukaa na Frida na alimfanya akajisikia mwanamke kweli kweli.

Miezi michache baada ya uhusiano wao kuanza, jambo lisilo la kawaida lilitokea. Fred alikuwa amempigia Frida simu zaidi ya mara 10, lakini bahati mbaya haikupokelewa. Ujumbe aliomtumia haukujibiwa. Jambo hili lilimkasirisha Fred. Usiku huo, akiwa amekasirika, aliondoka hosteli alikokuwa anaishi kwenda nyumbani kwa Frida kujua kilichokuwa kinaendelea.

Frida alikuwa na wenzake watatu wakisoma kwa ajili ya mtihani uliokuwa ufanyike kesho yake asubuhi. Pengine kwa kufikiri kwamba Frida amemdharau, Fred bila hata kuuliza kilichotokea alimfokea mbele ya rafiki zake kwa maneno magumu. Frida alijisikia kudhalilika. Alimwomba Fred aondoke na watazungumza wakati mwingine. Fred hakusikia. Alimshika mkono kwa nguvu na kumvuta watoke nje. Frida aligoma hali iliyoibua ugomvi. Fred alimzaba kibao na kuondoka.

Kwa kushuhudia mtafaruku uliotokea, rafiki zake Frida walimsikitikia na kushauri angeachana na Fred. Huo haukuwa ushauri mzuri na Frida hakuelewa. “Namjua Fred ana hasira, nimeshamzoea. Huwa akikasirika anaweza kufanya vituko. Lakini siwafichi, ana mapenzi ya kweli. Siwezi kumwacha najua atabadilika,” alieleza. Frida hakumwacha. Hatimaye walifunga ndoa na kuanza maisha mapya ya ndoa.

Kama tulivyogusia kwenye makala iliyopita, tabia hasi za mwanadamu, kama ukatili na udhalilishaji, wakati mwingine hujificha kwa muda mrefu. Inaweza kuchukua muda mrefu kufika mahali ukaweza kumbaini mpenzi mwenye tabia za kikatili. Lakini pia, wakati mwingine kama ilivyokuwa kwa Frida, zinaweza kujitokeza dalili za udhalilishaji na bado zikapuuzwa.

Swali ni je, kwanini watu hung’ng’ania wapenzi wakatili? Kwanini mtu kama Frida aliyeshuhudia tabia zisizo za kawaida kwa Fred lakini bado hakuwa tayari kuukabili ukweli na kufanya uamuzi? Sababu zipo nyingi, mojawapo ni upofu wa mapenzi. Mtu mwenye tabia za udhalilishaji anaweza pia kuwa ‘fundi wa mapenzi’ kiasi kwamba kwa yule anayefanyiwa udhalilishaji, wazo la kuchukua hatua mapema linaweza lisiingie kichwani. Mapenzi anayojisikia yanaweza kumfanya mtu akawa kipofu kwa matarajio kuwa kuna uwezekano akabadilika. Bahati mbaya, tabia hizi huwa hazibadiliki kirahisi kama watu wanavyofikiri.

Pili, watu kama Frida huvumilia udhalilishaji kwa sababu ya hofu ya matokeo ya kusitisha uhusiano. Chukulia una mpenzi unayejua ana tabia mbovu lakini unafahamu wazazi, marafiki, ndugu na jamaa zako wanaufahamu uhusiano wenu huo. Katika mazingira ambayo uhusiano wenu unafahamika wazi, na wakati mwingine mtu huyo anaheshimika katika jamii, inaweza kuwa vigumu kuchukua uamuzi mgumu.

Hata hivyo, hatari ya kuvumilia tabia hizi za kikatili ni kujikuta kwenye mazingira ambayo maisha yako mwenyewe yanakuwa hatarini. Kwa Frida, mwaka mmoja baada ya kufunga ndoa na Fred, vipigo vilizidi. Kila walipopishana, Fred alikuwa mwepesi kurusha mkono na kumzaba kibao mke wake. Mara nyingi tatizo lilikuwa wivu usio na kichwa wala miguu. Pamoja na vyote hivyo, bado Frida alivumilia kwa matarajio kuwa mambo yangebadilika. Kilele cha udhalilishaji ni pale Fred alipothubutu kumpiga kofi Frida mbele ya wazazi wake mwenyewe. Ndoa iliishia hapo.

Huenda una mpenzi mwenye tabia kama hizi za wivu uliopindukia, mgomvi, mbabe na mwenye tabia za kuweka vitu moyoni. Mapenzi uliyonayo kwake yanakufanya usite kuchukua hatua kwa matarajio kuna wakati utafika na atabadilika. Huwezi kufikiri maisha bila yeye kwa sababu ni kweli unampenda. Jambo la kukumbuka ni kwamba kama una mpenzi mwenye tabia kama hizi, usifikiri kuna siku atabadilika. Ikiwa uko tayari kuhatarisha maisha yako, endelea kumvumilia. Lakini kama usingependa kudhurika bila kutarajia, chukua uamuzi mgumu mapema.

Ikiwa uko kwenye mazingira ambayo huwezi tena kurudi nyuma kwa mfano, una mke au mume mwenye dalili zote za ukatili lakini huna unachoweza kufanya. Nina ushauri wa aina mbili. Kwanza, fungua macho na acha kukana ukweli. Kubali kuwa kuna tatizo na kwa pamoja msaidiane kutambua kuwa lipo tatizo linalohitaji kushughulikiwa. Pili, tafuteni msaada wa kitaalam mapema. Msiishi kwa matumaini. Nendeni mkapate tiba kabla mambo hayajaharibika ukajikuta kwenye hatari kubwa zaidi. Majuto ni mjukuu, wahenga waliwahi kusema.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Twitter: @bwaya, Simu: 0754870815

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles