23.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

MAPATO MANISPAA ILALA YAPOROMOKA

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

MAPATO ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilala yameshuka hadi kufikia kukusanya chini ya asilimia 50, kwa mwezi.

Sababu zilizotajwa kuchangia hali hiyo ni kunyang’anywa na Serikali kuu jukumu la kukusanya kodi ya majengo na  kufungwa kwa baadhi ya biashara.

Nyingine ni upungufu wa watumishi na marekebisho ya sheria za leseni za biashara, ambapo utaratibu wa sasa wa kupata leseni ni lazima mtu awe na Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN).

Hayo yaliainishwa jana wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo ambacho pia kilijadili taarifa za Kamati ya Kudumu ya Fedha na Utawala na Kamati ya Uchumi na Huduma za Jamii.

Taarifa ya fedha inayoanzia Oktoba hadi Desemba mwaka jana, inaonesha katika kipindi hicho halmashauri hiyo ilijiwekea lengo la kukusanya Sh bilioni 16.3 kwa hesabu za robo mwaka kuanzia Oktoba hadi Desemba mwaka jana, lakini ilikusanya Sh bilioni 12.8.

Akiwasilisha taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, Greyson Celestine, alisema hali ya mzunguko wa fedha ni ngumu, biashara nyingi zimefungwa, wamenyang’anywa kodi za majengo na hata maofisa biashara waliopo hawatoshelezi.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, hadi sasa maofisa biashara waliopo katika halmashauri hiyo ni 24 wakati mahitaji ni 39.

Akizungumza na MTANZANIA jana baada ya kikao hicho, Celestine alisema licha ya ripoti hiyo ya robo mwaka hata katika robo nyingine za mwaka hali ya ukusanyaji mapato haikuwa nzuri.

Alisema kwa mwaka wa fedha 2016/2017 walijiwekea lengo la kukusanya Sh bilioni 83 na kwamba katika kodi ya majengo pekee walitegemea kukusanya Sh bilioni 20, lakini fedha hizo zimekosekana kutokana na Serikali kuu kuchukua chanzo hicho.

“Siwezi kukupa taarifa zinazoonyesha mpaka sasa tumekusanya shilingi ngapi lakini kwa kifupi hali si nzuri, tumekuwa tunakusanya chini ya asilimia 50 na kuna wakati tunakusanya hadi asilimia 35.

“Maduka mengi yamefungwa kama pale Aroma na Segerea yako maduka nayafahamu yamefungwa kutokana na kufilisiwa na benki, watu walikopa wakashindwa kupeleka marejesho,” alisema Celestine”alisema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Msongela Palela, alikiri baadhi ya biashara kufungwa na kwamba wako wafanyabiashara waliotoa taarifa na wengine wameamua kukimbia.

“Si siri hali ya uchumi imekuwa ngumu, wakati wa kupanga bajeti ya mwaka 2016/2017 kuna baadhi vya vyanzo vya mapato vilipitishwa lakini vimeondolewa na kusababisha halmashauri kushindwa kufikia lengo. Pale kwangu (ofisini) kuna mabango ya milioni 200 yameshushwa kwa sababu wahusika wameshindwa kuyalipia.

“Makubaliano yalifikiwa tuendelee kupokea ada za leseni za biashara na kuwapa watu risiti lakini tusitoe leseni, suala hili lilifika ngazi ya kitaifa tukatuhumiwa kutofuata utaratibu wa TIN na kuisababishia Serikali hasara hivyo tukaamua kusitisha,” alisema Palela.

Baadhi ya tozo zilizopitishwa katika bajeti kisha kuondolewa kutokana na changamoto mbalimbali ni pamoja na ada za machinjio na nyingine zilizoko kwenye masoko.

Pia alisema kutokana na changamoto ya uhaba wa watumishi wamelazimika kuchukua maofisa ustawi wa jamii 10 ili wasaidie katika ukusanyaji wa mapato.

“Ajira zilisimamishwa kwa maelekezo ya serikali na sisi tumekwama tunashindwa kuendelea mbele, tuliamua kutafuta watumishi kutoka halmashauri nyingine lakini hili nalo limegonga mwamba haturuhusiwi kuhamisha watumishi,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema wameamua kutumia vikosi kazi ambavyo vinahamasisha wananchi na kupita kila kata kukusanya mapato hivyo kuwapunguzia mzigo wa kuja halmashauri.

Naye Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii na Vijana, Fransisca Makoye, alisema changamoto ya makusanyo ya mapato imewaathiri hasa katika kutoa mikopo ya vikundi vya wanawake na vijana.

Sheria imeelekeza kila halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kukopesha vijana na wanawake ambapo kwa Dar es Salaam fedha hizo zimekuwa zikipitia katika Benki ya DCB.

“Kiasi kilichopangwa kupelekwa kinapungua na katika robo ya mwaka iliyopita tulipeleka Sh milioni 450 lakini bado mahitaji ni mengi, mweka hazina anajitahidi kupeleka fedha kadiri inavyopatikana,” alisema Makoye.

MADIWANI

Diwani wa Kata ya Ukonga, Jumaa Mwaipopo (Chadema), alisema hali ya biashara katika kata yake imekuwa ngumu na hadi sasa maduka 220 yamefungwa.

“Wakati tunaokwenda nao si mzuri, maduka mengi yanafungwa hivyo ni lazima tuwe na mikakati mingine. Hayati Gadafi (Rais wa zamani wa Libya), baada ya kuona mafuta yanapungua aliamua kuanzisha kilimo cha matunda, sisi tunaweza kutafuta eka 400 ama 500 halafu tukaanzisha kilimo cha mtama,” alisema Mwaipopo.

Naye Diwani wa Kata ya Kitunda, Nice Gisunte (Chadema), alisema “Tunaandaa makisio lakini hatufikii lengo, napata shaka kama wataalmu wetu wanafanya kazi sawasawa,” alisema.

Diwani wa Kata ya Kipawa, Kenedy Simion (Chadema), alipendekeza kuwapo na utaratibu wa kupata mapato kutokana na biashara ya pikipiki maarufu kama bodaboda.

Hata hivyo Mbunge wa Segerea, Bonnah Kaluwa (CCM), alipinga hoja hiyo na kudai kuwa biashara hiyo imekuwa suluhisho kubwa la ajira kwa maelfu ya vijana nchini.

“Bodaboda ni watu wetu na ajira hakuna, wanafanya kazi katika mazingira magumu Trafic (Askari wa Usalama Barabarani), Sumatra (Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini) na askari wa jiji wanachukua fedha zao. Na sisi tukiweka utaratibu tutakuwa hatujawatendea haki…ni watu wetu tunawahitaji mwaka 2020,” alisema Kaluwa.

Naye Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), alipendekeza ifanyike tathimini kuonesha miradi iliyokwama na kupendekeza vyanzo vipya vya mapato.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Palela, alisema wana mpango wa kuwaingiza bodaboda na wamachinga na kuwa vyanzo vya mapato ya halmashauri hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles