25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Maombi ya kukamata nyumba ya mchungaji yakwama

Na Faraja Masinde, Dar es Salaam

Maombi ya kukamata nyumba ya Mchungaji wa Kanisa la City Christian Fellowship, Godfrey Mallasy kwa kushindwa kulipa Sh milioni 139 yamekwama kuendelea sababu Naibu Msajili aliyekuwa akisikiliza shauri hilo ameteuliwa kuwa Jaji.

Maombi hayo yametajwa leo Juni 10, 2021 Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi Dar es Salaam mbele ya Msajili Agatha Chagulu badala ya aliyekuwa Naibu Msajili, Safina Semfukwe kuteuliwa kuwa Jaji.

Msajili Chagulu aliahirisha maombi hayo hadi Agosti 9 mwaka huu ambapo Mahakama itakuwa imeshapanga Msajili mwingine wa kuendelea na shauri hilo.

Mchungaji Mallasy anadaiwa kiasi hicho cha fedha za kodi baada ya kushindwa kesi tangu mwaka 2016 ambapo mdai katika shauri hilo ni Prosper Rweyendera.

Awali mdai alishauriwa na mahakama kubadili maombi yake ya kutaka kumpeleka jela Mchungaji Mallasy kwa kushindwa kulipa Sh milioni 139 badala yake awasilishe maombi ya kukamata mali ambayo tayari yako mahakamani.

Mchungaji Mallasy alishindwa kulipa kiasi hicho cha fedha na kuomba alipe Sh milioni 12 huku mdai akitaka kiasi hicho kilipwe kama ilivyoamriwa na mahakama.

Mallasy alidai kwamba kesi ilikuwa ya Kanisa la City Christian Fellowship lililokuwa Sinza Palestina Dar es Salaam, na yeye alikuwa kiongozi lakini baada ya mgogoro huo kumalizika, kanisa lilisambaratika na kubaki yeye peke yake.

Aliomba mdai amsamehe na alipokataa aliomba amlipe Sh milioni 12 ambapo kwa kila mwezi alitaka kulipa Sh 200,000 kwa sababu hana kipato kwani alikuwa anategemea kanisa ambalo kwa sasa halina waumini.

Alidai hivi sasa anapata fedha pindi anapoitwa kwenda kutoa mada. Aliyekuwa Naibu Msajili Semfukwe alimtaka mdaiwa kuangalia anafanyaje ili kulipa hilo deni kwani kesi ipo kwa jina lake

“Wakati hawa wanaendelea kuwasilisha maombi, wewe uangalie namna ya kulipa deni kabla amri ya kukamata nyumba haijatolewa,” alisema Naibu Msajili.

Aprili 2016 Mahakama hiyo iliamuru kanisa hilo liondolewe mara moja na kumuachia mdai eneo lake.

Uamuzi ulitolewa na jaji John Mgeta na hukumu kusomwa na Msajili Richard Kabate.

Pia Mahakama uliamuru Mchungaji Mallasy kulipa kodi ya Sh milioni moja kila mwezi tangu alipoacha kulipa mwaka 2004 wakati wanatumia kanisa hilo lililokuwepo Sinza Palestina kufanyia ibada.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles