Maofisa benki, Brela kizimbaniwakituhumiwa uhujumu uchumi

0
870

NA KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

MSAJILI Msaidizi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), Noel Shani (44), wafanyakazi wawili wa Benki ya Equity na wafanyabiashara wawili, wamepanda kizimbani kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo kughushi na kutakatisha dola za Marekani 300,000.

Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu na kusomewa mashtaka ya uhujumu uchumi na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon.

Wankyo aliwataja washtakiwa kuwa ni Mohammed Nur (48) raia wa Afrika Kusini na Umulkher Mohammed (34) raia wa Somalia ambao wote ni wafanyabiashara.

Wengine ni Msajili Msaidizi Brela, Shani na wafanyakazi wa Benki ya Equity; Alex Ndondole (33) na Emma Chikaonda ambaye hakuwepo mahakamani.

Katika shtaka la kwanza washtakiwa wote wanadaiwa kati ya Machi 2011 na Mei 30, 2016 Dar es Salaam, walikula njama kufanya udanganyifu wa kujipatia fedha kwa udanganyifu.

Shtaka la pili mshtakiwa wa kwanza na wa pili, wanadaiwa kughushi maamuzi ya Bodi ya Kampuni ya Alliance Cargo Handling Ltd ya Februari 8, 2014 kuonyesha kampuni hiyo imekubaliana kufungua akaunti katika Benki ya Equity tawi la Prestige wakati si kweli.

Shtaka la tatu mshtakiwa wa kwanza na pili, Aprili 12, 2015 wanadaiwa kughushi maamuzi ya bodi ya Aprili 12, 2015 wakionyesha kwamba bodi imekubali kufungua akaunti Benki ya Amana Tawi la Nyerere Road.

Wankyo alidai shtaka la nne, mshtakiwa wa kwanza anadaiwa Aprili 18 mwaka 2011 alighushi barua kuonyesha imetolewa na Brela kwa kuonyesha kwamba Mohammed ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Alliance huku akijua si kweli.

Alidai katika shtaka la tano mshtakiwa wa kwanza na pili, wanadaiwa kughushi maamuzi ya bodi ya Machi 5, 2016 wakionyesha Kampuni ya Alliance inabadili jina kutoka Alliance Cargo kwenda Africa Flight Service Tanzania wakati si kweli.

“Shtaka la sita Februari 8, 2014 mshtakiwa wa kwanza aliwasilisha nyaraka ya uongo ya maamuzi ya bodi kuonyesha kwamba wamekubali kufungua akaunti Equity benki.

“Katika shtaka la saba mshtakiwa huyo aliwasilisha nyaraka  Amana benki kuonyesha kampuni imekubaliana kufungua akaunti.

“Mshtakiwa anadaiwa kuwasilisha Brela nyaraka kuonyesha wamekubaliana kubadilisha jina la kampuni,” alidai Wankyo.

Alidai katika shtaka la tisa, inadaiwa Februari 10, 2014 maeneo ya banki ya Equity, mshtakiwa wa kwanza na pili kwa nia ya kufanya udanganyifu katika akaunti ya Kampuni ya Cargo kwa udanganyifu walichukua mkopo wa dola za Marekani 300,000.

Katika shtaka la kumi mshtakiwa wa nne na tano, wanadaiwa kushindwa kuzuia kosa kutendeka, wakiwa maofisa wa Benki ya Equity.

Wankyo alidai shtaka la 11, mshtakiwa wa tatu akiwa Msajili Msaidizi Brela anadaiwa kushindwa kuzuia uhalifu, shtaka la 12 la kutakatisha linamkabili mshtakiwa wa kwanza na wa pili na shtaka la 13 washtakiwa wote wanadaiwa kutakatisha dola za Marekani 300,000.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo la uhujumu uchumi.

Wankyo aliomba washtakiwa warudi Polisi kwa sababu hawajapimwa corona, mahakama ilikubali, washtakiwa walirudi polisi kwa ajili ya vipimo, kesi itatajwa Septemba 7.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here