NA HERIETH FAUSTINE, DAR ES SALAAM
MGOMBEA udiwani wa Kata ya Mbagala Kuu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuph Manji, amesema akishinda atahakikisha anaanza na elimu, afya, kuboresha huduma ya maji na kutoa ahadi kwa vijana.
Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam juzi, wakati wa uzinduzi wa kampeni zake katika Viwanja vya Zakhem.
“Suala la elimu limekuwa tatizo katika kata hiyo, hivyo nitatoa shilingi milioni 200 kila mwaka kwa ajili ya kusaidia kujenga miundombinu ya elimu,” alisema Manji.
Kuhusu afya alisema akipata ridhaa ya kuwa diwani, atahakikisha katika kata hiyo zinajengwa zahanati 20 zitakazotoa huduma kwa saa 24.
“Kwa kutumia kampuni yangu nitachimba visima virefu vya maji ambavyo vitakuwa vinatoa huduma kwa gharama nafuu na fedha zitakazopatikana kupitia mradi huo zitasaidia katika miradi mingine ya maendeleo katika kata hii,” alisema Manji.
Alitaja vipaumbele vyake vingine kuwa ni kujenga soko la kisasa, kuikopesha Halmashauri ya Temeke magari 20 ya kuzoa taka na matrekta matatu.