22.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 31, 2023

Contact us: [email protected]

MANJI AMKATAA WAKILI KIBATALA KORTINI

 

NA KULWA MZEE
-DAR ES SALAAM

MFANYABIASHARA Yusufali Manji (41), anayekabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi, amekataa mbele ya mahakama kutetewa na Wakili Peter Kibatala, kutokana na kile alichosema ni sababu za kisiasa.

Manji alitoa kauli hiyo jana mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu, Isaya Arufani, kabla hajatoa uamuzi wa kutupilia mbali ombi la dhamana la mfanyabiashara huyo ambaye sasa inabidi akaitafute dhamana Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

“Mheshimiwa Jaji, nilipowasilisha maombi ya dhamana nilimpa maelekezo Wakili Joseph Thadayo aniwakilishe, lakini nilishangaa kesi ilipokuja kusikilizwa Wakili Kibatala alikuja kuniwakilisha.

“Sitaki kuwakilishwa na Kibatala kwa sababu za kisiasa, nitakuwa nawakilishwa na Wakili Alex Mgongolwa, Hudson Ndusyepo na Seni Malimi,” alidai Manji.

Hata hivyo, Kibatala na Thadayo wanatoka katika kampuni moja ya uwakili.

Pia Manji ni Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu kupitia CCM, huku Kibatala akiwa ni Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)

Jaji Isaya akitoa uamuzi, alisema mleta maombi hatawakilishwa tena na Wakili Kibatala kwa sababu za kisiasa.

 

OMBI LA DHAMANA

Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi, alidai upande wa Jamhuri wamewasilisha hati kinzani na nia ya kuwasilisha pingamizi la kisheria kuhusu maombi hayo ya dhamana.

Kadushi aliomba kabla ya kuanza kusikiliza maombi ya dhamana, mahakama ianze kusikiliza mapingamizi yao.

Kwa upande wake, Wakili Mgongolwa anayemtetea Manji, alikiri kuwa maombi ya dhamana yaliyowasilishwa na mteja wake, yana dosari hivyo wanakubaliana na mapingamizi yaliyowasilishwa na Jamhuri kwamba yana msingi.

Wakili Kadushi aliomba mahakama kutokana na hoja za upande wa utetezi, maombi ya dhamana yatupwe.

Jaji Isaya akitoa uamuzi alisema: “Mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza maombi ya dhamana, hivyo maombi yaliyowasilishwa yanatupwa.”

 

SABABU ZA KUTUPA MAOMBI

Jamhuri walikuwa na sababu tatu za kutaka maombi hayo yatupwe, ikiwa ni pamoja na kuwa Mahakama Kuu haina mamlaka ya kusikiliza maombi hayo kwa sababu yanapaswa kusikilizwa Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Pia walidai vifungu vya sheria vilivyotumika kuwasilisha maombi si sahihi na hoja ya mwisho ni kwamba hati ya kiapo iliyoambatanishwa kuunga mkono maombi ina dosari ambazo haziwezi kurekebishika.

Katika maombi yaliyotupwa, Manji aliomba mahakama imwachie kwa dhamana kwa sababu ana matatizo ya kiafya, anasumbuliwa na maradhi ya moyo.

Mawakili waliwasilisha vyeti vya daktari kuthibitisha mteja wao ni mgonjwa.

Manji anashtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa uhujumu uchumi, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi. Upelelezi haujakamilika.

Katika kesi hiyo, Manji na wenzake wanakabiliwa na mashtaka saba chini ya sheria ya uhujumu uchumi na usalama wa taifa kwa kukutwa na vitambaa vinavyotengeneza sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 200 na mihuri.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Deogratius Kisinda (28), Abdallah Sangey (46) na Thobias Fwere (43). Kesi itatajwa Agosti 4, mwaka huu.

Hati ya mashtaka inayowakabili washtakiwa hao inadai Juni 30, 2017 katika eneo la Chang’ombe ‘A’, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam kwa pamoja walikutwa na askari polisi wakiwa na bunda 35 za vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za Jeshi la Wananchi Tanzania zenye thamani ya Sh milioni 192.5 ambayo ni mali iliyopatikana kinyume cha sheria.

Katika shtaka la pili, inadaiwa Julai mosi, 2017 Chang’ombe ‘A’, washtakiwa hao walikutwa na polisi wakiwa na mabunda manane ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za Jeshi la Wananchi Tanzania yenye thamani ya Sh milioni 44 mali ambayo yalipatikana isivyo halali.

Katika shtaka la tatu, washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Juni 30, 2017 Chang’ombe ‘A’, walikutwa na muhuri wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania wenye maandishi ‘Mkuu 121 Kikosi cha JWTZ’ bila ya kuwa na uhalali, kitendo ambacho kingehatarisha usalama wa nchi.

Shtaka la nne, anadai kuwa Juni 30, 2017 kwenye eneo hilo la Chang’ombe ‘A’, Manji na wenzake hao watatu walikutwa wakiwa na mhuri wenye maandishi ‘Kamanda Kikosi 834 KJ Makutupora Dodoma’  bila ya kuwa na uhalali, kitendo ambacho kingehatarisha usalama wa nchi.

Manji na wenzake katika shtaka la tano wanadaiwa kuwa Juni 30, 2017 huko Chang’ombe ‘A’, walikutwa na mhuri wa Jeshi la Ulinzi la Tanzania wenye maandishi ‘Commanding Officer 835 KJ Mgambo P.0. Box 224 Korogwe’, kitendo ambacho kingehatarisha usalama wa nchi.

Katika shtaka la sita, washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Julai Mosi, 2017 katika eneo hilo la Chang’ombe ‘A’, walikutwa na askari polisi wakiwa na namba ya usajili wa gari SU 383 ambayo ilipatikana kwa njia isiyo halali.

Katika shtaka la saba, washtakiwa wote wanadaiwa kuwa Julai Mosi, 2017 eneo la Chang’ombe ‘A’, walikutwa na askari polisi wakiwa na namba za usajili wa gari SM 8573 ambayo ilipatikana kwa njia isiyo halali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,205FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles