Mangula awataka vijana kujiunga na VETA

0
886
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula akiangalia moja ya mashine zilizotengenezwa na wanafunzi alipotembelea katika banda la VETA katika maonesho ya Sabasaba leo Julai 12, kushoto kwake ni Meneja Uhusiano wa VETA, Sitta Peter.

Na Asha Bani, Dar es Salaam

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Philip Mangula amewataka vijana nchini kujiunga na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta), ili kupata ujuzi na hatimaye kujiajiri.

Mangula ameyasema hayo leo Julai 12, wakati alipotembelea banda la Veta kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba ambapo amesema ni jambo jema hasa kwa wakati huu ambapo nchi inaelekea katika uchumi wa viwanda.

Amesema amefarijika sana kuona wanafunzi wa aina mbalimbali hata wenye mahitaji maalum wakiwa wanajifuza na kujipatia ujuzi katika chuo hicho.

“Mwanafunzi anasoma kuanzia shule ya msingi mpaka sekondari, kidato cha tano na cha sita lakini hana ujuzi hivyo ni vyema akijiunga na akitoka hapa anakuwa na ujuzi wake tosha kabisa wa kuweza kujiajiri mwenyewe,”amesema Mangula.

Naye kijana aliyejitambulisha kwa jina la Paul Ngonyali, ambaye ni mlemavu wa viungo alimwelezea Mangula jinsi Veta inavyowasaidia katika kuibua vipaji vyao.

“Sisi tusiojiweza tumeona tusibweteke tu baada ya kusikia Veta wanakitengo maalum cha kuwasaidia watu wenye mahitaji nimeamua kuja kujiendeleza  kuliko kukaa na kudharauliwa na jamii kwamba hatuwezi,” ameeleza Ngonyali.

Makamu Mwenyekiti CCM Bara, Philip Mangula (mwenye shati la kitenge) akioneshwa moja ya vitu vinavyotengenezwa na wanafunzi wa VETA Lindi anayemuonesha ni mwalimu wa useremala Ostan Mgaya, wa kwanza kushoto ni Meneja Uhusiano wa VETA, Sitta Peter.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here