25.7 C
Dar es Salaam
Saturday, December 4, 2021

Mangula atoa agizo zito kwa madiwani CCM

ELIZABETH KILINDI-NJOMBE

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula, amewataka madiwani wa chama hicho nchini kuitisha vikao vya halmashauri kuu za kata zao ili kujadili tathmini za utekelezaji wa ahadi mbalimbali zilizotolewa na viongozi wakuu wa kitaifa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Agizo hilo alilitoa juzi wilayani Wanging’ombe mkoani hapa, kwenye kikao cha tathimini cha kazi za CCM.

Alisema jambo hilo likifanyika nchi nzima, litawasaidia wananchi kujua Serikali yao imefanya nini na kuondoa chuki dhidi yake.

“Madiwani muitishe vikao vya halmashauri kuu na mkawaeleze wananchi vitu vinavyotekelezwa, vinavyoonekana kama miradi mbalimbali inayotekelezwa katika kata zenu na kisiwe kitu cha kufikirika, hiyo itaondoa chuki kwa wapigakura.

“Na aliyoyaeleza Mbunge Lwenge (Garson, Mbunge wa Wanging’ombe) hapa muyachukue na kuyapeleka katika  kata zenu mkaeleze juu ya yaliyofanyika katika kipindi cha mwaka mmoja.

“Madiwani mnalo jukumu nanyi kwenye maeneo yenu, mkatoe taarifa kwenye maeneo yenu ya kata kwa kuwa mbunge na yeye ameshatoa taarifa ya jimbo. Mbunge ni wajibu wake sasa, isitokee mtu mwingine akatoa misaada, huyo ni mbabaishaji na ni mgogoro, mbunge ni wakati wako sasa kuwajibika kwa wannachi,’’ alisema Mangula.

Mangula alisema kwa kuwa CCM inaingia kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji mwaka huu, utaratibu wa madiwani hao kwenda kwa wananchi kutawafanya waelewe nini kinachoendelea kwenye kata zao.

“Nawapongeza sana mkuu wa wilaya, mbunge kwa kuwakutanisha viongozi wa kata na mashina wa CCM kuungana na mimi kusikiliza yaliyotekelezwa katika mwaka mmoja.

“Tumeona mafanikio mengi mnayojivunia kama vile afya na maji kwa kuyatangaza kwenye Serikali ya kijiji, hayo ndiyo maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali ya Mitaa,” alisema Mangula.

Kwa upande wake, Mbunge Lwenge alisema katika jimbo lake kuna changamoto kubwa ya maji na kumwomba Mangula amkumbushe Rais kuhusu suala hilo.

Tayari mkuu huyo wa nchi ameidhinisha Sh bilioni 80 za kutatua kero za maji wilayani Wanging’ombe.

“Malengo ya taifa kwa Watanzania ni kupata maji asilimia 85 katika umbali wa mita 400, lakini sisi Wana Wanging’ombe tupo chini katika hizo asilimia,” alisema Lwenge.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe, Jasery Mwamwala, alisema kumekuwepo na ucheleweshaji wa malipo ya utekelezaji wa miradi ya maji kwa wakandarasi na kuiomba Wizara ya Maji ilitazame suala hilo kwa kuwa miradi mingi haiendi.

Katika kikao hicho, Mangula alikabidhi pikipiki mbili kwa Jumuiya ya Vijana ya CCM (UVCCM) zilizotolewa na Lwenge kuanzisha mradi wa kuimarisha jumuiya hiyo kimapato.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,875FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles