28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Maneno ya Nape yanafikirisha

Barnabas Maro

‘FIKIRISHA’ ni fanya au sababisha mtu afikiri. ‘Fikiri’ ni waza kwa kutumia akili ili kuelewa kitu, kufanya uamuzi au kutatua tatizo; tafakari. ‘Fikiria’ ni waza juu ya jambo fulani kabla ya kufikia uamuzi; tilia maanani; tafakari.

‘Maneno ni kama fumo, yakitoka mdomoni hayarudi.’ Maana yake neno analotamka mtu ni kama mkuki, likitoka halirudi na huweza kuleta madhara. Hutunasihi tuwe na tabia ya kuyatafakari maneno tuyasemayo kabla. Ni vizuri kulipima neno kabla ya kulisema na kujiletea majuto baadaye.

Akiwa bungeni hivi karibuni, Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye aliwaambia wenzake: “Tujifunze kidogo kuweka akiba ya maneno, hasa tunaposhutumiana bila sababu …” Ikumbukwe kuwa Nape alijiuzulu uenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii jambo lililoleta suitafahamu (hali ya watu kutoafikiana kimawazo juu ya jambo) kuhusu kujiuzulu mbunge huyo kijana.

Suala la Nape kujiuzulu lilimuibua m-bunge wa Mbozi, (Chadema), Paschal Haonga aliyesema kuwa Nape alijiuzulu baada ya shinikizo lakini alipoambiwa Spika Job Ndugai atoe ushahidi, alishindwa hivyo akalazimika kuifuta kauli yake. Kwa nini alitoa kauli asiyokuwa na hakika nayo? Je, kauli ya Nape kuwa “Tujifunze kidogo kuweka akiba ya maneno hasa tunaposhutumiana bila sababu” ilimhusu yeye?

Naye Mbunge wa Siha aliyejitoa Chadema na kujiunga na CCM, Dk. Godwin Mollel alilieleza Bunge kwa kirefu kuwa vikosi vya kigaidi vya Chadema ndivyo vilivyompiga risasi Tundu Lissu! Kwamba chama hicho cha upinzani kina wafadhili wake nje ya nchi wanaokipatia chama hicho fedha kuratibu shughuli za chama hicho.

Dk. Mollel hakuishia hapo kwani alidai pia kuwa viongozi wa Chadema walimkatalia kupeleka sampuli ya uchunguzi wa tukio la mlipuko wa mabomu Afrika Kusini yaliyotokea jijini Arusha baada ya yeye kuziiba katika uchunguzi. Alisema aliwaambia wenzake kuna vitu ameviiba na atavipeleka kwa mkemia mkuu wa Afrika Kusini, lakini viongozi wa Chadema walikataa. Akauliza humo bungeni ni kwanini walikataa?

Akaendelea: “Wanapinga suala la Lissu? Kilimtokea nini Chacha Wangwe alipotaka kugombea nafasi ya uenyekiti wa Chadema? Kulikuwa na mpango namba moja wa kuzuia Serikali isifanye kazi na katikati ya mpango huo Lissu akapigwa risasi ili kusisimua watu waivuruge Serikali yetu.”

 Dk. Mollel pia alisema anajua kuhusu vikosi hivyo vya Chadema na kwamba anaweza kuthibitisha na kwamba anaweza kuzungumzia popote mahakamani kuwa fedha wanazopata Chadema wanatumia kufadhili vikundi hivyo. Akasema pia anatambua mpango wa vikosi hivyo kutumika ili kumwangamiza lakini anajua havina uwezo huo na mpango wao hautafanikiwa na kamwe hawana uwezo wa kumdhuru wala wasijaribu.

Yote hayo aliyasema bila Spika wa Bunge kumtaka athibitisha madai yake kama alivyotakiwa kufanya Mbunge wa Mbozi (Chadema), Paschal Haonga,  hata ikambidi afute usemi wake. Kwanini Spika hakumtaka Dk. Mollel athibitishe madai yake au kwa kuwa ni wa CCM?

Alisema pia ana mpango wa kuishtaki Chadema kwa kukiuka haki za Tundu Lissu kwa kumzungusha nchi mbalimbali ilhali yungali mgonjwa.

Hapa pana maswali mengi yanayomhusu Dk. Mollel. Kama anajua mipango yote hiyo ya mauaji yaliyoandaliwa na Chadema wakati yeye akiwa mbunge wake, kwanini hakuiarifu polisi ili ichukue hatua stahiki? Kama alikuwa anajua yote hayo, kumbe angeokoa maisha ya Chacha Wangwe, Lissu na kufichua uharamia uliokuwa ukifanywa na chama chake wakati ule? Kwanini aseme sasa baada ya watu kuuawa na Lissu kuponea chupuchupu kuuawa? Kwanini hakutoa taarifa polisi?

Kwanini hakujiuzulu wakati ule ila baada ya mkururo wa madiwani na wabunge wengi wa Chadema kuvutwa kujiunga na CCM? Je, mtu kama huyu anawezaje kuaminika na chama chake alichohamia? Akiachana na chama hicho hatatoa siri zake hadharani kama anavyofanya sasa?

Je, tangu alipotamka maneno yote hayo polisi imechukua hatua gani dhidi yake kwa kuficha uharamia huo uliosababisha watu kadhaa kupoteza maisha na Lissu kuponea chupuchupu kuuawa na chama anachokipigania? Atakuwa shahidi muhimu sana kama ataisaidia polisi kufungua kesi kwa yale anayodai kufahamu. Endapo atashindwa kuthibitisha itakuwaje?      

 “Enyi wazao wa nyoka, mwawezaje kunena mema, mkiwa wabaya? Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake. Mtu mwema katika akiba njema hutoa mema, na mtu m-baya katika akiba mbaya hutoa mabaya. Basi nawaambia: Kila neno lisilo maana watakalolisema wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu. Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.” (Mathayo 12:34-37).

‘Shindana’ ni kitendo cha kupimana uwezo katika jambo. ‘Shindano’ ni tendo la kupimana uwezo katika jambo kama vile mchezo; makabiliano yenye lengo la kuwania jambo baina ya pande mbili au zaidi. Kwa muktadha huu, CCM na vyama vya upinzani vinashindana kuwania kuunda Serikali ambayo sasa inaongozwa na CCM.

Kwa kawaida katika shindano lolote, washindani hupewa nafasi sawa na uwezo wa upande mmoja ndio unaowapa ushindi. Maana hiyo ni kila upande upewe haki sawa na mwingine na wasimamizi watumie haki bila upendeleo. Kinyume chake ni sawa na ghiliba yaani udanganyifu wenye nia ya kuunufaisha upande mmoja na kuudhulumu mwingine.

Wakati vyama vya upinzani vimekatazwa kufanya mikutano ya ndani na nje, viongozi wa CCM wanatembea nchi nzima kunadi sera zao, wakijipongeza, kuwasema vibaya na kuwadharau wapinzani.

Katibu Mkuu wa CCM anatembea nchi nzima kufanya mikutano ya ndani na nje kama ilivyo kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM  Humphrey Polepole, akifanya vivyo bila kutiwa msukosuko na Jeshi la Polisi. Wapinzani wakithubutu kufanya hivyo hukamatwa na kufunguliwa mashitaka ya kufanya mikutano isiyo na kibali na kufanya uchochezi!

Demokrasia ni mfumo wa kisiasa wa kuendesha Serikali iliyochaguliwa na raia kwa manufaa yao; mfumo unaoshirikisha raia katika uamuzi. CCM kipo madarakani kwa kuwa kilichaguliwa na raia kwa manufaa yao. Hii haina maana kuwa chama hicho kutashika madaraka maisha. Lazima utafika wakati kitapoteza umaarufu wake baada ya viongozi wake kulewa madaraka. Je, wakati huo ukifika nao wakafanyiwa kama wanavyowafanyia wenzao wa upinzani watathubutu kulalama?

Wahenga walisema: “Mtenda mema (wema) kwa watu atendea nafsiye.” Anayewafanyia wengine mema huwa kaifanyia nafsi yake hata kama watu hawautambui wema wake. Hutufunza umuhimu wa kuwafanyia wenzetu wema hata kama hawaelekei kuutambua. Labda kuna siku watautambua na kuurudisha wema wao.

“Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, na masikio yake hukielekea kilio chao. Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya, aliondoe kumbukumbu lao duniani. Walilia, naye Bwana akawasikia, akawaponya na taabu zao zote. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, na waliopondeka roho huwaokoa. Mateso ya mwenye haki ni mengi, lakini Bwana humponya nayo yote. Uovu utamwua asiye haki, nao wamchukiao mwenye haki watahukumiwa.” (Zaburi 34: 15-19,21).

“Waaibishwe, wafedheheshwe, wanaoitafuta nafsi yangu. Warudishwe nyuma, wafadhaishwe, wanaonizulia mabaya. Wawe kama makapi mbele ya upepo, malaika wa Bwana akiwafuatia.Njia yao na iwe giza na utelezi, malaika wa Bwana akiwafuatia.” (Zaburi 35:4-6).

Kama nchi ni moja iitwayo Tanzania na watu wake ni Watanzania wasio na udini, ukabila wala rangi kwa nini tuwekeane upasi (hali ya kutopendana), vikwazo, kudharauliana na kuchukiana?

Nimalizie na methali hii: “Hakuna kubwa lisilo ukomo/lisilo mwisho.” Kila jambo huwa na mwisho wake. Hata maisha ya binadamu hufikia kikomo chake. Methali hii yaweza kutumiwa kumliwaza mtu (kwa maktadha huu wapinzani), anayepambana na hali ngumu au matatizo kuwa ajitahidi kuvumilia hatimaye yatafikia mwisho wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles