TIMU ya Manchester United jana ilifungwa mabao 3-1 dhidi ya Watford katika mchezo wa Ligi Kuu England, uliochezwa Uwanja wa Vicarage, jijini Watford.
Mchezo huo ulishuhudiwa kwa Kocha wa timu ya Manchester United, Jose Mourinho, kupoteza mchezo wa tatu mfululizo, ikiwa mara ya kwanza tangu mwaka 2006 alipokuwa akifundisha timu ya Chelsea.
Mashabiki zaidi ya 21,118 waliokuwapo katika mchezo huo, walishuhudia Watford kupata bao la kuongoza dakika ya 32 kupitia kwa Etienne Capoue.
Kipindi cha kwanza kilimalizika huku Manchester United wakiwa nyuma bao 1-0 licha ya kulishambulia lango la wapinzani wao mara kwa mara.
MShambuliaji wa United, Marcus Rashford, alifanikiwa kupata bao la kusawazisha dakika ya 61 kipindi cha pili, hata hivyo Watford waliongeza bao la pili kupitia kwa Juan Zuniga dakika 82 na kuchangia ushindi huo wa kihistoria, baada ya miaka 30 tangu walipowafunga wapinzani wao.
United waliongeza bao la tatu kwa mkwaju wa penalti dakika ya nne ya nyongeza baada ya dakika 90 kumalizika kupitia kwa Troy Deeney baada ya Marouane Fellaini kumfanyia madhambi Juan Zuniga.
Mchezo huo ulimalizika kwa United kufungwa jumla ya mabao 3-1, ukiwa ni mchezo wa pili wa ligi kuu kupoteza baada ya kufungwa dhidi ya Manchester City mabao 2-1.
United pia ilifungwa bao 1-0 katika mchezo wa ligi ya Europa dhidi ya Feyenoord na kufanya Maourinho kupoteza jumla ya michezo mitatu.