Na JOHANES RESPICHIUS,
KWA kasi iliyopo kwenye muziki wa Singeli, ni wazi kwamba unaelekea kuupoteza muziki wa Bongo Fleva kutokana na kasi ya kuenea kwake hapa nchini, jambo linalosisitizwa na mkali anayetesa katika muziki huo, Amani Khamisi ‘Man Fongo’.
Man Fongo ambaye amepachikwa jina la Mfalme wa Singeli, anayesumbua na kibao chake cha Hainaga Ushemeji amesema wasanii wa Bongo Fleva wana kazi kubwa kuhakikisha wanabaki kileleni kutokana na namna muziki wao ulivyopokelewa vizuri na mashabiki.
“Muziki tunaouimba ni wa mtaani ambapo ndiko chimbuko na watu wa uswahilini, kwa sasa huwaambii kitu kuhusu muziki wetu. Nawaambia ukweli kabisa wasanii wa Bongo Fleva, wakaze buti twende sawa au watafute kitu kingine cha kufanya.
“Ujue wao wanaimba vitu vya kubuni wakati sisi tunaimba maisha halisi hasa ya uswahilini kwa masikini wenzetu,” anasema Man Fongo.
Awali watu waliuita muziki wa kihuni kutokana na vijana kufanya matukio mbalimbali ulipokuwa unapigwa kwenye shughuli za mitaani nyakati za usiku maarufu vigodoro.
Kadiri siku zinavyokwenda, muziki huo umeanza kueleweka kiasi cha baadhi ya wasanii wa Bongo Fleva kushirikiana na wasanii wa Singeli kwenye nyimbo zao.
Mfano mzuri ni mwana-Hip Hop mwenye nguvu Bongo, Joseph Haule maarufu Profesa Jay ambaye ni Mbunge wa Mikumi kupitia Chadema alipofanya kolabo ya nguvu na msanii wa Singeli Sholomwamba.
Katika mazungumzo na jarida hili, Man Fongo ambaye anasimamiwa na Makes Entertainment amezungumza mengi kuhusiana na safari yake ya maisha na muziki kwa jumla.
SAFARI YAKE KIMUZIKI
Anasema alianza muziki tangu akiwa darasa la tano mwaka 2006 wakati akifanya shughuli zake za udj ambapo ilikuwa kama kurusha roho tu.
“Kipindi hicho Msaga Sumu ndiye alikuwa anajulikana zaidi na nilikuwa napitisha maneno kwenye baadhi ya nyimbo zake, mashabiki wakatokea kunikubali wakataka nijaribu kuimba.
“Licha ya kuanza muziki niliendelea na masomo yangu hadi nilipomaliza darasa la saba mwaka 2008, sikufanikiwa kuendelea na sekondari kutokana na kipato cha familia yangu.
“Muziki ukawa maisha yangu, namshukuru Mungu mwaka jana nilianza kupata mashabiki wengi na mwaka huu naweza kusema wameuelewa zaidi muziki wangu,” anasema Man Fongo.
FIESTA 2016
“Kwangu shoo kubwa ambazo nilikuwa nazifanya ni za kuitwa kwenye shughuli za watu kama ndoa, sherehe za kuzaliwa nk, lakini mwaka huu nashukuru Mungu nimeitwa Fiesta.
“Najua nitakutana na mashabiki wangu wengi katika mikoa nitakayopita. Zamani Singeli ilionekana kama muziki wa kihuni lakini nashukuru sasa watu wameuelewa muziki wetu.”
MALENGO YAKE
Anasema matarajio yake ni kufika mbali kimataifa lakini hawezi kufika kama Watanzania hawatauunga mkono muziki wa Singeli.
“Kila siku nawaza kuwaburudisha mashabiki wangu na kuupaisha muziki huu kimataifa zaidi, ni ndoto yangu kuwainua wadogo zangu ambao hawajasikika.
“Pia nimeamua kuacha tabia ya kutoa nyimbo tatu na sasa nitaanza kutoa albamu nzima, natarajia kutoa albamu yangu ya kwanza hivi karibuni,” anasema.
SINGELI KUONEKANA UHUNI
Anasema muziki huo umekuwa ukiitwa wa kihuni kutokana na mazingira ambayo umekuwa ukichezwa kuwa ya uswahilini sana ambapo vijana wa huko ndiyo wahuni.
“Naona ni kawaida kwa sababu Singeli ni muziki wa vijana na vijana ni damu changa, kwahiyo wao muda wote wanataka kucheza labda katika kufanya vile watu wengine wakauona ni wa kihuni.
“Muziki huu jamani siyo wa kihuni, labda watu wanaoupenda ndiyo wanaonekana wahuni… uswahilini hawaishi mabrazamen, huku wanaishi watu wa kawaida, ndiyo maana labda unachukuliwa kiivyo, lakini ni muziki mzuri, mtamu na unachezeka,” anasema.
CHANGAMOTO
Unapokuwa staa lazima kuwe na changamoto mbalimbali unazokutana nazo, kwa upande wake anasema amekuwa akipata usumbufu mkubwa kutoka kwa wasichana katika mitandao mbalimbali ya kijamii wanaomtaka kimapenzi.
“Siishiwi kupigiwa simu na baadhi ya wadada wakinisumbua, Instagram huko ndiyo shida zaidi… lakini najua ni mashabiki wangu, siwezi kuwachukia ila ukweli ni kwamba mimi nina mchumba wangu ambaye nipo naye miaka mitatu sasa na muda siyo mrefu tutafunga ndoa.
“Kupendwa kupo, lakini wajue tayari miye ni mali ya mtu. Napenda sapoti yao, waendelee kupenda muziki wa Man Fongo lakini siyo mambo ya mapenzi,” anasema Man Fongo.
Man Fongo pia alieleza kinachomchukiza zaidi katika muziki ambapo alisema: “Sipendi kupigana kwa sababu tukipigana ndiyo tunaonekana wahuni wakati lengo letu ni kuufanya kuwa wa kimataifa. Tukifanya vurugu hatuwezi kufikia popote.”