24.4 C
Dar es Salaam
Monday, November 28, 2022

Contact us: [email protected]

MAMLAKA ZISIKURUPUKE KUBOMOA NYUMBA ZA WANANCHI

 

KWA wiki kadhaa sasa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, hasa maeneo ya Kimara, wanaishi kwa hofu kubwa kutokana na kasi kubwa ya bomoabomoa inayoendelea katika eneo hilo.

Pamoja na kuwapo na zuio la mahakama juu ya kesi iliyofunguliwa, lakini ya ubomoaji imeendelea kutikisa, huku mamia ya wananchi wakikosa makazi na biashara zao nyingi kuharibiki.

Lakini wakati  hali ikiwa hivyo Kimara hadi Kiluvya, wananchi wa maeneo ya Tuangoma na Bonde  la Msimbazi wao wamepata ahuweni baada ya Rais Dk. John Magufuli kutangaza kusitisha ubomoaja uliokuwa umepangwa.

Katika eneo la Kimara wananchi wamevunjiwa nyumba nyingi na kutakiwa kuwa umbali wa mita  121.5 ili kupisha ujenzi wa  njia sita hadi Chalinze mkoani Pwani.

Jambo la kusikitisha katika eneo hili, kumefanyika bomoabomoa hiyo kwa  nguvu kubwa, huku wananchi kadhaa wakiwa na madai yao mahakamani, jambo ambalo tuliamini lingeheshimiwa hadi uamuzi utakapotolewa.

Hata hivyo Wakala wa Barabara (Tanroads), waliendelea na kazi zao kama kawaida. Msimamizi wa ubomoja huo Johnson Rutechura alisema pamoja na nyumba kadhaa katika eneo la Kimara hadi Kiluvya  ambazo  hazina kinga zitaendelea kubomolewa.

Tunasema kauli hii ni uungwana na inaonesha wazi namna ambavyo vyombo vya dola vinapaswa kufanya kazi kwa kuheshimiana kuliko kukomoana, jambo ambalo linazua maswali mengi mbele ya jamii.

Ni ukweli  usiopingika kwamba tangu hali hiyo, imeanza Tanroads imelaumiwa na watu wengi  hata baadhi ya vyombo vya habari kuandika kuwa imekiuka agizo la Mahakama.

Jambio jingine, ambalo limeshutua wengi ni uamuzi uliotangazwa wiki iliyopita la ubomoaji wa nyumba 17,000 katika eneo la Mto Msimbazi na Tuangoma ambako nyumba 300 zingevunjwa.

Si nia yetu kueleza mambo mengi juu ya tukio hili, lakini tunajiuliza hivi mamlaka hizi zinapofikia uamuzi huu huwa hazina mawasiliano?

Tunasema hivyo, kwa sababu hadi Rais Magufuli anatoa agizo la kusitisha ubomoaji hakuwa na taarifa wala mkuu wa wilaya husika, tunaona wazi kwamba kuna tatizo kubwa ndani ya mfumo wa Serikali katika utekelezaji wa majukumu yake.

Haiingii akilini jambo kubwa kiasi hiki lifanywe  na  mkuu wa wilaya  bila kupata baraka za mamlaka za juu wala waziri mwenye dhamana au Rais wa nchi.

Hata wananchi wa maeneo ya Tuangoma wamesikika wazi wakisema walipewa amri ya kuondoka kwenye nyumba zao na mkuu wa wilaya ambaye hakuwaonyesha sehemu nyingine ya kwenda kujihifadhi.

Kutokana na mambo kufanyika bila mawasiliano ya kutosha na kujali athari ambazo zinaweza kuwapata waathirika, tunazishauri mamlaka zilizopewa dhamana ya kusimamia mambo haya kuyafanya kwa umakini mkubwa.

Tunaamini kwa kufanya hivyo kutasaidia kuepusha malalamiko mengi na hasara kubwa ambayo inaweza kutokea.

Si kila jambo mpaka mamlaka zisubiri Rais atoe kauli, hili linatia shaka kwa watendaji hawa ambao  ni wateule wa Rais.

Wapo wananchi ambao wamenunua viwanja tena kwa watendaji wa Serikali na kupata vibali vyote, lakini hao nao utakuta wamejumuishwa kwenye orodha ya kubomolewa nyumba zao.

Sisi MTANZANIA, tunasema mamlaka zilizopewa dhamana hii zijitafakari vizuri kwenye utendaji wao, hasa linapokuja suala muhimu la kuvunja makazi ya watu.

Tunasisitiza hili, kwa sababu mwananchi wa kawaida ndiye anayeathirika zaidi tofauti na watawala ambao wanatumia kodi ya walalahoi kulipiwa gharama za pango.

Tunamalizia kwa kusema si kila jambo limsubiri Rais, mamlaka hizi ziache tabia ya kukurupuka kuvunja nyumba za wananchi kwa kutofuata taratibu.

Katika hali ya kawaida humvuruga mwananchi wa kawaida ambaye kesho anashindwa kujua wapi pa kuanzia kuendesha maisha yake ili kujipatia kipato.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,405FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles