23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MAMLAKA ZAJIPANGA KUNUSURU MAZAO YA MISITU NCHINI

NA ASHA BANI,

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani na Mamlaka ya Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), imeanza kampeni ya kutoa elimu juu ya njia halali za usafirishaji wa mazao ya misitu hususani mkaa katika barabara kuu zilizopo nchini kote.

 Akizungumza na waandishi wa habari juzi jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Tulizo Kilaga, alisema uvunaji holela na usafirishaji haramu wa mazao ya misitu hususani wa mkaa kwa kutumia pikipiki na baiskeli kutoka misitu ya hifadhi, mapori ya akiba na hata hifadhi za Taifa, unatajwa kuwa chanzo kikuu cha uharibifu wa misitu.

Kutokana na hali hiyo, TFS imeamua kutoa elimu kwa umma kabla ya kuchukua hatua za kusimamia sheria na kanuni za usafirishaji kwa lengo la kudhibiti uharibifu huo kabla nchi haijageuka jangwa siku za karibuni.

Alisema Tanzania inakadiriwa kuwa na hekta milioni 48 za misitu ambapo jumla ya hekta 372,000 za misitu huaribiwa kwa mwaka. Kiwango ambacho ni sawa na asilimia 1.1 ya eneo lote lenye misitu hapa nchini na ni sawa na kufyeka zaidi ya hekta 1,000 kwa siku.

Alisema Jiji la Dar es Salaam pekee hutumia zaidi ya magunia 500,000 ya mkaa huingizwa katika kipindi cha mwezi mmoja na kuongeza kuwa inakadiriwa pikipiki 20 zikisafirisha mkaa ni sawa na lori moja la tani 7 lililojaa mkaa na njia hii ya usafiri wa mazao ya misitu kwa baiskeli na pikipiki inakiuka mwongozo wa uvunaji endelevu wa mazao ya misitu, 2015 unaoeleza kuwa vyombo vya usafiri vinavyoruhusiwa kusafirisha mazao ya misitu ni vile vyenye magurudumu manne.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Elimu, Makao Makuu ya Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mossi Ndozero, alisema usafiri unaoendelea wa mazao ya misitu kwa baiskeli na pikipiki ni hatarishi na unaokiuka sheria.

 Kaimu Meneja wa Mawasiliano wa Mamlaka ya Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini, Salum Pazi, alisema kwa mujibu wa Kanuni ya Leseni za Usafirishaji ya Sumatra (Motor cycle and Tricycles), 2010 inatambua pikipiki kama chombo cha kusafirisha abiria na si vinginevyo.

“Kwa sasa tunatoa elimu kwa lengo na baada ya elimu hii watakaokaidi watachukuliwa hivyo ni vema kwa wale wanaofanya biashara za mazao ya misitu hususani mkaa wafuate sheria na kanuni za nchi,” alisema Kilaga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles