25.8 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Mamilioni laini za simu kuzimwa

WAANDISHI WETU

LEO ni siku ya mwisho iliyotangazwa kwa ajili ya usajili wa laini za simu kwa alama za vidole, huku Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ikisisitiza kutongezwa kwa muda wa usajili hata kwa dakika moja.

Pamoja na hiyo TCRA imesema kuwa kwa wale ambao wameshindwa kusajili laini zao, ifikapo saa 6 kamili usiku laini za simu milioni 22,478,727 zikitarajiwa kuzimwa na watumiaji wakijikuta wakishindwa kuwasiliana.

Muda huo wa nyongeza ulitolewa na Rais John Magufuli ambaye Desemba 27, 2019 aliongeza siku 20 kwa Watanzania watakaoshindwa kusajili laini zao za simu kwa alama za vidole ifikapo Desemba 31, mwaka jana.

Takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha hadi kufikia Januari 12 mwaka huu, laini zilizosajiliwa ni 26,170,137 sawa na asilimia 53.8 ya laini 48,648,864 zinazotumika nchini.

Kwa mujibu wa takwimu hizo za TCRA, kufikia Januari 12, siku nane kabla ya kuzimwa laini, laini za simu 22,478,727 sawa na asilimia 46.3 zilikuwa bado hazijasajiliwa kwa mfumo wa alama za vidole ikiwa ni siku nane kabla ya siku ya mwisho.

Aidha takwimu zilizotolewa Januari 2 mwaka huu na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dk. Anold Kihaule, zinaonyesha watu milioni 7.6 tayari wana namba, na kila siku mamlaka hiyo inaendelea kutoa sehemu mbalimbali nchini.

Mkurugenzi wa TCRA, James Kilaba, alisema zoezi hilo ni endelevu, hivyo kwa watakaositishiwa huduma, wanaweza kuendelea na utaratibu wa usajili kwa lengo la kuzirudisha au kupata laini mpya.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Msemaji wa TCRA, Semu Mwakyanjala alisema bado wanaendelea kukusanya takwimu za laini zilizosajiliwa kufikia leo watatoa taarifa rasmi.

Alisema hakuna mabadiliko na kwa kuwa TCRA inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na maelekezo, kwa maana hiyo ifikapo leo saa 6 kamili usiku wanatarajia kutekeleza agizo.

“Deadline (siku ya mwisho) ni kesho (leo) na ni kwamba kampuni zote za simu, Nida, Rita na Uhamiaji wanaendelea na zoezi katika hatua za mwisho. Kwa hiyo ikifika kesho (leo) saa sita usiku ni kwamba laini zote kwa wale wote ambao hawajasajili kufikia muda huo simu zao hazitakuwa hewani, kwa mujibu wa utaratibu.

“Hii n wazi kwa mujibu wa maelekezo, kwamba itakapoisha tarehe 20 Januari wale wote ambao hawajasajili wajue kuwa hawatakuwa hewani kuanzia dakika ya mwisho ya deadline hiyo. Labda yatokee maelekezo mengine,” alisema Semu.

MAKONDA ATOA NENO

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda amesema Serikali haitaongeza hata dakika moja katika usajili laini za simu kwa alama za vidole unaoendelea.

Akizungumza katika tamasha la kusajili laini za simu kwa alama za vidole lililofanyika Mbagala Zakhiem jijini Dar es Salaam jana, Makonda alisema kumekuwapo na tabia ya watu kupuuza maagizo ya Serikali ambayo inazidi kuzoeleka katika jamii.

Alisema Watanzania wamekuwa wakisubiri dakika za mwisho katika kila jukumu wanaloagizwa na Serikali jambo ambalo linajenga tabia mbaya.

“Rais Magufuli alipotangaza kuongeza siku ishirini watu wakasimama kujiandikisha wakisubiri siku za mwisho ndipo wajitokeze, kwa taarifa tu hatutaongeza hata nukta ya kusajili simu itakapofika muda,” alisema Makonda.

Alisema tabia hiyo imejengeka kwa kudharau hata maagizo yanayohusu maisha yao binafsi jambo ambalo halitafumbiwa macho.

“Kusajili laini yako mwenyewe mpaka tukuletee muziki, usalama wa simu yajo mpaka tukuitie wasanii, kuchagua kiongozi wajo wa serikali ya mtaa nayo mpaka ubembelezwe hii haiwezekani,” alisema Makonda.

Alisema alipokwenda katika uwanja huo kipindi cha kujiandikisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa alikuta watu waliojiandikisha wasiozidi 50.

“Sikuja kutafuta kura kwenu mimi sio mwana siasa, kipindi kile cha uchaguzi tulidhani kuwa watu hawaoni umuhimu wa kuchagua viongozi wa Serikali za Mitaa, suala la kuchagua kiongozi wako mwenyewe mtaani mpaka tukubembeleze?,” alihoji Makonda.

Alisema idadi ya watu wanaokwenda kutoa taarifa polisi kuhusu kuibiwa fedha zao zilizopo katika simu ni kubwa ndio sababu ya kuanzisha usajili huo.

 “Kuna watu wanaweza kutoa vitisho kwa Taifa kwa kutumia simu hizi lazima watambuliwe, hii ni kwa ajili ya usalama wako na fedha zako, familia yako na jamii kwa ujumla,” alisema Makonda.

Alisema mpaka sasa Jiji la Dar es Salaam lina laini milioni saba lakini zilizosajiliwa ni chache ndiyo maana wameamua kuongeza vituo vya kujiandikisha Vitambulisho vya Taifa.

Naye Meneja Usajili na Utambuzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Julien Mafuru alisema wameongeza vifaa na rasilimali watu ili kukidhi mahitaji yaliyopo kwa sasa.

Alisema mwamko wa kujiandikisha umeongezeka hasa katika kipindi hiki cha usajili hivyo wamejipanga kuendelea kuwahudumia kwa wakati.

Aliongeza kuwa changamoto iliyopo ni baadhi ya watu waliowahi kujiandikisha awali mpaka sasa hawajaenda kuchukua vitambulisho vyao katika ofisi za Serikali za Mitaa.

“Waliojiandikisha zamani vitambulisho vyao vipo serikali za mitaa hawaendi kuvichukua badala yake wanakuja tena kujiandikisha na kuongeza idadi ya watu katika foleni,” alisema Mafuru

Alisema pamoja na kuwapa taarifa mara kwa mara kupitia njia za ujumbe mfupi wa simu lakini wamepuuza taarifa hizo.

“Vitambulisho hivi tumeanza kuandikisha mwaka 2013 , wenyeviti wengi wa mitaa wameondoka bila kukabidhi hivyo baadhi ya vitambulisho havionekani,” alisema

WANANCHI WAOMBA NYONGEZA

Huko mkoani Njombe, wananchi wameomba Serikali kuwaongezea muda wa kusajili laini kwa sababu zoezi la upatikanaji wa namba limekua gumu na wkamba usajili wa laini hizo ulitangazwa kuwa ni bure lakini kwa sasa wanatozwa fedha.

Wakizunguma na MTANZANIA mmoja wa wananchi, Aghatha Kiyeyeu, alisema kuwa bado hwajakamilishiwa kumaliza usajili na kuna ambao walishajiandikisha lakini taarifa zao hazipo kabisa hivyo kuanza upya.

“Kwa hali ilivyo wangetuongezea muda kidogo na walisema zoezi ni bure lakini sasa hivi tunachajiwa na  hela kama elfu moja hadi elfu mbili, sasa hali hii imeendelea kutuumiza namba usumbuke na hela tena,’’ alisema

Kiyeyeu alisema changamoto nyingine ni upande wa laini za uwakala ambapo alisema asilimia kubwa za laini za uwakala zinatokana kwa kununuliwa hazikukamilishiwa usajili.

“Kwa mfano unaenda pale Tigopesa au Mpesa ukakuta watu walishazisajili alafu hawakwenda kuzichukua kwa hiyo unanunua unaenda kutumia yale majina sasa kufuatia hili zoezi ndo wanazizima na hela zako zinabaki kulekule, unaambiwa ujaze fomu umtafute huyo mtu unakuta alishakufaga mawasiliano hayapo miaka kumi iliyopita,’’ alisema Kiyeyeu.

Naye Sophia Ramadhani, alisema ni vema busara ikatumika kwa kuongeza muda kwa sababu watakosa mawasiliano ambayo ni muhimu.

“Mimi nakuja hapa wiki ya tatu sasa lakini sijapata nasioni dalili kwa hivyo muda hautoshi lich ya kuzunguuka kwa wiki zote hizo lakini sina nilichopata naumia kwa sababu mawasiliano ndio kila kitu kwenye biashara zetu,’’ alisema Ramadhani.

VIONGOZI WA DINI

Kwa upande Imam wa Msikiti  Mkuu wa Ijumaa Njombe, Sheikh Selenga Yassin, alisema jambo la usajili wa laini kwa alama za vidole ni changamoto kwa sababu limekua na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.

“Sio waumini tu hata sisi viongozi, mimi mwenyewe sasa hivi nina wiki tatu inamaana nimeshajiandikisha lakini mpaka leo hii namba sijaipata hivyo inapaswa kutumike busara ili watu wote wapate namba kwa kuongeza muda,’’ alisema Yassin.

Imam  huyo alisema kuwa swala la vitambulisho limekaa vibaya kutokana na kushindwa kwenda haraka kwa kisingizio cha mtandao.

“Lazima waendane na kasi ya watu kwa sababu kama umemwambia mtu ajaze fomu nimekuja pale watu wa uhamiaji wapo wakahoji ukaonekana umeshapita bado kupiga picha kinachofanya ukose namba kwa wakati kama ni kitambulisho sio mbaya kwa sababu ni matilio,’’ alisema Sheikh Yassin.

Kwa upande Ofisa wa Nida Mkoa wa Njombe , Odoyo Albetus, alisema kwa kawaida mtu akijisajili lazima fomu yake ipitiwe ili iweze kwenda kituo cha uzalishaji.

“Ikifika kule mtu ndo anapitishwa kwenye taarifa ambazo zinachunguza vidole na nyingine zinachunguza taarifa hii ili zipite ndo mtu apate namba,sio kwamba mtu akijiandikisha hapa Njombe mimi hapa sizalishi hata namba hakuna mkoa unaozalisha namba wotetaarifa namba na vitambulisho  zinazalishwa kituo cha uchakashaji wa taarifa,’ ’alisema

HABARI HII IMEANDALIWA NA ANDREW MSECHU, TUNU NASSOR (DAR) Na ELIZABETH KILINDI (NJOMBE)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles