Mamilioni kufungiwa laini za simu

0
1070

Na NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM

ZIKIWA zimesalia siku tatu kabla ya kuzimwa kwa laini za simu ambazo hazijasajiliwa kwa mfumo wa alama za vidole, laini milioni 22.4 ziko hatarini kufungiwa.

Awali Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilitangaza kuwa Desemba 31 mwaka jana ingekuwa siku ya mwisho ya kutumika laini zisizosajiliwa kwa mfumo huo, lakini Rais Dk. John Magufuli aliongeza muda hadi Januari 20, mwaka huu.

Rais Magufuli alisema anaongeza muda huo ili watu walioshindwa kusajili namba zao kwa sababu ya kuugua na wasiokuwa na namba ama vitambulisho vya taifa, waweze kumalizia mchakato huo.

 Alisema muda huo ukiisha hakuna kisingizio chochote kitakachokubalika na kuiagiza TCRA kuzima laini zisizosajiliwa.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kaimu Meneja Mawasiliano wa TCRA, Semu Mwakiyanjala, alisema hadi kufikia Januari 12 mwaka huu, laini zilizosajiliwa ni 26,170,137 sawa na asilimia 53.8 ya laini 48,648,864 zinazotumika nchini.

 “Laini za simu 22,478,727 sawa na asilimia 46.3 bado hazijasajiliwa kwa mfumo wa alama za vidole,” alisema Mwakiyanjala.

Takwimu zinaonyesha hadi Desemba 10 mwaka jana, laini zilizokuwa zinatumika zilikuwa 47,063,603 ambazo zinamilikiwa na watu milioni 21.1.

TCRA ilisema zoezi hilo ni endelevu, hivyo kwa watakaositishiwa huduma za laini za simu wanaweza kuendelea na utaratibu wa usajili kwa lengo la kuzirudisha au kupata laini mpya.

“Kwa watumiaji au waombaji wapya wa laini za simu, wataendelea kusajiliwa muda wote na usajili huo kwa kutumia kitambulisho cha taifa na kuhakikiwa kwa alama za vidole ni endelevu,” alisema Mwakiyanjala.

TCRA pia ilisema kwa wanadiplomasia au taasisi ambazo hazijakamilisha usajili wa laini za simu au zinazotumika kwenye vifaa vyao vya mawasiliano, wanatakiwa waendelee kufuata utaratibu uliowekwa.

Tangu Mei mwaka jana, Serikali ilizielekeza kampuni za simu kuanza usajili wa laini za simu kwa kutumia alama za vidole.

Hata hivyo, usajili huo umekumbwa na changamoto nyingi kutokana na wananchi wengi kutokuwa na namba ama vitambulisho vya taifa.

Katika maeneo mbalimbali nchini kumeshuhudiwa foleni kubwa za watu katika ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), wakihangaika kutafuta namba au vitambulisho huku wengine wakilalamikia kufuatilia bila mafanikio.

WALIOPATA VITAMBULISHO, NAMBA

Wakati akizungumza jijini Mbeya Aprili mwaka jana, Rais Magufuli alisema Watanzania milioni 14 ndio waliokuwa wamepata vitambulisho vya taifa.

Aidha takwimu zilizotolewa Januari 2 mwaka huu na Mkurugenzi Mkuu wa Nida, Dk. Anold Kihaule, zinaonyesha watu milioni 7.6 tayari wana namba na kila siku mamlaka hiyo inaendelea kuzitoa sehemu mbalimbali nchini.

Dk. Kihaule alitoa takwimu hizo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni, alipotembelea kituo cha kuchakata taarifa za waombaji nchi nzima kilichopo Kibaha mkoani Pwani.

Masauni aliagiza kuongezwa idadi ya watumishi katika kituo hicho na saa za kufanya kazi hadi kufikia 16 ili kwenda sambamba na muda ulioongezwa na Rais Magufuli.

Alisema katika vituo mbalimbali vya Nida wananchi wengi wamekuwa wakilalamikia kufuatilia vitambulisho bila mafanikio, licha ya kwamba wengine waliomba miaka mitatu iliyopita.

Hata hivyo, wakati wa mkutano wa pamoja uliohusisha Nida, TCRA, Polisi na wawakilishi wa kampuni za mawasiliano Kanda ya Ziwa, Nida walisema licha ya kuwapo msongamano mkubwa katika ofisi zao, lakini hali hiyo inasababishwa na watu wenyewe kujiandikisha zaidi ya mara mbili kwa kutumia taarifa tofauti, hususan watumishi.

Meneja wa Nida Kanda ya Ziwa, Raphael Manase, alisema watu wengi wanaofika vituoni wanagundulika taarifa zao si za kweli na wanaondolewa katika mfumo na wengine wamejisajili majina tofauti, wakiwamo watumishi wa umma na wastaafu ambao wana lengo la kukwepa madeni na vitu vingine.

Katika mkutano huo, Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Francis Mihayo, alisema kama si agizo la Rais Magufuli kuongeza siku 20 za usajili, laini za simu ambazo zilitakiwa kuwa hewani ni 24,021,757 kati ya 48,321,949 zinazotumika  nchini.

Alisema baada ya siku 20 zilizoongezwa, hawatakuwa na huruma tena kwa wale ambao wanatumia simu bila kukamilisha usajili wa laini kwa njia ya alama za vidole na kwamba zitaondolewa kwenye mfumo wa mawasiliano.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here