28.4 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Mamia Chadema, CCM wamzika Dk. Mahanga

Tunu Nassor – Dar es Salaam

MAMIA ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamejitokeza kuuaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Ilala, Dk. Makongoro Mahanga.

Dk. Mahanga alifariki dunia Machi 23 mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa akitibiwa.

Alikuwa mwanachama wa CCM na kushika nyadhifa mbalimbali kabla ya mwaka 2015 kukihama chama hicho na kwenda Chadema.

Hadi mauti yanamfika, alikuwa ni mwanachama wa Chadema na Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Ilala.

Akizungumza katika msiba huo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alisema walifanya kazi na Dk. Mahanga kwa muda mrefu kabla hajahamia Chadema.

“Nimekuja hapa kumwakilisha Katibu Mkuu (CCM) kutoa pole kwa niaba ya CCM kwa familia, Chadema na walioguswa wote,” alisema Polepole.

Alisema Dk. Mahanga alipoondoka CCM waliendelea kumtambua kama Mtanzania mwenzao ambaye waliwahi kufanya naye kazi kwa muda mrefu.

“Msiba huu umetuleta pamoja kama Mungu wetu alivyotaka, hivyo niwaombe tuendelee kumwomba ili asimame upande wetu na kutuepusha na ugonjwa wa corona,” alisema Polepole.

Naye Makamu Mwenyekiti Bara wa Chadema, Benson Kigaila alisema Dk. Mahanga alikuwa kiongozi, mpiganaji aliyejisimamia na kulinda imani yake bila kuwa na hofu.

Alisema si mtu wa kuyumbishwa katika misimamo yake, hata kama angetingishwa na misukosuko mizito.

“Nikutaarifu mama uliyeachwa kuwa umeachiwa familia nyingine nje na uliyonayo, ambayo ni Chadema, hivyo mkiwa na shida mjue mna wanafamilia wengine,” alisema Kigaila.

Naye Meya wa Manispaa ya Ilala, Boniface Jacob, alisema Dk. Mahanga alikuwa ni mtu mwenye kupenda kushikamana na wengine katika kipindi chote.

Kwa upande wake, Diwani wa Tabata Kimanga, Manase Mjema alisema Watanzania wanatakiwa kuishi kwa upendo wa kweli.

“Tunapokuwa viongozi tunajisahau kwa kuishi maisha ya kuwadharau wengine na kusahau  kuwa siku moja nasi tutakwenda kaburini, hivyo nashauri tuishi kwa upendo wa dhati kama alivyosema mchungaji,” alisema Mjema.

Naye Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, alisema watamkumbuka Dk. Mahanga kama mpiganaji ambaye hakutaka kukisaliti chama hicho hata katika mazingira magumu.

Msiba huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,206FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles