27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mamelodi kuvunja benki kwa Ngoma

DONALD NGOMA*Yaanza kumfuatilia, Yanga kunufaika dili likifanikiwa

ABDUCADO EMMANUEL NA JENNIFER ULLEMBO, DAR

NYOTA ya mshambuliaji wa timu ya Yanga, Donald Ngoma, inazidi kung’ara kila kukicha baada ya taarifa kutoka nchini Afrika Kusini kudai kuwa yupo kwenye rada za moja ya vigogo wa Ligi Kuu ya huko, Mamelodi Sundowns.

Mzimbabwe huyo pia inadaiwa yupo kwenye rada za timu nyingine za Asia na Ulaya, ikiwemo moja kutoka Denmark, anakokipiga nyota wa zamani wa Simba, Emmanuel Okwi.

Inadaiwa Mamelodi wanajipanga kuvunja benki yao ili kumng’oa nyota huyo Yanga, aweze kucheza Ligi ya Afrika Kusini ambayo ipo juu kiushindani.

Ngoma, aliyeteka nyoyo za mashabiki wengi wa Yanga kutokana na kiwango chake bora, alijiunga na Yanga Juni, mwaka huu akitokea FC Platinum ya Zimbabwe, mpaka sasa msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), amefunga jumla ya mabao nane ndani ya mechi tisa.

Habari zilizolifikia gazeti hili jana zimedai kuwa Ngoma anahitajika kwa vigogo hao, ili kuimarisha kikosi katika mbio zao za kutwaa taji la Ligi Kuu ya huko (PSL), walilolikosa msimu uliopita.

Sundowns, inayofundishwa na Kocha Mkuu wa zamani wa timu ya Taifa ya Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’, Pitso Mosimane, ndio mabingwa wa kihistoria wa PSL tokea ianze mwaka 1996, wakilitwaa mara sita na mara ya mwisho ilikuwa msimu wa 2013/14.

MTANZANIA lilifanya jitihada kuutafuta uongozi wa Yanga kuhusu suala hilo, ambapo Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya timu hiyo, Jerry Muro, alisema kuwa mpaka sasa hawajapokea barua au ofa kutoka timu hiyo.

Muro alisema watakuwa tayari kufanya biashara ya kumuuza Ngoma pale tu itakapokuja ofa nzuri kutoka Sundows na timu yoyote inayotaka kumsajili nyota huyo.

“Bado Sundowns haijaja kwetu, kama wanamtaka Ngoma waje na walete ofa yao tuongee, sisi hatuna tatizo lolote, tunachukulia mpira kama biashara, tunaangalia maslahi, wakifika dau watamchukua,” alisema.

Katika kujipanga kuziba pengo lake endapo ataondoka, Yanga inadaiwa tayari imeshafanya msako katika baadhi ya nchi Afrika Magharibi, ikiwemo Ghana, pia imeelezwa inammendea straika wa Stand United aliye kwenye fomu ya hali ya juu, Elias Maguli.

 

Hii si mara ya kwanza kwa Ngoma kutakiwa na timu za Afrika Kusini, mara ya kwanza ilikuwa ni Agosti, 2013, alipokwenda kufanya majaribio katika timu ya Amazulu kabla ya dili la kusajiliwa kushindikana.

Coutinho arejea

Upande wa ujio wa winga wao, Andrey Coutinho, aliyekuwa anataka kujiengua kijanja ndani ya timu hiyo akiwa nchini kwao Brazil, Muro alisema  mkwara walioutoa juzi katika vyombo vya habari, umechangia mchezaji huyo kurejea nchini haraka.

Muro alisema Coutinho anatarajiwa kuwasili nchini leo saa nane mchana na tayari taratibu zote za kuwasili kwake zimekamilika.

“Unajua Coutinho alivyoondoka hakuwa muwazi, ndiyo maana hata kurejea kwake kulikuwa kunaleta mashaka makubwa.

“Kama angeshindwa kurejea nchini ndani ya hizi siku mbili tulipanga kuvunja mkataba wake, nadhani marafiki zake walisikia na kumpa hizo habari,” alisema.

Uongozi wa Yanga ulipanga kumuuza Coutinho katika timu ya St. George ya Ethiopia, hata hivyo mpaka sasa bado haijaelezwa kama dili hilo lipo tena au limesitishwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles