27.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 20, 2023

Contact us: [email protected]

Mambo ya kufanya unapopitia wakati mgumu

CHRISTIAN BWAYA

INAWEZEKANA unasoma safu hii kwa sababu unajiona kama mtu unayeishi kwenye ukingo wa maisha. Mambo hayaendi kama ulivyotarajia. Umekata tamaa. Ukitazama wapi pa kupata msaada, unaona giza tororo.

Hakuna tumaini. Ujumbe wangu kwako ni mwepesi. Pamoja na ugumu wa hilo unalopitia sasa, bado lipo tumaini. Muhimu ni kujua kitu gani unaweza kufanya unapopita kwenye nyakati ngumu.

Ukweli ni kwamba hakuna bin­adamu anayependa shida. Lakini, hata hivyo, shida hutufundisha mambo ya msingi tunayoyahitaji ili tufanikiwe. Watu wengi waliofanikiwa, kwa mfano, hawakukwepa shida. Hawaku­tumia shida zao kama kisingizio cha kujihurumia na kuwalaumu wengine. Walizichukulia shida kama mwalimu wa kuwafundisha namna ya kwenda kule wanakotaka kwenda. Ufanye nini unapopita kwenye nyakati ngumu?

Usijihurumie kupita kiasi

Kuna mambo ni vigumu kuyakubali yanapotutokea. Kupokea taarifa za msiba, mathalani, si jambo rahisi. Mara nyingi tunazilazimisha fa­hamu zetu zinaamini kinyume chake. Kule kufikiri kuachwa na wapendwa wetu kunatufanya tuwe kwenye hali ya maombolezo kwa muda mrefu.

Tunaiaminisha akili kwamba tuko us­ingizini na kilichotokea ni ndoto tu ya kupita. Kukana hali ngumu, hata hivyo, huwa ni suluhisho la muda tu.

Kukubali hali halisi hata kama kufanya hivyo kunakuumiza hisia ni sehemu ya tiba ya nafsi yako. Kubali uliyempenda amefariki dunia. Kubali kazi uliyoitegemea haipo tena. Kubali mipango uliyokuwa nayo, haijaenda kama ulivyopanga. Kubali ndoa uliyofikiri ingekuwa ‘pepo ndogo’ du­niani, haijawezekana. Kubali pengine shauku ya kupata mtoto haitatimia. Ukikubali kilichotokea bila kujali unajisikiaje, hiyo ni hatua ya kwanza inayoweza kuanza kubadili maisha yako.

Changamoto moja wapo inay­oweza kukuzuia kukubali hali halisi, ni ile imani kwamba kilichotokea si haki. Ulichotendewa si haki. Unajiuliza, “Kwa nini wengine hawapatwi na kile kinachonitokea mimi?” Pambana na mawazo kama hayo ya kujihurumia. Usipopambana na mawazo kama haya unaweza kuishi na maumivu kwa muda mrefu sana. Wakati mwingine, unapokuwa kwenye magumu kama haya jambo muhimu unaloweza kufanya sio kujiuliza kwa nini kilicho­tokea kimetokea bali kukubali kwamba ni kweli kimetokea.

Tathmini kile ulichojifunza

Inawezekana umefukuzwa kazi. Inaumiza kwa sababu hukuwa umejiandaa na mbaya wako mmoja kazini amekuharibia. Baada ya kuku­bali kwamba ni kweli sasa huna kazi, kinachofuata ni kile unachojifunza.

Je, inawezekana hukujua namna ya kufanya kazi na mtu asiyekupenda? Je, inawezekana kupoteza kazi ikawa ndio mwanzo wa kufikiri namna ya kuanzisha na kuendesha shughuli zako mwenyewe?

Siku zote kuna upande mzuri kwenye kila kibaya kinachokutokea. Jitahidi kuufahamu upande huo.

Nawafahamu watu wengi waliolazimi­ka kufungua biashara zao na wakapata mafanikio kwa sababu tu walifukuzwa kazi. Wasingefanyiwa fitna kazini na kupoteza kazi, wangeendelea kuajiriwa kwa muda mrefu ujao. Kumbe nyakati ngumu kama hizi ukizitumia vizuri zinaweza kukufungua macho na kubadilisha kabisa uelekeo wa maisha yako.

Pengine ni madeni. Je, umeji­uliza kwanini kila mtu anakudai na unapata mshahara unaowatosha watu wengine? Je, kuna namna ambayo ungeweza kukwepa madeni hayo kama ungejifunza jambo fulani? Je, in­awezekana ni mtindo wako wa maisha umechangia kuingia kwenye matatizo yasiyo ya lazima? Pamoja na ubaya wa madeni, wakati mwingine, unaweza kuingia kwenye tatizo la kudaiwa, ili uone matokeo ya kufanya maamuzi ya kifedha yasiyo sahihi. Kudaiwa kunaweza kuwa fursa ya kubadilika.

Usijitenge na watu

Ni kweli, wakati mwingine, kujitenga kunaweza kukusaidia ku­waepuka watu wanaoweza kukufanya ukajisikia vibaya zaidi. Hata hivyo, uka­ribu na watu wanaoaminika ni hatua muhimu kuchukua unapopita katika kipindi kigumu. Watu wenye mtazamo chanya, kwa mfano, ndio watakaoku­saidia kukutia moyo, kukufariji na kukutazamisha mambo kwa namna itakayochangamsha tena moyo wako.

Kwa vyovyote vile unawafahamu watu katika maisha yako unaoweza kusema unawaamini. Hawa ni watu mnaoaminiana na kuheshimiana. Hawa si watu wepesi kukushambulia, kukuhukumu na kukuonyesha namna gani hali

uliyonayo hukupaswa kuwa nayo. Jitahidi kuambatana nao.

Tafuta msaada zaidi

Unahitaji msaada wa mawazo. Mahali pa kuanzia watu ulionao karibu kupitia vikundi vya kijamii ulivyonayo tayari mfano kanisani au msikitini. Hata kama huwafahamu zaidi watu hawa kiundani, bado kwa kule kuwa nao karibu itakusaidia kuyatazama maisha kwa sura ya matumaini. Kaa karibu na vikundi hivi ujijenge ki­imani. Nyakati ngumu ziwe kichocheo cha kuwa karibu na Muumba wako.

Lakini pia, ni vizuri wakati mwing­ine kukutana na watu waliowahi kupitia changamoto yako wanaoweza kukupa mawazo chanya ya namna ya kukabiliana nayo. Kama umepoteza kazi, mathalani, na kuna mtu unayem­fahamu aliwahi kupoteza kazi pengine unahitaji kuonana naye kupata uzoefu wa namna alivyoweza kupita kipindi hicho.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Mawasiliano 0754870815, Twitter: @bwaya/

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
210,784FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles