25.9 C
Dar es Salaam
Friday, May 27, 2022

Mambo ya kuepuka upate mafanikio  

maendeleoNa ATHUMANI MOHAMED

YAPO mambo mengi yanayochangia mtu kufikia ndoto zake na kupiga hatua kuelekea kwenye mafanikio. Leo nitaongelea mambo muhimu zaidi yanayohusisha uhusiano na watu wanaotuzunguka.

Inawezekana una tabia hizo na pengine hujui kuwa zinakuchelewesha na pengine zinakuweka kwenye hatari kabisa ya kutokufanikiwa maishani.

Bila shaka kwa kuzisoma hapa, zitakusaidia kubadili namna yako ya maisha ili milango yako ya kimafanikio iwe wazi na rahisi kufikika.

Kijasiriamali, mikopo ni moja ya njia zinazosaidia kwa kiasi kikubwa kutunisha mitaji na kuwasogeza watu mbele kuelekea kwenye mafanikio. Inapaswa kuheshimiwa.

Tatizo ni kwamba wapo ambao ni wagumu kulipa madeni. Hilo ni tatizo. Unaweza kuona siyo tatizo sana kumsumbua au kumdhulumu mtu mmoja, lakini kumbe ripoti za tukio lako hilo zimeshageuka bango kwa watu wengine.

Ni vizuri kuwa makini na hilo. Jambo jingine ni usengenyaji. Wapo watu ni hodari wa kuwasema wenzao. Wao hutumia muda mwingi zaidi kuwasengenya wengine bila sababu.

Kwa bahati mbaya ni kwamba, hawajui kuwa hiyo huchangia kuwaweka mbali na mafanikio. Hakuna siri duniani, unaweza kuongea jambo leo mbele ya watu watatu au wanne ukadhani limeishia hapo, kumbe linafika kwa watu wengine wengi zaidi.

Maana yake ni kwamba kwa kufikishwa kwa taarifa zako hizo mbaya, watu hawatapenda kukaa karibu nawe wala kukupa dili au taarifa za namna ya kuingiza fedha. Utakuwa umejiharibia mwenyewe.

Ndugu zangu hakuna uongo mdogo na mkubwa, uongo ni hatari sana kwa maisha yetu. Huwezi kuaminika ukiwa mtu usiye mkweli kwenye ahadi zako.

Kama una tabia ya kudanganya kwa namna yoyote ile, badilika. Shughulikia tatizo hilo, hata kuwahi tu kwenye miadi muhimu kama vikao vya ofisini, mikutano ya nyumba za ibada n.k.

Acha kumgandisha mtu mahali muda mrefu, huku ukiendelea kudanganya, “nipo karibu nakuja” wakati unajua wazi bado upo mbali. Kuwa mkweli, kama upo mbali sema na utoe muda ambao unaamini utakuwa umefika sehemu husika.

Lakini pia wapo wazee wa matanuzi, nyumbani ana familia kubwa lakini anaacha pesa ndogo au inayotosha lakini chakula kisichofurahiwa na familia.

Inawezekana kuacha fedha ndogo kama huna, lakini wapo ambao wanafanya hivyo halafu mitaani wanatumbua!

Watu wenye tabia hizi wanajinyima mafanikio bila kujua. Riziki zitaongezeka vipi ikiwa nyumbani watoto wanalalamika, wewe ukipiga michemsho na nyama choma baa?

Ni vizuri kujifunza zaidi kuhusu kanuni za mafanikio. Mfano kuwasaidia wenye mahitaji. Hii nayo ni kanuni nyingine ya uhakika ya kufanikiwa kwenye maisha.

Acha kuangalia una kiasi gani. Kusaidia si lazima uwe tajiri, hicho kidogo ulichonacho, jifunze kula na wenzako wanaohitaji.

Kuna wengine utashangaa hata kuwasaidia watu ambao ni chanzo cha mafanikio yao wanayoyaita madogo hawapo tayari.

Mzazi wako anakuomba fedha kidogo tu, utanung’unika siku nzima, lakini watu mliokutana barabarani upo tayari kuwasaidia. Siyo maisha hayo.

Kumbuka ulipotoka, wasaidie wazazi na ndugu zako, lakini pia ukiangalia ziada kila inapojitokeza kwa watu ambao hawajiwezi kwa namna moja ama nyingine.

Wenye kujua kanuni hii wamepiga hatua kubwa kimafanikio. Jaribu kanuni hii, utaona mafanikio yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,528FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles