24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

MAMBO USIYOYAJUA YANAYOWEZA KUONDOA KITAMBI KWA WANAWAKE

Na FADHILI PAULO,

WANAWAKE wengi siku hizi wanakabiliwa na tatizo la kuwa na tumbo kubwa kupita kiasi, hali inayosababishwa na mlundikano wa mafuta tumboni.

Mlundikano huo wa mafuta hutokea sehemu ya chini ya tumbo na tumbo lote kwa ujumla. Hali hii huwafanya wengine waonekane kama wajauzito kumbe ni mafuta tu yamezidi tumboni.

Kwa ujumla ni vigumu mno kupunguza tumbo la namna hii, hivyo ni muhimu zaidi kufahamu visababishi vya tatizo lenyewe, dawa za asili zinazoweza kuondoa tatizo hilo na aina ya maisha unayotakiwa kuishi ili kufanikiwa kirahisi kuepukana na adha hiyo.

UTAJUAJE UNA KITAMBI

Kitambi kinaweza kuonekana kirahisi kwa macho. Ila kujua ni kwa kiwango gani kitambi chako kipo inabidi kufanya vipimo vya kiuno(waist) na nyonga (hips).

Mzingo wa kiuno ukiwa >102 cm au 40 kwa wanaume na >88 cm au 35  kwa wanawake, na uwiano wa kiuno na hips(Waist-Hip Ratio) ikiwa >0.9 kwa wanaume na >0.85 kwa wanawake.

BMI ya 30 au zaidi inaashiria ‘Obese’ uzito kuzidi kiasi. Kuwa na mzingo uliozidi kawaida ni kiashiria hatari cha matatizo ya kimetaboliki, kuliko hata cha BMI.

Kipimo kingine cha kitambi ambacho kimeonyesha uwezo zaidi kuliko BMI katika kutabiri uwezekano mkubwa wa magonjwa ya moyo ni Index Of Central Obesity(Waist-To-Height Ratio-WHtR) ambapo uwiano ukiwa sawa na 0.5 au zaidi, hii ikimaanisha mzingo wa kiuno angalau ni nusu ya kimo cha mtu.

Kipimo kingine ni Body Volume Index, kinachopima kitambi kwa kupima umbo la mtu na mgawanyo wa uzito wake.

Nini kinasababisha tumbo kwa kina mama

Sababu kubwa ya kina mama kuwa na mafuta mengi tumboni ni kula vyakula feki (Junk food), kutumia vyakula vya wanga kupita kiasi, kutokunywa maji ya kutosha kila siku, kula chakula kizito muda mchache kabla ya kwenda kulala.

Sababu nyingine ni kukaa saa nyingi kwenye kiti, kutofanya mazoezi, kuwa na msongo wa mawazo, kula wali kila siku, ugali wa sembe, kula vyakula vinavyopikwa katikati ya mafuta mengi kama chipsi na maandazi.

Vyakula vinavyoondoa mafuta tumboni

ASALI NA LIMAU

Chukua asali kijiko kikubwa kimoja cha chakula na majimaji ya limau vijiko vikubwa viwili, changanya hivi viwili ndani ya glasi moja (robo lita) ya maji ya uvuguvugu na unywe yote mara tu ukiamka asubuhi.

Tumia kwa muda wa wiki tatu hadi mwezi mmoja.

MAJI YA UVUGUVUGU

Kunywa maji ya uvuguvugu kama lita moja hivi wakati tumbo likiwa tupu hasa asubuhi pindi unapoamka. Hii inasaidia kusafisha mwili na kuondoa mafuta yasiyohitajika.

NYANYA

Kula nyanya ambazo hazijapikwa husaidia kupunguza tumbo kwa kina mama, hivyo kula kachumbali ya kutosha kila siku ya nyanya peke yake na utaona mabadiliko.

TANGAWIZI

Chemsha chai ya tangawizi, ipua na usubiri ipowe kidogo, ongeza asali mbichi kidogo na pilipili manga kidogo ya unga. Pata kikombe kimoja cha chai hii kila siku asubuhi mapema ukiamka tu. Asali inasaidia kuyeyusha mafuta wakati pilipili itauongezea nguvu mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.

SIKI YA TUFAA

Siki ya tufaa (apple cider vinegar) inasaidia kupunguza njaa na kukufanya ujisikie umeshiba kwa kipindi kirefu. Kunywa kijiko kikubwa kimoja cha siki ya tufaa mara moja kwa siku, kila siku wakati unakula chakula cha usiku. Kazi nyingine ya siki ni kuweka sawa damu sukari mwilini hivyo ni nzuri pia kwa wenye kisukari.

MAJANI YA BIZARI

Majani ya bizari husaidia kuondoa sumu na takataka nyingine mwilini kitu ambacho moja kwa moja hufanya mlundikano mdogo wa mafuta tumboni. Kunywa chai ya majani ya bizari kila siku asubuhi, ukikosa majani unaweza kutumia hata unga wake.

ILIKI

Iliki hufanya kazi ya kuongeza nguvu katika mfumo wa mmeng’enyo wa chakula na ni dawa nzuri ya kuondoa sumu na takataka nyingine mwilini. Iliki pia hutumika katika kupunguza uzito. Tengeneza chai yenye iliki kila siku ndani yake, pia ni kiungo cha vyakula vingi hivyo hakikisha unaiweka katika kila chakula unachopika kwa matokeo mazuri zaidi.

MDALASINI 

Mdalasini hufanya kazi ya kuchoma mafuta mwilini. Chukua kijiko kidogo kimoja cha mdalasini ya unga na uweke ndani ya glasi moja ya maji ya moto na uache kwa dakika tano hivi. Ongeza kijiko kidogo kimoja cha asali mbichi ndani yake na ukoroge vizuri, kisha unywe mchanganyiko wote asubuhi unapoamka.

JUISI YA LIMAO 

Kunywa maji ya limao au juisi ya limau kila mara kunasaidia kuondoa mafuta tumboni kwa haraka. Ongeza majimaji ya limau vijiko vikubwa viwili ndani ya glasi moja ya maji na uongeze punje moja ya chumvi ya mawe, koroga vizuri na unywe asubuhi ukiamka kila siku.

KITUNGUU SWAUMU

Ili kupunguza mafuta tumboni katakata vipande vidogo vidogo (chop) punje tatu hadi nne za kitunguu swaumu na unywe na maji vikombe viwili asubuhi kisha shushia na glasi moja ya maji yenye limao kidogo kwa mbali.

Hii ndiyo njia nzuri kabisa ya asili ya kuondoa mafuta tumboni kwa haraka zaidi.

TIKITI MAJI

Tikiti maji lina asilimia 82 ya maji kitu kinachofanya tumbo kutokuwa na njaa ya kuhitaji chakula. Pia lina vitamini C ambayo ni muhimu kwa afya bora.

MAHARAGWE

Kula maharagwe kila mara kunasaidia kupunguza mafuta tumboni. Hii ni kwa sababu yana kiasi kingi cha nyuzinyuzi (faiba) kitu kinachosaidia tumbo kutojisikia njaa na hivyo kukuwezesha kula chakula kiasi kidogo. Kadri unavyokula chakula kichache ndivyo unavyokuwa mbali na uwezekano wa kuzalisha mafuta mengi tumboni.

TANGO

Tango lina asilimia 96 ya maji na asilimia zinazobaki ni nishati. Tumia kachumbari yenye tango ndani yake kila siku au kula tu tango moja kila siku ili kupunguza mafuta tumboni kwa haraka.

PARACHICHI

Parachichi ni tunda lingine zuri kwa ajili ya kuchoma mafuta yaliyozidi mwilini. Pia ni chanzo kizuri cha nyuzinyuzi (faiba). Hukufanya usihisi njaa kali. Lina mafuta ambayo ni mazuri (monounsaturated fatty acids) yanayosaidia kuchoma mafuta na hivyo kuondoa mafuta mabaya tumboni kirahisi zaidi.

TUFAA (apple)

Tufaa husaidia kupigana na magonjwa mengi mwilini, pia husaidia kuondoa mafuta tumboni. Humfanya mtu ajisikie kushiba kwa muda mrefu kwa sababu lina potashiamu na vitamini nyingi.

MAFUTA YA SAMAKI

Mafuta ya samaki hulenga kuyachoma moja kwa moja mafuta yanayozidi tumboni. Unaweza kuyafanya yawe ndiyo mafuta yako ya kupikia, pia unaweza kunywa kijiko kikubwa kimoja kila siku unapoenda kulala.

SIAGI YA KARANGA

Siagi ya karanga hupunguza njaa na kuongeza nguvu katika mfumo wa mmeng’enyo wa chakula. Ina kiinilishe kinachoitwa niacin, ambacho chenyewe huzuia mafuta kujilundika tumboni. Unaweza kuitumia kwenye mkate, kuungia mboga au kuweka katika wali.

MAYAI

Mayai yana vitamini nyingi ndani yake (ya kienyeji) na yana madini kama kalshiamu, zinki, chuma, omega -3 nk.

Viinilishe vyote hivyo katika mayai husaidia kuchoma mafuta yanayozidi tumboni. Hivyo kula mayai asubuhi kila siku ili kuondoa na kupunguza mafuta mwilini. Mayai pia ni moja ya vyakula vinavyomfanya mtu ajisikie kushiba kwa muda mrefu bila kuhitaji kula mara kwa mara.

CHAI YA KIJANI

Chai ya kijani maarufu ‘Green tea’ hufanya kazi ya kuondoa sumu mwilini jambo linalosaidia pia kuchoma mafuta yaliyozidi. Kunywa chai hii kila siku pia kunasaidia ngozi kukua pia kulifanya tumbo kukaa sawa bila kuwa na mafuta mengi.

MTINDI

Ingawa mtindi unaweza kusababisha kuongeza uzito zaidi, hata hivyo mtindi mtupu kabisa ule ambao haujaongezwa kitu chochote ndani yake unaweza kusaidia kupunguza mafuta tumboni.

Matumizi yake kwa siku yasizidi kikombe kimoja (robo lita). Pia ni moja ya vyakula vinavyoweza kukufanya ujisikie umeshiba na hivyo kukuondolea njaa ya kutaka kula.

JUISI YA KOTIMIRI 

Juisi ya kotimiri (Parsley juice) huondoa sumu na takataka nyingine zozote mwilini, pia huchoma mafuta na nishati. Kotimiri ni dawa nzuri kwa matatizo mbalimbali ya figo pia kwa kuchoma mafuta mwilini.

NDIZI

Kama lilivyo tufaa, ndizi pia zina kiasi kingi cha potashiamu na vitamini za aina mbalimbali ndani yake. Kula ndizi kila mara kunasaidia kuondoa hamu ya kutaka kula vyakula feki (fast food). Pia huuongezea nguvu mfumo wa mmeng’enyo wa chakula na hivyo kufanya mafuta ya tumboni kuyeyuka kirahisi zaidi.

MAJI YA KUNYWA

Kunywa maji ya kutosha kila siku kunasaidia pia kupunguza uzito. Kunywa lita mbili mpaka tatu kila siku ili kupata matokeo mazuri. Kunywa maji kidogo kidogo kutwa nzima. Hii haitafanya kazi ya kusafisha mwili tu bali pia kung’arisha ngozi. Pia hufanya nywele zionekane zenye afya.

Kitu cha kwanza ukiamka tu ni kunywa maji glasi mbili na uendelee kunywa glasi moja kila baada ya saa moja au mbili kutwa nzima. Maji ni uhai, bila kunywa maji kila siku ni sawa na kwenda dukani bila hela mfukoni.

Ikumbukwe kuwa asilimia 94 ya damu ni maji, asilimia 85 ya ubongo ni maji, asilimia 27 ya mifupa ni maji, asilimia 75 ya mwili ni maji.

Sehemu kubwa ya dunia hii imefunikwa na maji na sehemu yenye ardhi ni kipande kidogo mno. Haijalishi unaishi kwenye baridi au joto unatakiwa kunywa maji ya kutosha kila siku na si kusubiri hadi kusikia kiu.

MAZOEZI YA KUTEMBEA

Shida kubwa kwa wanawake wengi ni kutojishughulisha na mazoezi. Mazoezi yanaonekana kama ni jambo linalowahusu wanaume pekee.

Ili kuchoma mafuta mwilini kwa haraka zaidi tembea kwa miguu mwendo kasi kidogo kwa muda wa saa moja kila siku.

Zoezi hili linapaswa kufanywa kila siku ndani ya mwezi mmoja hadi miwili mfululizo.

Mwandishi wa makala haya ni tabibu wa tiba asili. Kwa mawasiliano zaidi tuma ujumbe mfupi wa maneno kupitia WhatsApp +255769142586

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles