Na William Shao,
“Mamilioni ya watu kotekote duniani wana magonjwa ya akili na jambo hilo huwaathiri sana wapendwa wao. Inasemekana kwamba mmoja kati ya watu wanne ataugua ugonjwa wa akili wakati fulani maishani. Ugonjwa wa kushuka moyo ndio kisababishi kikubwa cha magonjwa ya akili,” inasema ripoti ya utafiti ya Shirika la Afya Duniani (WHO).
Ripoti hiyo inayojulikana kama ‘Mental Health: A Call for Action by World Health Ministers’ inaongeza hivi: “Pia, ugonjwa wa ‘Schizophrenia’ na ule wa kubadilika-badilika kwa hisia ni miongoni mwa magonjwa yanayowadhoofisha watu wengi … Ingawa watu wengi leo wanaugua magonjwa ya akili, magonjwa hayo hupuuzwa na hayashughulikiwi sana au wagonjwa huaibikia hali yao.”
Kulingana na taarifa hiyo, watu wengi wanaougua magonjwa ya akili hawatafuti matibabu kwa sababu ya kuogopa jinsi jamii itakavyowaona.
Ripoti moja ya Shirika la Kitaifa la Magonjwa ya Akili nchini Marekani linalojulikana kama NAMI (National Alliance on Mental Illnes) , katika chapisho lake ‘Mental Illness, Facts and Numbers’, linasema kwamba ingawa magonjwa ya akili yana tiba, nchini humo takribani asilimia 60 ya watu wazima na karibia asilimia 50 ya vijana wenye umri wa kati ya miaka minane hadi 15 wanaougua magonjwa ya akili hawakutibiwa katika mwaka uliopita.
Wataalamu wanautaja ugonjwa wa akili kama tatizo kubwa la akili linaloathiri uwezo wa mtu wa kufikiri, kudhibiti hisia na tabia. Kwa kawaida hali hiyo huvuruga uwezo wa mtu wa kufurahia uhusiano mzuri na kukabiliana na changamoto za maisha.
Athari za ugonjwa wa akili hutofautiana ikitegemea muda na kadiri ambayo mtu ameugua na pia, hali za mgonjwa na aina ya ugonjwa anaougua.