MAMBO MATATU YATAKAYO KUFANYA UWASILIANE VIZURI NA WATU

0
1386

Na Christian Bwaya,

UMEWAHI kuzungumza kitu cha kawaida lakini ukashangaa mtu anasirika? Unafikiri ni kwa nini mtu akasirike kwa jambo dogo ambalo pengine lilisemwa kwa nia njema? Kuna sababu nyingi. Mojawapo ni namna unavyowasiliana naye. Vile unavyoweka ujumbe wako inaweza kufanya ama usieleweke au ueleweke tofauti na vile ulivyotarajia.

Mara nyingi tunafikiri tunajua kuwasiliana kwa sababu tu tunawafahamu wale tunaozungumza nao na tunajua wanataka kusema nini. Hata hivyo, wataalamu wa mawasiliano wanasema tunapowasiliana na watu tunaofikiri tunawafahamu vizuri, hatuwasiliani vizuri kama tunavyowasiliana na watu tusiowafahamu.

Unapozungumza na mtu unayemfahamu, ni rahisi kujiaminisha unajua anachotaka kukisema. Hufanyi jitihada za maana kumwelewa na kumsikiliza kwa sababu tayari akili yako inakuaminisha unajua atasema nini. Lakini tunapozungumza na mtu usiyemjua ni rahisi kuwa makini zaidi hasa kama unamheshimu.

Kuelewa kinachosemwa

Maisha yetu ni mtiririko wa mawasiliano. Mke na mume wanahitaji kujifunza namna ya kuwasiliana vyema. Wazazi wanahitahitaji kujua namna ya kuwasiliana vyema na watoto wao. Mawasiliano yakifanyika vizuri, huboresha uhusiano wa watu kwa sababu mwenye ujumbe anajisikia kueleweka na mpokeaji naye anajisikia kueleweka.

Hata hivyo, si kila mawasiliano yanaweza kujenga uhusiano. Uhusiano haujengwi kwa uwezo wa kueleza mtazamo wako kwa namna ambayo yule anayekusikiliza anaweza kukuelewa. Uhusiano hujengwa na uwezo wako wa kumsikiliza mwenzako na kumpa nafasi ya kufafanua anachokitaka.

Kwa kuzingatia umuhimu huo, makala haya yanasaili mbinu tatu zinazoweza kukusaidia kuwasiliana vizuri zaidi na mwenzako.

Heshimu hisia za mwenzako 

Hatua ya kwanza ya kuwasiliana na mwenzako ni kujali hisia zake. Binadamu ni kiumbe anayeheshimu hisia zake. Ukigusa hisia zake, iwe kwa kumkwaza au kumfurahisha, atachukulia kwa uzito. Hisia hazisahauliki.  Usipoweza kugusa hisia za mtu hutaweza kuwasiliana naye ipasavyo.

Ili uweze kugusa hisia za mtu lazima uondoe kiambaza kinachoweza kukutenganisha naye. Kiambaza kimoja wapo ni kujiona una hadhi kuliko yeye. Unapojiona ‘uko juu’ unaharibu. Jifunze kujiona mtu wa kawaida anayejali utu wa mtu zaidi kuliko hadhi na madaraka. Unapoweza kufanya hivyo, unagusa hisia za mwenzako na kwa vyovyote atakusikiliza. 

Sikiliza zaidi

Mara nyingi tunapozungumza tunatamani kusikilizwa. Tunaamini sisi ndio watu wenye taarifa na uelewa sahihi kuliko wanaotusikiliza. Ukishaamini una haki ya kusikilizwa, hata katika mazingira unayoonesha kusikiliza, kimsingi unakuwa ukingoja zamu yako ya kuongea. Unafikiria utasema nini baada ya hapo.

Tatizo ni kuwa kadri unavyotamani kusikilizwa ndivyo unavyomfanya anayepaswa kukusikiliza ajione hathaminiki. Kutokuthaminika humfanya ajenge umbali wa kihisia na hivyo kukosa ari ya kukusikiliza.

Jenga mazoea ya kusikiliza watu kwa makini. Hapa hatuzungumzii kusikiliza kinachosemwa pekee, bali namna gani kinasemwa, kitu gani hakisemwi wazi na kipi kimejificha.

Fuatilia mazungumzo

Kumfanya mtu ajisikie anaheshimiwa na kusikilizwa ni sehemu muhimu ya mawasiliano. Unahitaji kujifunza kuonyesha unafuatilia mazungumzo. Kwanza, epuka kumkatisha mtu anapoongea au kumalizia sentensi yake. Mtu anapoona unaingilia maneno yake anahisi tayari unaamini unajua anachotaka kusema.

Pia, itikia anachokisema mwenzako kumtia moyo kuwa unajali na kufuatilia mazungumzo yake. Itikia kwa kutikisa kichwa, kumwangalia machoni, maneno kama ‘mmh-mh!’

Muhimu ni kuwa unapozungumza na mtu mpe mrejesho. Rudia anachokisema kwa maneno yako na uliza maswali hapa na pale. Kwa kufanya hivyo, utamfanya aone unajali.

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Moshi. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here