Mambo manne ya kujifunza ufufuaji ATCL

0
807

 

Na DEUS KIBAMBA

NIKIWA safarini kwenda Hungary kwa shughuli za kawaida, nimebahatika kupitia na kujifunza mengi mjini Istanbul, Uturuki. Swali kubwa nililokuwa nalo kabla ya kukutana na baadhi ya watumishi wa shirika la ndege la nchi hiyo maarufu kama TK ilikuwa ni vipi wameweza kumudu kuwa na ndege zaidi ya 300 za ukubwa tofauti tofauti na kuendelea na biashara hiyo ya usafirishaji wa anga pasipo misukosuko wakati huu ambapo mashirika ya ndege katika nchi za Afrika Mashariki ndiyo yanajaribu ‘kufungwa mashine za kupumulia’ ili yasife na kuzikwa moja kwa moja.

Nchi ya Uganda, ambayo iliwahi kuwa na ndege zake za Air Uganda ilijikuta ikiyumba katika uendeshaji kiasi kwamba ndege nyingi ziko juu ya mawe zikiliwa na kutu pale Entebbe. Kenya, ambayo kwa miaka mingi ilisifiwa sana kwa kuwa na Shirika imara la ndege likijiendesha kama Kenya Airways au  KQ nalo limejikuta likiwa matatizoni.

Kwanza, Serikali imeshindwa kuliendesha shirika hilo na kuachia hisa takribani zote kumilikiwa na watu binafsi huku utendaji wake ukiyumba kiasi cha kujaribu kufumua safu nzima ya uongozi wa juu na kuleta watendaji wapya.

Pili, mbinu za kuchukua biashara iliyokuwa imetawaliwa na mashirika ya ndege ya Tanzania zilifanikiwa kwa muda tu baada ya kuingia makubaliano ya ushirikiano na Shirika la Precision la mfanyabiashara toka Tanzania lakini mambo yakaharibika kiasi cha kuivunja ndoa hiyo miaka kadhaa iliyopita.

Kwa upande mwingine, Tanzania, ambayo iliwahi kutembea kifua mbele ikirusha ndege zenye nembo ya mnyama Twiga kutoka Dar es Salaam hadi Johannesburg, Afrika Kusini na maeneo mengi barani Afrika na Ulaya imejikuta ikipoteza ndege zake zote kwa sababu ya uendeshaji mbovu wa shirika kiasi cha kupata hasara kwa miaka mingi mfululizo.

Mpaka kabla ya Uchaguzi Mkuu 2015, Tanzania ilikuwa ni kama haina ndege baada ya ndege zake mbili za mwisho ambazo zilipatikana kwa msaada kufikia hatua ya kuwekwa juu ya mawe, moja ikiwa ni kutokana na kupata ajali kidogo mkoani Kigoma.

Kwa sababu hiyo, imenipasa kujiuliza juu ya mambo gani yanapaswa kuzingatiwa ili kuendesha biashara ya usafiri wa ndege au anga? Wanaofanya biashara hii ya usafirishaji angani kwa mafanikio makubwa kama KLM, SA, Rwand Air na hao Turkish Airlines wanafanyaje mpaka wanaendesha biashara hii kwa mafanikio? Sisi tunashindwa, wao wanaweza wana nini? Je, tunahitaji mambo gani ya kujiangaliza ili juhudi mpya za Tanzania, chini ya uongozi wa Rais Magufuli zisije zikaishia ukingoni kama vile ilivyotokea siku za nyuma? Majibu ya mambo hayo, pamoja na maelezo mengine kadhaa ya kitaalamu niliyoyapata yamenisukuma kuandika tafakuri hii leo.

Kwanza, nianze kwa kupongeza Juhudi za Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Pombe Magufuli kwa kuamua kutuondolea aibu ya kuwa nchi isiyokuwa na ndege hata moja ya kupeperusha bendera ya Tanzania katika matukio yote makubwa ambayo yanastahili kushuhudia ujumbe wa Tanzania ukitua kwa ndege yao yenye rangi zake zote na nembo ya Bibi na Bwana?

Hivi tunakumbuka kuwa Tanzania iliwahi kuwa na ndege ambazo zilikuwa zikiruka Dar mpaka Jo’burg na hata London? Mnaikumbuka ATC  ilivyopata umaarufu wakati huo? Je, tunaweza kujiuliza ilipotea vipi? Iliishia wapi? Mara ya mwisho kusikia habari za ATCL ilikuwa ni taarifa kuwa ndege yake ilishindwa kukunjua mbawa, ikaangukia tumbo katika Uwanja wa Ndege wa Kigoma.

Kabla ya hapo, kulikuwa na tukio la ndege yake moja kunasa topeni katika moja ya viwanja nchini. Na kulikuwa na habari kuwa ndege hizi za mwisho mwisho hazikuwa zimenunuliwa kwa pesa yetu wenyewe bali zilikuwa zimepatikana kwa msaada wa Wachina fulani. Je, ni kweli? Na Je, Wachina walivuna nini kwetu mpaka watoe msaada wa ndege mbili, moja kubwa na moja ndogo?

Je, hata baada ya kupata hitilafu, ndege hizo ziliwezaje kutotengenezwa na kurejea ulingoni? Hazikuwa na bima? Bima ilishindwa nini kulipa gharama ya matengenezo? Maswali haya yote ni muhimu sana wakati tukitafakari wapi tulipojikwaa katika uendeshaji wa Shirika la Ndege Tanzania siku za nyuma kama sehemu ya kujipanga kwa siku zijazo!

Kwa sasa, tayari ndege nyingine kadhaa zimeagizwa na nyingine kutua Dar kama mkakati wa kulifufua Shirika letu la Ndege la Tanzania. Tulishuhudia uzinduzi wa mbwembwe wa bombardier likiruka kutoka Dar es Salaam – Dodoma na viwanja vingine. Binafsi najisikia fahari na faraja kubwa kusikia kuwa zipo ndege nyingine, tena kubwa zaidi zitakuja mwaka huu, mwakani na mwaka 2019.

Swali kubwa lililopo ni Je, tutalazimika kufanya nini ili ndege hizo na shirika lake viwe endelevu? Natoa mapendekezo manne ya mambo muhimu ambayo lazima yazingatiwe ili Watanzania na hasa Rais John Pombe Magufuli tusije tukapata ugonjwa wa moyo kwa kuambiwa kuwa ndege zetu, ambazo zimekwishatumia na bado zitatumia mabilioni ya shilingi za Kitanzania zikilipiwa kwa pesa adimu za kigeni zimezorota na kufa tena.

Ikitokea hivyo, itatukatisha tamaa sana na mimi najiona nina wajibu wa kuweka angalizo kabla hatujafika huko kubaya.

Jambo la kwanza, ni lazima tujue kuwa usafiri wa anga ni biashara. Lazima tuendeshe ndege zetu kibiashara. Upo wakati tuliendesha ATCL kama shamba la bibi lisilohitaji hata kupiga hesabu ya endapo tunazalisha faida au la! Tulikuwa na wafanyakazi makumi elfu wanaohudumia shirika lenye ndege mbili au tatu, huku mishahara yao ikilipwa na Hazina Kuu pasipo kujiuliza kama shirika linaleta faida au la.

Jambo hili ni jambo la ajabu na likijirudia, tutaua tena shirika kama ilivyotokea siku za nyuma. Sambamba na hilo, biashara ya ndege ni njia (route) zake. Tuliwahi kuwa na njia kadhaa barani Afrika na nje ya Afrika. Tulikuwa na safari za Afrika Kusini, Kenya, Malawi, Zambia na wakati fulani Ulaya.

Nadhani nitawashangaza wengi kusema kuwa njia hizi ziliuzwa kabla ndege hazijafa. Tulirubuniwa na kutapeliwa na mashirika kadhaa ya ndege ya nchi nyingine ili tuingie ubia na ushirikiano kiasi kwamba wakati fulani kwa mfano, kulikuwa na ndege ya ATC inaruka kutoka OR Tambo kuja Dar es Salaam muda ambao ndege mshirika wake SA nayo inaruka OR Tambo kuja Dar. Na hili lilitokea bila kujali kuwa ndege hizo mbili zimejaa au la! Sasa niliwahi kujiuliza, ushirika huu vipi?

Ushirika gani wa ndege zote mbili kuruka zikiwa hazijajaa? Mafuta wanalipaje? Baadaye nilikuja kuambiwa kuwa ilikuwa ni njama ya kupoka njia (route) ya ATC kutoka Dar – Jo’burg na Jo’burg – Dar kiujanja. Baada ya miezi au miaka kadhaa ya ujanja huo, ATC ilishindwa kununua hata mafuta ikaacha kuruka Dar – Jo-burg na kumwachia SA akiendelea kuruka, tena kwa kujaza ndege mara tatu kwa siku.

Mbinu kama hiyo ilifanywa kwa njia nyinginezo kama Dar – Nairobi. Huko nako, tulirubuniwa na kujikuta tukipokwa njia hiyo na Shirika la Ndege la Kenya (KQ). Baadaye, hata safari za ndani ya nchi ziliporwa na ushindani kutoka kwa Precission Air tukaishiwa pumzi na kuweka ndege zetu juu ya mawe. Ujanja unaofanana lakini wa tofauti kidogo ulikuja kutumiwa na washindani wa PW yaani FastJet kwa kuleta ndege za vunja bei ya mpaka Sh.32,000 kwa safari kiasi cha kuliyumbisha sana Shirika la Precission wakati fulani. Kwa ujumla, nataka niseme kuwa biashara ni njia au routes kama ijulikanavyo kwa lugha ya usafiri wa anga.

Kutokana na hilo, nimejifunza sana kutokana na utafiti wangu kwa mashirika mengine yanayofanya vyema duniani. Moja ya mashirika hayo ni Shirika la Ndege la Uturuki ambalo linaendeshwa kwa nguvu ya Serikali ya nchi hiyo. Wao, ni wabobevu wa masuala ya biashara ya ndege na wanazo ndege lukuki. Imenishangaza kusikia kuwa hawanunui ndege mpaka kwanza wafanye utafiti wa kimahitaji. Kwa mfano, itashangaza wengi kuwa si kweli kuwa madege makubwa ndiyo yanayohitajika sana. Kwa uzoefu wa TK, ndege za ukubwa wa kati nzito zinalipa na kuhitajika zaidi. Katika hazina yao ya ndege, TK wanazo ndege za ukubwa wa kati nyingi kuliko kubwa sana na ndogo sana. Kwa mfano, shirika lina ndege za ukubwa wa juu aina ya Boeing B 777 – 300 ER zipatazo 33 tu zenye uwezo wa kubeba hadi abiria 400 kwa wakati mmoja.

Chini yake, wanazo nyingine za ukubwa wa chini kidogo aina ya Ambrier A 340 – 311/313 na A330 – 200/300 zipatazo 56. Hizi zina uwezo wa kubeba abiria kati ya 270 na 354 kwa wakati mmoja.

Chini zaidi ya hizo, kuna kundi lenye ndege nyingi zaidi aina ya Ambrier A 321 – 231/232 zipatazo 68 na A 320 – 232/214 zipatazo 92 zikiwa na uwezo wa kati wa kubeba abiria 150 – 194 kwa wakati mmoja.

Chini zaidi ya hapo kuna Ambrier A 319 – 100 zipatazo 7 na Boeing B 737 -900 ER zipatazo 15 ambazo huweza kubeba kati ya abiria 132 na 159 kwa wakati mmoja. Fungu lenye ndege nyingi kuliko zote ni lile la ndege za Boeing za ukubwa wa wastani B 737 – 800 ambazo huweza kubeba abiria 151 hadi 165. Hizi, Shirika la ndege la Uturuki wanazo 108 huku Boeing ndogo zaidi ya Boeing B737 – 700 wakiwa nayo moja tu kwa sasa. Kwa ujumla, Shirika la Ndege la Uturuki wana ndege zipatazo 312 za abiria na nyingine 14 za mizigo na kufanya jumla ya ndege (fleet) kuwa 326.

Hivyo basi, wakati tukijiandaa kuingia katika biashara hii ya ndege ni vyema tukafahamu jambo moja kubwa kuwa wakati tupo tunaotambaa, wako wanaokimbia siku nyingi. Kwa ushauri wangu, Tanzania tusinunue ndege kwa lengo la kuingia katika ushindani wa soko la Nje. Nionavyo, tulenge kushika soko la ndani ya nchi ili ATC iwe kiunganishi kati ya mashirika makubwa kama TK ambayo tayari yamekamata soko la dunia la usafiri wa anga na nchi yetu ambayo ina kila aina ya vivutio vya wageni kuja kuviona. Tukijichanganya, tukaanza kutaka kutandaa na kurusha ndege zetu hadi Istanbul na Ljubljana tutaishiwa pumzi na kushindwa kuendelea na biashara hii.

Angalia hata TK ambao wana misuli kama hiyo wamelazimika kujiunga katika muungano wa ndege wa Star Alliance ili kuweza kuhimili ushindani kutoka kwa magwiji wengine wa biashara ya usafiri wa anga duniani wa Sky alliance wakiongozwa na Shirika la ndege la Uholanzi (KLM).

Mwisho, biashara ya ndege ni nyeti na inataka nidhamu kubwa katika maeneo mawili. Kwanza ufundi na matengenezo na pia uendeshaji. Tukipokea ndege hizi, tukazifananisha na magari yetu binafsi ambayo huweza kutembea na kuvusha kilomita za matengenezo (service) kwa zaidi ya mara mbili au tatu, tutaziua zenyewe au kuua watu wetu kwa kuzidondosha.

Nashauri tuzingatie ustaarabu mkubwa ambao huhitajika katika uendeshaji na usimamizi wa ndege ili tuweze kudumu na biashara hiyo adhimu nchini. Vinginevyo, nashauri tubadilike katika utamaduni wetu wa uwajibikaji. Biashara ya ndege, tofauti na basi, inavutia inapokwenda na wakati na muda. Lengo hasa mtu huweza kuamua kutumia ndege na si basi au punda ni ili afike haraka na salama.

Tukiendelea na tabia yetu ya kufurahia matangazo ya ‘tunasikitika kutangaza kuwa ndege TC imechelewa kwa masaa manne au matano’ tutakimbiwa na kujikuta tukirusha madege yetu kwa kukaanga ambao utakuwa mwanzo wa kufunga biashara.

Kila la kheri Rais Magufuli katika kufufua ATCL na ninawaomba Watanzania tumuunge mkono. Mimi nimeanza kwa ushauri huu!

Deus M Kibamba ni Mtafiti, Mhadhiri na Mshauri wa Masuala ya Demokrasia ya Katiba, Siasa na uhusiano wa Kimataifa. Amekuwa mwangalizi wa Kimataifa katika Michakato ya uchaguzi, Maridhiano na mazungumzo ya kitaifa katika nchi kadhaa za kiafrika. Kwa sasa, Kibamba anafuatilia mchakato wa Mazungumzo ya Kitaifa Katika Nchi ya Sudan ulioanza mwaka 2013.Anapatikana kwa simu: +255 788 758581; email: [email protected]

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here