30.4 C
Dar es Salaam
Saturday, December 2, 2023

Contact us: [email protected]

Mambo magumu Ligi Kuu Bara

NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM

MAMBO magumu! Hiyo ndiyo hali halisi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu, baada ya kutokea mchuano mkali miongoni mwa timu shiriki.

Mchuano huo mpaka sasa umeonekana kuzihusu zaidi timu zinazoshika nafasi ya kwanza hadi ya 10 kwenye msimamo wa ligi, huku timu za Simba, Yanga na Azam zikipewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa.

Ligi imefikia raundi ya saba huku baadhi ya timu zikicheza mechi sita lakini pia tofauti ya pointi katika msimamo wa ligi hiyo imeonekana kuwa ni ndogo.

Yanga ambao ndio vinara wa ligi wakiwa na pointi 16 sawa na Azam FC wamepishana pointi moja tu na timu za Simba na Mtibwa Sugar zenye pointi 15 katika nafasi ya tatu na nne, zote zikiwa zimecheza mechi sita.

Stand United ya Shinyanga iliyocheza mechi saba iko nafasi ya tano wakiwa na pointi 12, imezidiwa pointi nne na vinara Yanga, Azam na pointi tatu dhidi ya Simba na Mtibwa.

Mwadui chini ya kocha mkongwe nchini, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ na Mgambo JKT, nazo zimefanya kweli kwa kuzikimbiza kwa kasi timu tazo za juu kwani zimefanikiwa kujizolea pointi 11 katika mechi saba walizocheza.

Timu mbili zilizopanda daraja za Toto Africans na Majimaji nazo zimekomaa kama Mwadui zikitaka kushika nafasi za juu zote zikiwa zimejizolea pointi 10 sawa na Tanzania Prisons, wakidaiwa pointi sita kuwafikia vinara.

 

Makocha tumbo joto

Mtihani mkubwa upo kwa timu sita za chini zilizopo kwenye janga la kushuka daraja, kuanzia Ndanda inayoshika nafasi ya 11 hadi JKT Ruvu inayoburuza mkia huku makocha wa timu hizo wakiwa na presha kubwa ya kutimuliwa kwa matokeo mabaya.

Ndanda inayofundishwa na Amini Mawazo, imejikusanyia pointi sita kwenye mechi sita walizocheza, ikiwa na wastani wa kuchukua pointi moja katika kila mchezo.

Kocha bora wa ligi msimu uliopita, Mbwana Makata, anayeifundisha Kagera Sugar naye amejiweka mtegoni baada ya kuambulia pointi tano kwenye mechi saba, wakiwa wamepoteza nne, sare mbili na kushinda mmoja.

Mbeya City iliyoondokewa na kocha wao kipenzi, Juma Mwambusi, ipo kwenye hali mbaya baada ya kujikusanyia pointi nne ikiwa nafasi ya 13 na kumpa kazi kubwa ya kufanya kocha Abdul Mingange ili kuirudisha kwenye fomu timu hiyo kabla mambo hayajaharibika.

Mahasimu wa Jiji la Tanga, Coastal Union, inayofundishwa na Mganda, Jackson Mayanja na African Sports chini ya Joseph Lazaro, nao wapo pabaya hadi sasa wakiwa na pointi tatu katika nafasi ya 14 na 15.

Coastal Union ndio inasikitisha zaidi ikiwa mpaka sasa haijafunga bao lolote wala kushinda mechi, sawa na JKT Ruvu iliyopo mkiani ambayo imefungwa mechi sita na sare moja.

 

Vita ya ufungaji yanoga

Baada ya takribani mwezi mmoja wa Mganda, Hamis Kiiza (Simba) kutesa kwenye kilele cha ufungaji bora, hatimaye mambo yamebadilika baada ya kupinduliwa na Elias Maguli (Stand United) aliyefikisha mabao sita.

Kiiza aliyetupia mabao matano sawa na Donald Ngoma (Yanga), wanafuatiwa kwa karibu na Amissi Tambwe (Yanga), Kipre Tchetche (Azam), Fully Maganga (Mgambo JKT) waliofunga manne kila mmoja huku Atupele Green (Ndanda) akipachika matatu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles