MAMBO 20 YA KUZINGATIA UKIWA KIJANA – 6

0
1762

Na ATHUMANI MOHAMED

BILA shaka wasomaji wangu mtakuwa wazima wa afya njema na mnaendelea na majukumu yenu salama kabisa. Kwa upande wangu, afya yangu ni njema kabisa.

Leo tunahitimisha mada yetu iliyoanza majuma matano yaliyopita. Ni mada ndefu, lakini yenye maana na faida kubwa kwa vijana ambao wanatamani kuwa wenye mafanikio maishani mwao.

Kama nilivyotangulia kusema kwenye matoleo yaliyopita, maisha ni kuchagua. Wewe ndiye utakayeamua maisha yako yaweje.

Waswahili wana msemo wao unasema, ‘ukiona vyaelea, ujue vimeundwa.’ Hapo kuna somo kubwa sana, kwamba usione watu wana mafanikio ukadhani wameyapata kwa urahisi, walisotea.

Lazima nyakati fulani ujinyime vitu fulani ili siku moja ufurahie maisha. Unaweza ukapenda raha leo, lakini baadaye maisha yako yakawa mabovu.

Nimeandika mada hii kwa vijana kwa sababu wana muda. Wakitengeneza misingi mizuri leo, bila shaka kesho yao itakuwa nzuri. Hawatakuwa na maisha yenye dhiki.

Sasa tumalizie vipengele vya mwisho vilivyosalia.

 

  1. THUBUTU MAMBO MAGUMU

Wengi waliofanikiwa walijaribu kufanya mambo magumu ambayo wengine wanayaogopa. Sababu moja ya kufanikiwa kwa kufanya mambo magumu ni kwa sababu ya uoga wa wengi.

Ndani ya muda mfupi unaweza kufanikiwa na kuwashangaza watu, mpaka wengine waje kufahamu unachokifanya, tayari utakuwa umefanikiwa.

Umiza ubongo wako juu ya kitu gani ufanye ambacho wenzako hawajafanya ili ufanikiwe. Ubongo wako una mengi ya utajiri ni vile tu hujajipa muda wa kufikiri sawasawa.

 

  1. JIFUNZE UJASIRIAMALI

Jenga mazoea ya kujifunza ujasiriamali. Tafuta mafunzo ya utengenezaji bidhaa, ufugaji na biashara nyingine za kijasiriamali.

Usipende sana kuwaza kuhusu kuajiriwa maana ukweli siyo mstari mzuri wa mtu anayetamani kuwa na mafanikio baadaye. Waza kuanzisha chako kisha kuwaajiri wengine.

 

  1. RUDISHA FADHILA

Kamwe usiwe mtu wa kusahau ulipotoka. Mafanikio ya mtu yana uhusiano mkubwa sana na uhusiano mzuri na waliomsaidia.

Kwanza wazazi wako. Usiwasahau kwa namna yoyote. Unapaswa uwatunze na kuwasaidia hata kama wana uwezo mzuri kimaisha. Kuwapa zawadi ni shukrani tosha na inaweza kuwa baraka kwako.

Wengine wamesaidiwa na ndugu zao wa karibu na hata marafiki. Ukipanda juu usisahau nyuma. Shukrani yao ni dua na mtaji wa mafanikio yako. Usiwasahau kabisa waliokusaidia.

 

  1. KUWA KARIBU NA WALIOFANIKIWA

Hapo ndipo kwenye umuhimu zaidi.  Waliofanikiwa ni msaada kwako. Siyo kwamba hutakiwi kuwa na urafiki na watu wa kawaida, hapana lakini wale waliofanikiwa ni muhimu zaidi.

Kuwa na urafiki na waliofanikiwa watakusaidia kufahamu zaidi mbinu za namna ya kupata mafanikio. Kuwa nao kwa faida, acha stori zisizo na mashiko. Ulizia zaidi yale mambo unayotamani kuyajua kuliko kuzungumzia mambo ambayo hayana maana.

Siyo rahisi kuwa karibu na watu wote waliofanikiwa, lakini wapo walioandika vitabu mbalimbali, wasome kupitia vitabu vyao watakusaidia namna ya kusogea mbele zaidi.

Hii ni nguzo muhimu na unapaswa kusafiri nayo hadi unapokuwa kwenye kilele cha mafanikio.

 

 

  1. UWEKEZAJI WA ASILI

Huko nyuma tuliona kuhusu uwekezaji, hakuna tofauti kubwa sana na kipengele hiki, lakini hapa unatakiwa kuwekeza kwenye vitu vya asili ambavyo vina faida kubwa na ya kudumu.

Uwekezaji huu uhusisha mifugo na ardhi kwa maana ya kilimo. Waliogundua njia hii wamefanikiwa sana. Bado kuna maeneo mengi wanauza ardhi kwa bei nafuu. Nunua kwa wingi kadiri unavyoweza.

Unaweza kufanya uwekezaji wa mifugo na kilimo na ukapata fedha nyingi sana. Mfano yapo maeneo huko Dodoma (vijijini) ambapo unaweza kupata ardhi kwa bei ndogo kisha ukaweka mifugo yako.

Kazi yako itakuwa kuweka watu ambao watakusaidia kulima na kutunza mifugo yako, kisha utawalipa. Uwekezaji huu haukuhitaji kuwepo eneo hilo. Unaweza kuamua kuishi mjini na uwekezaji wako ukaendelea bila shaka yoyote.

Matajiri wengi wanaijua siri hii, wamewekeza kwenye kilimo na mifugo ambayo gharama zake za uendeshaji siyo za kutisha sana hasa kama utafuga mifugo ya kawaida (ya kiswahili) ambayo mahitaji yake siyo ya kutisha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here