24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

MAMBO 20 YA KUZINGATIA UKIWA KIJANA- 4

Na ATHUMANI MOHAMED

KAMA utachagua kuishi mradi unasukuma siku huwezi kuona mabadiliko katika maisha yako. Ukweli ni kwamba wale wanaoishi kwa malengo huwa na nafasi kubwa zaidi ya kufanikiwa kuliko wale wanaosubiri bahati.

Ni kweli wakati fulani unaweza kupata mafanikio kwa  bahati yako, ila siyo jambo la kutegemea sana wala kusubiria.

Ni jambo lenye afya zaidi ikiwa mtu utaamua kusaka mafanikio kwa juhudi na ubunifu. Hii ndiyo sababu tunajifunza mambo ya msingi ambayo kijana anapaswa kuyafanya.

Nasema kijana kwa sababu ndiye mwenye mwanga wa mafanikio, atakuwa anatengeneza msingi mzuri wa kufanikiwa mbele.

Kwenye somo hili, kijana akiweza kuyafuata mambo haya na mengine akasafiri nayo hadi anapokuwa mtu mzima kwake kufanikiwa ni jambo la kawaida.

Kwa bahati mbaya, watu wengi ni wavivu wa kuchukua vitu katika vitendo. Wengi wa Watanzania na Waafrika kwa ujumla si watu wanaopenda kujisomea, lakini hata hao wachache wanaojisomea siyo wajuzi wa kubadilisha waliyojifunza na kuhamishia kwenye vitendo.

Ni imani yangu kuwa wewe kijana unayesoma hapa, utakuwa unajifunza na kuweka mambo haya akilini mwako na baadaye katika vitendo ili kukusogeza kwenye mafanikio.

Sasa tuendelee na mada yetu ambapo leo tunaendelea na kuona jambo nambari tisa kati ya 20 yaliyopo kwenye mada hii.

 

9. ISHI KWA UAMINIFU

Ukizungumza na watu waliofanikiwa, kwenye stori zao hutakosa kusikia wakisema uaminifu ulikuwa kati ya vitu vilivyowasaidia.

Msingi wa kuwa na uhusiano mwema na jamii yako ni kuwa mwaminifu. Baadhi ya vijana hushindwa kabisa jambo hili.

Uaminifu ni mtaji mkubwa wa mafanikio. Huwezi kupanda siku zote, kuna wakati utahitaji usaidizi wa watu wengine hivyo ni muhimu sana kuwa mwaminifu.

Jiambie mwenyewe ndani ya moyo wako kwamba uaminifu ni jambo la msingi unapaswa kuwa nalo kama sheria. Ukiweza kuwekeza kwenye uaminifu, maisha yako yatakuwa rahisi.

Ukikopeshwa rejesha kwa wakati, hakikisha watu unaoshirikiana nao wanajenga imani kwako kwa kiasi kikubwa. Sifa yako ya uaminifu itangazwe na watu wengine hata kama ukiwa haupo.

Kabla ya fedha, hebu jifunze kuwa mwaminifu.

 

10. IJUE KIU YAKO YA NDANI

Inawezekana unafanya kazi kwenye shirika fulani au ndiyo kwanza umemaliza masomo. Pengine unafanya biashara au ujasiriamali lakini huoni mafanikio, unataka kupiga hatua.

Watu wengi wanafeli kwa kushindwa kufanya kazi zilizopo mioyoni mwao. Hebu jiulize, ni kweli kazi unayofanya ipo moyoni mwako? Ukijichunguza vizuri ndani mwako utagundua kilicho moyoni mwako na utatafuta namna ya kufanya.

Kumbuka kufanya kilicho ndani yako, unajiweka kwenye nafasi nzuri na ya hakika ya kufanikiwa. Huwezi kufanikiwa kwenye biashara wakati ndani yako kuna sanaa ya uchekeshaji!

 

11. POTEZA MUDA KUSAKA MAARIFA

Ukishajua kiu yako au kazi iliyopo ndani yako, fanya uamuzi mgumu wa kuijua. Inawezekana hujaisomea kwa sababu hukujua na sasa umefahamu, ni wakati wako wa kusaka maarifa.

Usiogope kupoteza muda. Tafuta kazi kwenye kampuni au shirika linalojishughulisha na kazi ya ndoto zako. Hata kwa kujitolea kubali kufanya ukiwa na malengo yako. Baada ya muda hutakuwa kama ulivyokuwa mwanzo.

Inawezekana ni ujuzi ambao unatamani kuujua ili ufanyie kazi mwenyewe, jitolee ujifunze. Ukishaelewa hutakuwa mgeni tena na hapo mrija wa mafanikio utakuwa umefunguka.

Kumbuka ni rahisi kujitolea ili kujifunza kazi ya ndoto yako ukiwa kijana, ukishakuwa mtu mzima, kasi ya kutafuta mahitaji huwa kubwa zaidi kuliko kutafuta mafanikio.

Mtu mzima mwenye majukumu yake, huangalia zaidi familia yake, tofauti na kijana mwenye muda wa kupanga na kusaka mafanikio zaidi kwa sababu bado atakuwa hana familia na hata kama akiwa nayo, haitakuwa kubwa kiasi cha kumfanya ashindwe kufikiria namna ya kufanikiwa kwenye maisha yake.

Somo letu litaendelea Jumamosi ijayo, usikose msomaji wangu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles