Brighiter Masaki – Kisarawe.
Bishara Foundation wakiongozwa na Mwenyekiti, Nunu Rashidi, wamemsaidia kijana mwenye ulemavu wa viungo mkazi wa Kisarawe Mkoa wa Pwani, kwa kumpatia kiti cha kutembelea (Weelchair) na kiasi cha fedha.
Akizungumza na Mtanzania mapema leo, Oktoba 14, wakati wa kukabidhi kiti hicho kwa kijana Jafari, aliyepata ulemavu baada ya kusumbuliwa na ukungu kwenye ubongo.
“Bishara Foundation tumeguswa na Jafari tukaona tuchukue nafasi hii kumnunulia kiti kitakachomsaidia kuweza kufanya baadhi ya shughuli zake, lakini Watanzania mnatakiwa kuguswa na kumsaidia chochote ulichonacho ili aweze kupata dawa,” anasema Nunu.
Mama yake Jafari anayeitwa Zawadi Hassan anasema kuwa mwanae huyo alizaliwa akiwa mzima kabisa, lakini alikuja kupata tatizo hilo lililomsababishia ulemavu.
Anawaomba Watanzania kumsaidia kwa kuwa mume wake amemtelekeza na yeye hana kazi ya kufanya ukizingatia Jafari anahitaji dawa ambazo zinagharimu kiasi cha Tsh. 40,000 kila mwezi.