23.8 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

Mama Mwinyi asema Dini ya Uislamu imehimiza kuwatunza wazee…

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi amesema kuwa katika Dini ya Uislamu Mwenyezi Mungu amehimiza kuwatunza wazee kwa kuwafanyia wema na ihsani katika maisha yao yote.

Mama Mariam Mwinyi aliyasema hayo leo kwa nyakati tofauti katika hafla ya kuwakabidhi futari na sabuni wazee wanaoishi Sebleni na Welezo katika Mkoa wa Mjini Magharibi.

Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi akiwakabidhi Futari Wazee wa Nyumba za Wazee Sebleni jijini Zanzibar alipofika kuwasalimia katika makaazi yao Sebleni na kuwakabidhi Futari kwa ajili ya matumizi ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani

Katika hotuba yake fupi kwa wazee hao, Mama Mariam Mwinyi alieleza kuwa ibada ya kuwatunza wazee ina fadhila kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu hivyo, aliitaka jamii kuendeleza utamaduni huo.

Mama Mariam Mwinyi aleleza kuwa anafahamu kwamba wazee wana mahitaji mengi lakini aliwahakikishia kuwa Serikali inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi inazitambua changamoto zao na itaendelea kujitahidi kuzifanyia kazi hatua kwa hatua.

Aliwataka wazee waendelee kuishi kwa amani na upendo wakijua kwamba Serikali yao iko pamoja nao kwa shida na raha wakati wote.

Aidha, Mama Mariam Mwinyi aliwasisitiza wazee kuendelea kushirikiana na Serikali yao kwa kutoa michango na mawazo mbali mbali ambayo yana busara na hekima kubwa. “Na ndiyo maana wahenga walisema kwamba ‘Isiyokongwe haivushi”, alisisitiza Mama Mariam Mwinyi.

Pamoja na hayo, Mama Mariam Mwinyi alifikisha salamu za upendo kutoka kwa Rais Dk. Hussein Mwinyi kwa kuwatakia kheri na baraka za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani wazee hao wa Sebleni na Welezo.Mama Mariam Mwinyi alitumia fursa hiyo kuikumbusha jamii kutambua kwamba wapo waumini wengi wenye kutekeleza ibada ya Saumu wakiwa na uwezo mdogo wa kupata futari, daku na mahitaji mengine muhimu yanayoambatana na mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Aliongeza kuwa kuna idadi kubwa ya watoto yatima, wazee wasiojiweza, wajane wenye kipato kidogo, watoto waliotelekezwa, walemavu na makundi mengine yenye mahitaji maalum ambayo yanahitaji msaada.

Hivyo, aliitaka jamii kuzingatia miongozo ya dini katika kuyasaidia makundi hayo kwa wenye uwezo, sambamba na kudumisha utamaduni wa kuishi kwa misingi ya upendo na ujirani mwema huku akisisitiza kuendelezwa utamaduni uliorithiwa kwa wazee wa kupelekeana futari na kufuturu kwa pamoja.

Nao wazee hao kwa nyakati tofauti walitoa shukurani zao kwa Mama Mariam Mwinyi kwa msaada wake huo futari na kumuombea dua kwa Mwenyezi Mungu azidi kumpa neema ili aendelee kuwakumbuka wazee wake hao.

Wazee hao pia, walieleza jinsi wanavyofarajika na juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi katika kuhakikisha wanaishi katika mazingira ya amani, usalama na upendo sambamba na kupata huduma zote muhimu za kijamii katika makaazi yao.

Nae Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,Wazee, Jinsia na Watoto, Abeida Rashid Abdallah alitoa pongezi kwa Mama Mariam Mwinyi kwa hatua yake hiyo ya kwenda kuwasalimia na kuwapa futari wazee wa Sebleni na Welezo katika kipindi cha mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrisa Kitwana Mustafa kwa upande wake alimpongeza Mama Mariam Mwinyi na kueleza jinsi wazee wa Sebleni na Welezo walivyofurahi kwa kupata ugeni huo adhimu pamoja na futari huku akiwahakikishia wazee hao kwamba Mama Mariam Mwinyi ataendelea kuwatembelea

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles