Na TWALAD SALUM
MAMA lishe wa Kata ya Misungwi wilayani Misungwi wamemlalamikia Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya hiyo, Ackim Jackson, kuhusu baadhi ya maofisa afya wa kata hiyo wanaowaomba kati ya Sh 3,000 na Sh 5,000 kwa ajili ya kuwapima afya .
Walikuwa wakizungumza juzi wakati ziara ya siku mbili ya Katibu wa CCM wilaya hiyo kwenye Kata na Kijiji cha Misungwi kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Misungwi
Baadhi ya mama lishe hao ni wanaofanya shughuli zao katika soko kuu la Misungwi na soko la zamani .
Kwa mujibu wa kina mama hao, hutoa fedha za kupimwa afya zao bila kupatiwa huduma hiyo
Walisema wamekuwa wakitoa fedha kati ya Sh 3,000 na Sh 5,000 mara kwa mara kwa maofisa afya kwa ajili ya kupimwa afya zao lakini hawawapati huduma hiyo jambo ambalo wameliona kuwa ni rushwa kwa maofisa hao.
Mama lishe wa Soko la Zamani, Ester Samson, alisema maofisa afya wamekuwa wakipita sehemu wanazofanyia biashara zao wakiwa na daftari na kuwachangisha kati ya Sh 3,000 na Sh 5,000 na kuwaandika majina yao kwa ajili ya kupimwa afya.
“Tunaomba chama tawala kitusaidie kuna maofisa afya wawili hupita mara kwa mara wakituchangisha fedha na usipotoa wanakufungia biashara yako… sisi tuna watoto wanategemea kama mimi ni mjane mtusaidie tumegeuzwa Saccos,” alisema Ester Samson.
Naye Mariam John alsema kuna Ofisa Afya mmoja ambaye huwavizia asubuhi na akiwakuta hawajavaa sare anaomba sare ambazo hazijavaliwa na kuzichukua ili awalipishe faini.
“Wengine hutuvizia mapema, akikukuta unasukuma chapati umevaa kofia tu anachukua aproni unayotarajia kuivaa na kuondoka nayo ili aje baadaye akutoze faini ya Sh 50,000 … atakupa namba ya akaunti ya benki ya NMB ukalipie usipofanya hivyo anakufungia biashara,” alisema John.
Hata hivyo, Ofisa Afya ya Jamii wa Kata ya Misungwi, Paulina Kubimbi, alisema alikumbana siku moja na mama lishe ambaye alimpa Sh 1,000 kwa ajili ya soda na aliomba amrudishie.
“Tulikuwa na Mary tukapita kwa mama lishe huko bondeni akatupa Sh 1,000 ya soda, kama hiyo ni rushwa ntamrudishia asitupake matope sisi ni maofisa,” alisema Kubimbi.
Abubakari Abdallah, aliyetuhumiwa kuchukua sare zao na kuondoka nazo kwa lengo la kuwatoza faini, alisema amekuwa akitumia busara kwa wale wanaoshindwa kufuataSsheria za Afya ya Jamii kwa kuvaaa sare.
Alisema amekuwa akiwanyang’anya sare ambazo huwa wamezining’iniza bila kuzivaa ili wapate uchungu wazivae na wale wanaodai huwatoza faini ya Sh 50,000. Alikiomba chama kimuunge mkono.
“Nakiomba chama kiniunge mkono badala ya kunikatisha tamaa kwa sababu mimi naogoza wilaya hii kuingiza pato kwa kuwatoza faini nimeingiza zaidi ya Sh milioni mbili kwa mwaka huu, lengo ni kuwataka kufuata sheria ya afya,” alisema Abdallah.
Katibu wa CCM wa Wilaya, Jackson aliwataka watendaji kufanya kazi zao kwa kutowaonea wananchi na mama lishe akawashauri watimize masharti ya usafi kuepuka magonjwa ya mlipuko.