23.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Mama, baba lishe wafundwa kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Mama na baba lishe wametakiwa kuzingatia kanuni za afya na usalama wa chakula ili kuepuka hatari ya maambukizi ya maradhi yanayoenezwa kupitia chakula.

Akizungumza Agosti 29, 2023 wakati wa mafunzo kuhusu lishe, usafi na usalama wa chakula Ofisa Lishe kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Neema Manyama, amesema magonjwa mengi yasiyo ya kuambukiza yanaanzia kwenye ulaji.

Ofisa Afya na Mratibu wa Ubora na Usalama wa Chakula, Ally Makwana, akizungumza wakati wa mafunzo kwa mama na baba lishe kuhusu usalama wa chakula.

Mafunzo hayo yamehusisha mama na baba lishe kutoka mitaa mbalimbali ya Kata za Vingunguti na Mnyamani.

“Magonjwa mengi yasiyo ya kuambukiza yanaanzia kwenye ulaji, chanzo chake ni ulaji usiofaa ndiyo maana tunapeana elimu ili kuhakikisha tunatoa huduma nzuri kwa wale tunaowahudumia,” amesema Manyama.

Amesema mama na baba lishe wana dhamana kubwa kwa sababu watu wengi wanakula nje ya familia hivyo kama chakula hakitakuwa salama kinaweza kuzalisha vimelea vya maradhi kama vile homa ya matumbo, kipindupindu, kuharisha na minyoo tumbo.

Naye Ofisa Afya na Mratibu wa Ubora na Usalama wa Chakula, Ally Makwana, amesema mafunzo hayo yamelenga kujenga uelewa kwa mama na baba lishe ili waweze kubadilisha mapishi na kuondoa hatari ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Amewataka kutotumia ndoo zilizokuwa na rangi kwani zina madini ya risasi ambayo yanachangia kueneza ugonjwa wa saratani.

Amewataka mama na baba lishe kuzingatia makundi salama ya vyakula wanapoandaa vyakula, kuepuka matumizi mengi ya mafuta, sukari na chumvi na usalama wa maji wanayotumia ikibidi wayatibu.
Kwa mujibu wa ofisa huyo, makundi matano ya chakula ni vyakula vya nafaka, mizizi na ndizi, jamii ya kunde na asili ya wanyama, mbogamboga, matunda, mafuta na sukari.

Amesema pia fedha zinaweza kuwa chanzo cha vijidudu vya maradhi na kusisitiza mtayarishaji wa chakula asihusike katika kupokea fedha.

“Fedha pia zimebeba vimelea vya maradhi, kama uko mwenyewe kwenye biashara yako ukishapokea fedha kwa mteja nawa kwanza mikono ndipo umuhudumie au hakikisha mnakuwa wawili, mmoja anapokea fedha na mwingine anahudumia wateja,” amesema Makwana.

Mmoja wa mama lishe kutoka Mtaa wa Faru, Ptronia Simfukwe, amesema anatarajia baada ya kupata mafunzo hayo atabadilisha biashara yake kuanzia uandaaji wa chakula hadi kinapomfikia mlaji.
Katika mafunzo hayo pia mama na baba lishe wamehimizwa kupima afya zao kabla ya kuanza huduma ya chakula na kila baada ya miezi sita.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles