ALLY BADI
-LINDI
MTOTO Razaki Ally (9), mkazi wa Kitongoji cha Milamba Kata ya Kivinje wilayani Kilwa, amelazwa katika Hospitali ya Kinyonga, akiuguza majeraha a baada ya kuchomwa moto mikononi na mama yake mzazi, Zabibu Issa kwa tuhuma za kuiba Sh 7,000.
Razaki ameunguzwa vibaya mikono yake yote miwili na kwa sasa hana uwezo wa kushika kitu chochote kutokana na majeraha hayo ya moto.
Akizungumza na MTANZANIA jana baada ya kutembelea hospitalini hapo, mama wa mtoto huyo, Zabibu Binamu alisema alichukua uamuzi huo baada ya kuchoshwa na tabia ya wizi na mashtaka ya kila wakati kutoka kwa majirani zake.
Alisema siku ya tukio, mtoto wake alimuibia Sh 7,000 alizokuwa amezitunza chumbani kwake hali iliyomfanya achukie na kupatwa na hasira iliyosababisha kuchukua uamuzi wa kumchoma moto mikono yake.
“Jamani naomba nieleze ukweli kisa kwa ujumla mtoto wangu huyo amekuwa na tabia ya wizi na udokozi mara nyingi tu, hivyo hasira ilinipanda nikaamua kumchoma moto kukomesha tabia hiyo,” alisema Zabibu.
Hata hivyo, mwanamke huyo mwenye watoto watatu, alisema anajutia kitendo alichokifanya, akidai kinampotezea muda wa kuendelea na shughuli zake za kujitafutia riziki ikizingatiwa hana mume.
Mmoja wa mashuhuda, Mwanaharusi Kumala, ailiambia MTANZANIA kuwa siku hiyo ya tukio, Razaki akiwa nyumbani kwao alimsikia mtoto huyo akipiga kelele za kuomba msaada baada ya kuchomwa moto na mama yake.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kinyonga, Dk. Salehe Abubakari, alikiri kumpokea mtoto huyo akiwa na majeraha kutokana na kuchomwa moto na mama yake mzazi kwa madai ya kumuibia fedha.
Alisema kutokana na kiwango kikubwa alichoungua mtoto huyo, uchunguzi unaonyesha hali hiyo inaweza kumsababisha kupata ulemavu wa kudumu.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake wilaya Kilwa, Tumainieli Mpunga, ameiomba Serikali kuwachukulia hatua za sheria wazazi, walezi na watu wengine walio na tabia ya ukatili dhidi ya watoto, kama alivyofanya Zabibu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Renatha Mzinga alikiri kulifahamu suala hilo lakini hakuwa tayari kulieleza kwa kina kutokana na kuwa nje ya ofisi.