30.8 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

Malori ya mizigo zaidi ya 70 yakwama Misugusugu

Na MWANDISHI WETU-KIBAHA


MALORI zaidi ya 70 yamekwama katika kituo cha forodha cha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Misugusugu mkoani Pwani, huku madereva wakilalamikia hatua hiyo.

Madereva hao wamesema  wamekwama katika kituo hicho kwa zaidi ya siku 10 sasa huku wakikosa taarifa sahihi za lini wataruhusiwa kusafirisha mizigo kupeleka   Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, dereva Christian Urio, alisema   tangu alipopakia mzigo wa mafuta kwenda DRC Oktoba 13, mwaka huu, alijikuta akikwama katika kituo hicho   huku akikosa maelekezo ya kinachosababisha  kuzuiwa kuendelea na safari.

“Hapa tupo magari zaidi ya 70 na kila gari lina dereva na kondakta na kufanya idadi yetu kufikia 140. Tumepaki vizuri mizigo bandarini lakini tangu tulipofika hapa tumekwama tunaomba serikali iingilie kati suala hili.

“Tupo hata fedha zimetuishia chakula sahani moja ni Sh 5,000, huduma ya kuoga Sh 1,000 na kwenda haja ni Sh 500. “Ukiangalia unaona namna tunavyoteseka na hapo bado familia zetu hatujui zinaishi vipi kwa kweli ni mateso,” alisema Urio.

Naye Daud Ahmad, alisema   pamoja na kuzuiwa kwenye kutuo hicho bado maofisa wa TRA waliopo katika kituo hicho wamekuwa hawana kauli ya kuwaambia lini wataondoka zaidi ya kuelezwa kwamba wamekwama kwa sababu ya agizo la Kamishna wa Forodha.

“Tumekwama hatujui la kufanya hivi kama kweli serikali inajali watu wake inashindwa kujua sababu za sisi kukwama.

“Tumechoka na hali imekuwa ngumu hata fedha tulizolipwa tumemaliza tunalala hapa na kuumwa na mbu ndani ya magari hakuna namna,” alisema Ahmad.

Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa Wamiliki wa Malori Wadogo na wa Kati Tanzania (TAMSTOA), Chuki Shabani, alisema  ni vema viongozi wa TRA wafanye uamuzi wakiwa wamejiandaa.

Alisema kitendo cha kuzuia magari hayo Misugusugu na kuwaweka madereva kwa zaidi ya siku 10 ni sawa na unyanyasaji.

“Kazi kubwa inafanywa na Rais Magufuli kuhakikisha analeta wateja kwa ajili ya kutumia badari yetu lakini  wanapoona hivi watakimbia tu. Leo malori yenye mizigo yamezuiwa huku wafanyabishara wa Zambia na Kongo wanaendelea na vikao kujadili hali hii. Jamani watu tusitafute kiki tumsaidie Rais Magufuli kwa kufanya kazi kwa wakati,” alisema

Akijibu malalamiko hayo, Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Mlipakodi, Richard Kayombo, alisema suala la kuzuiwa kwa malori hayo lilitokana na kuondoa mrundikano   bandarini.

“Malori yaliondolewa bandarini  kuondoa msongamano na kupelekwa kwenye kituo cha ukaguzi Misugusugu na hadi kufikia sasa tayari taratibu zimekwisha kukamilika na kesho (leo) malori yote yataendelea na safari.

“Na suala la kusindikizwa kwa malori ni jambo la kawaida kwa sababu  lengo ni kuzuia bidhaa ambazo hazijalipiwa kodi kwa matumizi ya hapa nchini yanakwenda kwenye nchi husika. Lakini ninachoweza kusema malori yote kesho (leo) yataendelea na safari yake,” alisema Kayombo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles