Malipo ya Serikali kufanyika bure kupitia NMB mkononi

0
669
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, akipeperusha bendera pamoja na ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara Ndogo na za Kati, Filbert Mponzi (kulia), kuashiria uzinduzi wa huduma ya NMB Mkononi, Dar es Salaam jana. Wa kwanza kushoto ni Ofisa Mkuu wa Udhibiti Hatari, Victor Rugeiyamu, Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu, Emmanuel Akonay na Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Juma Kimori.

TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM

HUDUMA za malipo ya kodi na tozo mbalimbali za Serikali zitalipwa bila nyongeza ya gharama kupitia huduma mpya ya NMB Mkononi iliyoanzishwa na Benki ya NMB.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya NMB Mkononi iliyofanyika Dar es Salaam jana, Ofisa Mkuu wa Wateja Wadogo na wa Kati, Filbert Mponzi, alisema ankara zitalipwa bure kupitia mfumo wa malipo wa kielektroniki wa Serikali.

Alisema huduma hizo ni pamoja na ushuru wa forodha, ukusanyaji mapato ya ndani kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na tozo zinazokusanywa katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

“Tunakwenda kuirahisishia Serikali kukusanya mapato kupitia huduma hii. Hakutakuwa na malipo ya ziada katika kulipia kodi na tozo mbalimbali,” alisema Mponzi.

Alisema huduma hiyo pia itatoa malipo bila gharama za nyongeza katika kulipia ankara za maji, kulipia vibali na kusajili biashara katika Mamlaka ya Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), malipo ya ankara za umeme, faini za polisi na malipo ya pasi za kusafiria.

Mponzi alisema kutokana na utafiti uliofanywa na Taasisi ya Finscope Tanzania, asilimia 63 ya Watanzania wanamiliki simu za mkononi, hivyo kwa kutumia huduma hii Serikali itawafikia idadi kubwa ya Watanzania katika kukusanya kodi.

Alisema kwa sasa mwananchi anaweza kufungua akaunti ya benki hiyo akiwa popote bila kwenda katika matawi.

Mponzi alisema kupitia huduma hiyo, hata mwananchi aliye kijijini ambako hakuna matawi ya benki hiyo, anaweza kuwa na akaunti na kufanya miamala mbalimbali pasipo kwenda kutafuta matawi ya benki hiyo.

“Wateja wetu wana uwezo sasa wa kufanya miamala mahali popote na muda wowote wanapokuwa bila kwenda katika matawi yetu,” alisema.

Aliongeza kuwa kwa upande wa huduma za kutuma fedha kwenda katika benki nyingine, huduma hiyo imewezeshwa katika NMB Mkononi, kwamba mteja hahitaji kwenda tawini bali atafanya mwenyewe akiwa popote. 

“Mteja anaweza kutuma fedha kutoka benki hiyo kwenda benki nyingine bila kupitia katika tawi la benki, huduma ambayo NMB pekee inaruhusu kufanya hivyo, ambayo hapo awali ilimlazimu kwenda katika tawi kuhudumiwa,” alisema Mponzi.

Alisema kutokana na maombi mengi ya wananchi kuhitaji kubadili bidhaa za benki katika lugha rahisi ya Kiswahili, wameamua kubadilisha bidhaa zao za ‘Mobile banking’ na ‘Click’ kwa kuzihamishia katika NMB Mkononi.

“Asilimia 60 ya Watanzania hawana uelewa wa kusoma na kuandika lugha ya Kiingereza jambo ambalo linawatatiza kupata huduma hizi, hivyo kuhamia katika lugha ya Kiswahili itawarahisisha kuzipata,” alisema Mponzi.

Aliongeza kuwa matumizi ya simu katika kufanya huduma mbalimbali za kibenki,a kumekuwa kukirahisisha maisha kwa wateja wa benki hiyo.

Mponzi alisema kuwa kwa kutumia huduma za kibenki kupitia simu za mkononi, imeisadia benki hiyo kuongeza wateja na kufikia milioni 3.5.

“Benki ya NMB imejenga uwezo mkubwa kwa wateja wake kupitia huduma mbalimbali, ambapo tunavyosherehekea Wiki ya Huduma kwa Wateja kupitia kaulimbiu ya ‘maajabu yanaishi hapa’, wananufaika na huduma zetu,” alisema Mponzi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here