28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MALINZI, VIGOGO SIMBA, MWESIGWA WASOMEWA SHTAKA LA KUTAKATISHA FEDHA

: Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi(kushoto) na Katibu wa shirikisho hilo, Selestine Mwesigwa, wakiwa katika gari la polisi tayrai kupelekwa gerezani baada ya kusomewa mashtaka ya kutakatisha fedha katika Mahakama ya Hakimua Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana. Picha ni viongozi wa Simba wakiwa mahakamani. Picha na Jumanne Juma

PATRICIA KIMELEMETA-DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewapandisha kizimbani vigogo wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Rais, Jamal Malinzi (57), Katibu Mkuu, Mwesigwa Celestine (46) na Mhasibu wake Mkuu, Nsiande Isawayo Mwanga (27) na kuwasomea mashtaka 28 yakiwamo ya kughushi na kutakatisha fedha Dola za Marekani 375,418 sawa na Sh milioni 828.7.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga, alidai katika shtaka la kwanza, washtakiwa Malinzi na Mwesigwa wanadaiwa kuwa kati ya Juni 5, 2016 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kudanganya walighushi nyaraka zinazoitwa ‘Executive Committee Resolution’ zikionesha Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo imebadili mtia saini wa akaunti ya benki kutoka kwa Edgar Leonard Masoud kwenda kwa Nsiande Isawafo Mwanga huku wakijua si kweli.

Shtaka la pili wanadaiwa kuwa Septemba mosi mwaka jana, katika Benki ya Stanbic tawi la Kinondoni, jijini Dar es Salaam, Mwesigwa aliwasilisha nyaraka hiyo ya kughushi inayoitwa ‘Executive Committee Resolution’ ya Juni 5, 2016 inayoonyesha Kamati ya Utendaji ya TFF imebadili mtia saini wa akaunti ya fedha ya shirikisho hilo kutoka kwa Edgar Leonard Masoud kwenda kwa Nsiande.

Katika shtaka la tatu, wakili huyo alidai mnamo Desemba 17, mwaka 2013 huko TFF, Malinzi alighushi risiti namba 308 ya Novemba 6, mwaka 2013 akionyesha amelikopesha Shirikisho hilo Dola za Marekani 9,300 (Sawa na Sh milioni 20.5) wakati si kweli.

Shtaka la nne, Malinzi anadaiwa kuwa Desemba 17, mwaka 2013 katika ofisi hiyo, alighushi risiti namba 322 ya Desemba 17, mwaka 2013 akionesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 10,000 (Sh milioni 22 za kitanzania) wakati si kweli.

Shtaka la tano, Malinzi anadaiwa kuwa Desemba 17, mwaka 2013 katika ofisi ya TFF, alighushi risiti namba 323 ya Desemba 17, mwaka 2013, akionesha amelikopesha shirikisho hilo Dola za Marekani 18,000 (Sh milioni 39.7).

Shtaka la sita, wakili Katuga alidai kuwa Desemba 17, mwaka 2013, Malinzi akiwa kwenye ofisi hiyo ya TFF alighushi risiti namba 324 ya Desemba 17, mwaka 2013 akionyesha amelikopesha shirikisho Dola za Marekani 500 (Sh milioni moja), huku akijua kuwa si kweli.

Shtaka la saba, Malinzi anadaiwa kuwa Desemba 17, mwaka 2013 katika ofisi ya TFF, alighushi risiti namba 325 ya Desemba 17, mwaka 2013 akionyesha ameikopesha Dola za Marekani 1,032 (Sh milioni 2.2) wakati akijua si kweli.

Katuga alidai katika shtaka la nane kuwa Machi 26, mwaka 2014 akiwa katika ofisi hiyo, Malinzi alighushi risiti namba 1956 ya Machi 26, mwaka 2014 akionyesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 40,000 (Sh milioni 88.2).

Wakili huyo wa Serikali alidai katika shtaka la tisa kuwa Machi 13, mwaka 2014 katika ofisi ya TFF, Malinzi alighushi risiti namba 1957 ya Machi 13, 2014 akionyesha amelikopesha shirikisho hilo Dola za Marekani 5000 (Shilingi milioni 11).

Wakili Katuga alidai shtaka la kumi, mnamo Mei 13, mwaka 2014 katika Ofisi ya TFF, Malinzi alighushi risiti namba 1624 ya Mei 13,2014 akionyesha ameikopesha taasisi hiyo Dola za Marekani 40,000 (Sh milioni 88.2) huku akijua si kweli.

Shtaka la 11, Katuga alidai kuwa Mei 16, 2014 akiwa katika ofisi hiyo, Malinzi alighushi risiti namba 1634 ya Mei 16, 2014 akionyesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 10,000 (Sh milioni 22).

Shtaka la 12, Malinzi anadaiwa kuwa Julai 11, 2014 akiwa katika ofisi hiyo ya TFF alighushi risiti namba 1860 ya Julai 11, 2014 akionyesha amelikopesha shirikisho hilo Dola za Marekani 15,000 (Sh milioni 33.1).

Shtaka la 13, Malinzi anadaiwa kuwa mnamo Julai 11, 2014 akiwa katika ofisi hiyo ya TFF alighushi risiti namba 1861 ya Julai 11, 2014 akionyesha ameikopesha taasisi hiyo Dola za Marekani 3,000 (Sh milioni 6).

Inadaiwa kuwa, katika shtaka la 14, mnamo Julai 15, mwaka 2014 akiwa katika ofisi za taasisi hiyo, Malinzi alighushi risiti namba 1863 ya Julai 15, mwaka 2014 akionyesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 14,000 (Sh milioni 30.9).

Alidai shtaka la 15, kuwa mnamo Julai 15, mwaka 2014, Malinzi akiwa katika ofisi ya TFF alighushi risiti namba 1866 ya Julai 15, mwaka 2014 akionyesha ameikopesha taasisi hiyo Dola za Marekani 4000 (Sh milioni 8).

Wakili Katuga alidai katika shtaka la 16, Malinzi anadaiwa kuwa mnamo Julai 25, mwaka 2014 akiwa katika ofisi ya TFF, alighushi risiti namba 1876 ya Julai 25, 2014 akionesha amelikopesha shirikisho hilo Dola za Marekani 1,000 (Sh milioni mbili).

Shtaka la 17, wakili huyo wa Serikali alidai kuwa mnamo Agosti 19, mwaka 2014 huko TFF, Malinzi alighushi risiti namba 1890 ya Agosti 19, mwaka 2014 akionyesha ameikopesha taasisi hiyo Dola za Marekani 5000 (Sh milioni 11).

Katika shtaka la 18, Katuga alidai kuwa mnamo Oktoba 11, mwaka 2014 kwenye ofisi hizo, Malinzi alighushi risiti namba 1568 ya Oktoba 11, mwaka 2014 akionyesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 1,200 (Sh milioni 2.6) wakati akijua si kweli.

Shtaka la 19, Malinzi anadaiwa kuwa Agosti 17, mwaka 2015 akiwa katika ofisi hiyo ya TFF, alikula njama ya kughushi risiti namba 1511 ya Agosti 17, mwaka 2015 akionyesha ameikopesha taasisi hiyo  Dola za Marekani 5,000 (Sh milioni 11).

Naye Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, alisoma shtaka la 20 na kudai kuwa mnamo Julai 22, mwaka 2015 katika ofisi za TFF, Malinzi alighushi risiti namba 2981 ya Julai 22, mwaka 2015 akionyesha amelikopesha shirikisho hilo Dola za Marekani 2,000 (Sh milioni 4.4).

Wakili Swai alidai kuwa katika shtaka la 21 mnamo Mei 9, mwaka jana kwenye ofisi ya TFF, Malinzi alighushi risiti namba 832 ya Mei 9, mwaka jana akionyesha ameikopesha taasisi hiyo Dola za Marekani 7000 (Sh milioni 15.4) wakati akijua si kweli.

Katika shtaka la 22, wakili Swai alidai kuwa mnamo Juni 16, mwaka 2016 katika ofisi ya TFF iliyopo Ilala Dar es Salaam, Malinzi alighushi risiti namba 931 ya Juni 16,2016 akionyesha amelikopesha shirikisho hilo Dola za Marekani 10,000 (Sh milioni 22).

Malinzi anadaiwa katika shtaka la 23, mnamo Agosti 2, 2016 katika ofisi ya TFF, alighushi risiti namba 947 ya Agosti 2, 2016 akionyesha ameikopesha taasisi hiyo Dola za Marekani 1,000 (Sh milioni 2.2).

Wakili Swai alidai katika shtaka la 24, mnamo Septemba 19, 2016 katika ofisi ya TFF, Malinzi alighushi risiti namba 1029 ya Septemba 19, 2016 akionyesha ameikopesha taasisi hiyo  Dola za Marekani 1,000 (Sh milioni 2.2).

Swai katika shtaka la 25, anadai kuwa Septemba 22, 2016 katika ofisi ya TFF, Malinzi alikula njama ya kughushi risiti namba 1071 ya Septemba 22, 2016 akionyesha amelikopesha shirikisho hilo Dola za Marekani 15,000 (Sh milioni 33.1).

Alidai kwenye shtaka la 26 kuwa kati ya Septemba mosi na Oktoba 19, 2016 washtakiwa, Malinzi, Mwesigwa na Nsiande kwa kushirikiana pamoja walitakatisha fedha kiasi cha Dola  375,418 (Sh milioni 828.7) huku wakijua fedha hizo ni zao la kughushi.

Alidai, shtaka la 27, Malinzi na Mwesigwa katika kipindi hicho cha Septemba mosi na Oktoba 19, 2016, wakiwa katika benki ya Stanbic tawi la kati la Kinondoni walijipatia Dola za Marekani 375,418 (Sh milioni 828.7), wakati wakijua fedha hizo zimetokana na kughushi.

Katika shtaka la 28, linalomhusu mshtakiwa Nsiande, anadaiwa kati ya Septemba mosi na Oktoba 19, 2016 katika ofisi ya TFF alimsaidia Malinzi na Mwesigwa kujipatia Dola za Marekani 375,418 (Sh milioni 828.7) kutoka Benki ya Stanbic, huku akijua upatikanaji wake umetokana na kughushi.

Baada ya washtakiwa hao kusomewa mashtaka hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa, aliiambia mahakama kuwa upelelezi bado haujakamilika.

Hata hivyo, jopo la mawakili wa upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Jerome Msemwa na Aloyce Komba waliiomba mahakama hiyo kuwapatia dhamana washtakiwa hao.

Mawakili wa Serikali Waandamizi, Mutalemwa, Msigwa na Pius Hilla walipinga dhamana kwa washtakiwa hao kwa madai kuwa mashtaka yanayowakabili washtakiwa yakiwamo ya utakatishaji fedha kisheria hayana dhamana.

Aidha, Hakimu Mashauri aliiahirisha kesi hiyo hadi Julai 3 ,mwaka huu ambapo atatoa uamuzi kama washtakiwa hao watapata dhamana au la na washtakiwa hao wamepelekwa rumande.

Aveva, Kaburu wapandishwa kizimbani

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, pia iliwapandisha kizimbani Rais wa Klabu ya Simba, Evans  Aveva na Makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na kuwasomea mashtaka matano yakiwemo ya kughushi na kutakatisha fedha kiasi cha Dola za Marekani 300,000 sawa na Sh milioni 662.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu, Victoria Nongwa, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Christopher Msigwa alidai kuwa Machi 15, 2016 katika Jiji la Dar es Salaam, washtakiwa hao walikula njama ya kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha fedha za Klabu ya Simba iliyoonyesha inalipa mkopo wa Dola za Marekani 300,000 kwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Evans Aveva, huku wakijua kuwa si kweli.

Wakili Msigwa alidai shtaka la pili linaonyesha kuwa Machi 15, 2016 katika Benki ya CRDB tawi la Azikiwe Ilala, alitoa nyaraka za uongo ambazo ni fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15, 2016 wakati akijua ni kosa.

Shtaka la tatu la utakatishaji wa fedha linalowahusu washtakiwa wote ambapo wanadaiwa kuwa kati ya Machi 15 na Juni 29, 2016 jijini Dar es Salaam, kwa pamoja walikula njama ya kutakatisha fedha kwa kupata USD 300,000 wakati wakijua ni zao la uhalifu.

Kwa upande wa shtaka la nne pia la kutakatisha fedha linalomhusu Aveva peke yake, ilidaiwa kuwa kati ya Machi 15, 2016 katika benki ya Barclays iliyopo Mikocheni jijini Dar Es Salaam  alijipatia Dola za Marekani 300,000 sawa na Sh milioni 671 wakati akijua zimetokana na kughushi.

Shtaka la tano la kutakatisha fedha linalomuhusu mshtakiwa Nyange, anadaiwa kuwa Machi 15, 2016 katika Benki ya Barclays tawi la Mikocheni jijini, alimsaidia Aveva kujipatia Dola za Marekani 300,000 (Sh milioni 671), wakati akijua fedha hizo zimetokana na kughushi.

Licha ya washtakiwa hao kukana mara baada ya kusomewa mashtaka hayo, lakini upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika na washtakiwa hao wamepelekwa rumande kwa kukosa dhamana kutokana na kwamba makosa ya kutakatisha fedha hayana dhamana ambapo pia kesi iliahirishwa hadi Julai 13, mwaka huu.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa TFF, Wakili Revocatus Kuuli alieleza kuwa, iwapo mgombea atashindwa kutokea katika siku tatu zilizotengwa kwa ajili ya usaili, atapoteza sifa ya kuwa mgombea.

Malinzi na Kaburu ni wagombea wa nafasi za Urais na Makamu katika uchaguzi huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles