MALINZI MGUU NJE NDANI UCHAGUZI TFF

0
881
Rais wa TFF Jamal Malinzi
Rais wa TFF Jamal Malinzi

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imesema bado inaendelea kuwashikilia viongozi wa juu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Rais Jamal Malinzi na Katibu Mkuu wake, Selestine Mwesigwa, hadi watakapojiridhisha na uchunguzi wao.

Takukuru waliwaweka viongozi hao chini ya ulinzi tangu juzi usiku kwa madai ya kuwahoji kutokana na uchunguzi wanaoendelea nao.

Kwa muda mrefu kumekuwepo na tuhuma mbalimbali dhidi ya viongozi hao kuhusu matumizi mabaya ya fedha za TFF na inadaiwa Takukuru wamekuwa wakiwafuatilia kwa kipindi chote hicho kabla ya kuwatiwa nguvuni.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Takukuru, Mussa Misalaba, alisema uchunguzi wa viongozi hao ni wa muda mrefu hivyo wataendelea kuwahoji  hadi watakapojiridhisha kabla ya kuamua kuwaachia au kuwapeleka mahakamani Kisutu kutokana na matokeo ya uchunguzi huo.

“Ni kweli tunaendelea na uchunguzi dhidi ya viongozi mbalimbali wa TFF, uchunguzi huo tumekuwa nao kwa muda mrefu lakini kuhusu sababu za kuwashikilia, bado ni siri yetu upande wa uchunguzi, katika suala hili tunaongozwa na misingi ya sheria, kanuni na taratibu hatuwezi tukaweka wazi kila jambo.

“Tunaowashikilia bado tuko nao chini ya ulinzi wetu, tunaongozwa na sheria tutakapopata tunachokitaka tutawaachia bila kuchelewa kwani ushahidi ndio utakaoamua,” alisema Misalaba.

Mbali na viongozi hao, Takukuru ilimhoji Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF.

Wakati hayo yakitokea, Kamati ya Uchaguzi Mkuu wa TFF leo inatarajia kuendelea na mchakato wa mchujo kwa muda wa siku tatu baada ya kupokea mapendekezo na pingamizi kutoka kwa wagombea.

Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu mjini Dodoma na Malinzi anatetea nafasi yake dhidi ya Imani Madega, Wallace Karia, Fredrick Masolwa, Fredrick Mwakalebela, John Kijumbe, Shija Richard, Ally Mayay na Emmanuel Kimbe.

Waliojitokeza kuwania nafasi ya Makamu wa Rais na kurejesha fomu ni Mulamu Ng’hambi, Michael Wambura, Geofrey Nyange, Mtemi Ramadhani, Robert Selasela na Stephen Mwakibolwa.

Akizungumzia suala la kushikiliwa kwa Malinzi, Mwenyekiti wa Uchaguzi wa TFF, Wakili Revocatus Kuuli, alisema tuhuma haziwezi kumuondolea sifa mgombea hadi Mahakama itakapomtia hatiani na kuhukumiwa kifungo cha zaidi ya miezi sita ambacho hakitakuwa na dhamana.

“Kutuhumiwa tu haitoshi kumuondolea sifa mgombea, labda ahukumiwe kifungo cha zaidi ya miezi sita ambacho hakina dhamana, hapo tunaweza kumuondoa katika orodha ya wagombea kwa kuwa hana sifa za kuwa mgombea,” alisema Kuuli.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here