Na Clara Matimo, Mwanza
Mkuu mpya wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima amepokelewa Agosti 3, katika ofisi yake na kuanza rasmi majukumu mkoani humo.
Akizungimza na watumishi wa umma, kamati ya amani ya viongozi wa dini, wazee maarufu na baadhi ya viongozi wa taasisi binafsi waliofika kumpokea baada ya kusaini hati ya makabidhiano baina yake na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi Robert Gabriel, amesema kipaumbele chake cha kwanza ni ulinzi na usalama.
Amesema ili mkoa huo ukue zaidi kiuchumi na kijamii kama alivyoagizwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Agosti Mosi, mwaka huu baada ya kuapishwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza akitokea Mkoani Tanga amani na utulivu ndiyo silaha ya kwanza na muhimu itakayowapa fursa wakazi wa mkoa huo pamoja wa wafanyabiashara kufanya shughuli zao bila hofu.
“Rais Samia Suluhu Hassan hakuniagiza mambo mengi aliniambia “Mwanza ni sehemu kubwa kiuchumi na kijamii, nenda ukasimamie iwe kubwa zaidi,” hayo ndiyo maneno aliyoniambia Mheshimiwa rais hivyo nami naomba tushirikiane ili kutimiza agizo hili la rais.
“Watumishi wenzangu pamoja na makundi mbalimbali nitakayoongea nayo siku za hivi karibuni wakiwemo wafanyabiashara, naomba tuwe wabunifu ili kuleta maendeleo ndani ya mkoa wetu, lazima tuutazame Mkoa wa Mwanza kama mkoa wa kimkakati na uzalishaji,” amesema Malima.
Aidha, Malima amewataka viongozi wa kada mbalimbali mkoani humo pamoja na watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao kwa kufuata maadili ya utumishi wa umma wakitambua kwamba wanawajibika kwa wananchi vilevile wafanye kazi ambayo inatarajiwa na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na watanzania.
“Baadhi ya watumishi tuna tabia tunapopata hizi nafasi tunaona tuko juu hizi nafasi hazinaga mwenyewe tuwe wanyenyekevu tumuogope Mwenyezi Mungu,” amesema Malima.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Mstaafu, Mhandisi Gabriel amewataka watumishi wa umma wa mkoani humo kutekeleza majukumu yao kwa kumtanguliza Mwenyezi Mungu, waipende nchi yao pamoja na kumheshimu Rais Samia.